Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na kwa sababu ya muda itabidi niende haraka haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono taarifa ya Kamati zote mbili kwa asilimia mia moja. Pili, suala hili amelizungumza mwanangu Ndassa lakini kalizungumza kwa Kisukuma sikulielewa vizuri. Tunachokitaka maazimio tuyayoyapitisha katika Bunge hili yaundiwe Kamati ambayo itayasimamia. Kwa sababu hivi sasa tunapitisha tukiondoka hapa yamepita, tukirudi tena hakuna aliyenayo, hayasimamiwi, hatujui Serikali imetekeleza lipi na imeacha lipi. Kenya wana mfumo huu, kwa hiyo, iundwe Kamati ya Bunge ambayo itakuwa inasimamia maamuzi na maazimio yanayopitishwa na Bunge, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme tu mimi sijui tuna laana gani sisi Watanzania na miaka 60 ya Uhuru sasa tunayokwenda nayo bado tuna matatizo ambayo sisi wenyewe tunajitakia. Wizara ya Ardhi sasa hivi na hii Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Maji tutaendelea kuzilaumu kila siku kama hatuzipatii fedha zikafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi anafanya kazi vizuri, lakini anakwama kwa sababu ya fedha. Sasa atalaumiwa kila siku, watu watapigana, watauana kwa sababu anashindwa kupima ardhi kwa sababu ya fedha, apewe fedha afanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara hii ya Kilimo ya Mpina kama hawajapewa fedha hawa za kutosha hatuwezi. Kama hatujapanga leo maana niseme sijui tuna laana gani Libya walikuwa wanachukua maji kutoka Mto Nile ambao umeanzia kwetu wanajitosheleza kwa chakula na matunda yote siye Tanzania tuna mito na maziwa mangapi hapa tunashindwa, tupange fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabia nchi yanayojitokeza katika nchi yetu, mwaka huu mahindi hayana bei, mbaazi hazina bei, tumbaku haina bei na vitu vingi tu. Mwakani hapa mabadiliko ya tabia nchi tutakuwa na dhiki ya chakula kama wangepewa fedha hawa wakanunua hivi vyakula wakaweka katika Hifadhi ya Taifa vingetufaa mwakani kukitokea tatizo, hakuna, fedha tunakusanya hatujui. Kwa hiyo, hebu tukaeni chini sasa kama Watanzania jamani tunataka nini, tujipange miaka 60 inatosha si watoto tena katika Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni misitu. Naomba Serikali misitu yote nchini isimamiwe na taasisi au mamlaka moja, halafu hiyo mingine iendelee tu, ile ya kijiji ibaki kuwa ya kijiji, ya Halmashauri ibaki kuwa ya Halmashauri lakini kuwe na msimamizi mmoja ili zile sheria zinazohusiana na masuala haya ya misitu zisimamiwe. Tanzania nadhani tunapoteza hekta laki tatu na nusu kila mwaka kwa matumizi tofauti lakini upandaji wetu sidhani kama tunafika hata hekta laki moja kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukichukulia hilo na hiyo miti ambayo ni fast growing trees ukiipanda inaweza ikachukua zaidi ya miaka sita ndiyo unaanza kuvuna, nchi yetu baada ya miaka 20 ijayo tutakuwa katika hali gani? Sasa kama sisi tunavimba kichwa kusema kwamba tuna asilimia 35, sijui 52 ya misitu katika nchi yetu lakini na matumizi ni makubwa, ongezeko kubwa la watu mahitaji ni makubwa.

Kwa hiyo, ni lazima matumizi yetu yaendane na upandaji wetu na tuone kwamba mti tukiupanda leo hatuvuni leo rahisi kabisa ni baada ya miezi sita, kwa hiyo, lazima tuwe makini katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala lingine, Mheshimiwa Musukuma kamzungumzia sana Waziri Mpina, mimi nampa tena ushauri Mheshimiwa Waziri wa Maliasili. Mheshimiwa Waziri nilikupa ushauri ndani ya Kamati, nakupa ushauri leo ndani ya Bunge. Nikwambie Wizara hii ya Maliasili na Utalii ni yai viza. Yai viza lina matumizi mazuri sana kwa wanaolitumia lakini yai viza ukilikosea linanuka vibaya sana. Nikushauri tu Mheshimiwa Waziri uwe mtulivu, hii Wizara haitaki amri, haitaki nguvu, haitaki ubabe na haitaki hasira, hii Wizara ni lazima utulie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa nawashauri humu ndani kwamba ndani ya Wizara hii lazima mkae mafiga matatu. Community iseme inataka nini, Serikali iseme inataka nini, mwekezaji aseme anataka nini, nyote watatu mkae mseme mnataka nini ili mwende kwa pamoja. Sasa ukichukulia nguvu ukasema leo kwamba kwa mfano tu, nafunga vitalu vya uwindaji, kesho unasema nawaachia mwaka mmoja, kesho kutwa nawaachia miaka miwili, hii biashara ni nyepesi sana kuharibika na ndiyo nikasema ni yai viza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima utulie vizuri sana na hizi figure tatu, hii triangle zikae kuweka mkakati wa tunakwenda vipi vinginevyo utakuwa ni Waziri ambaye umetumikia Wizara hii muda mfupi sana. Kwa sababu imebeba uchumi wa Taifa letu, ukikoroga kidogo tu katika sekta hii unakoroga system nzima ya utalii na ukikoroga system nzima ya utalii umekoroga uchumi wa nchi yetu ambao asilimia sasa hivi zaidi ya 20 inatokana na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikushauri ukae vizuri, uwe makini, tupo ambao tumeshafanya kazi katika sekta hii, tupo ambao tumesoma, tutakushauri vizuri kwa nia safi kabisa ili twende mbele. Suala hili la kutumia nguvu ukaona labda ni sifa unapotumia nguvu si sifa unajiharibia na ukijiharibia wewe, unaliharibia Bunge, unaiharibia Serikali na unaiharibia nchi yote ya Tanzania. Kwa hiyo, nakushauri tu kwamba utulie vizuri sana sisi tutakusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala lingine la wawekezaji. Mtu ameshapewa vibali vyote vya kujenga lakini kuna tatizo la hii Environmental Impact Assessment inachelewa, mwekezaji anakaa miaka miwili, mitatu hajapewa hiyo, sasa atajenga lini huyu? Kwa hiyo, hili benchi la kutoa vibali vya ujenzi bora lote likae pamoja ili mwekezaji akipata kitu apewe kwa pamoja anaenda kuwekeza tujue kwamba mwekezaji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji akishawekeza labda kwa miaka mitatu amejenga anahitaji tena miaka miwili kufanya marketing kupata wageni hapa. Kwa hiyo, naomba sana Serikali itulie vizuri, ijipange, muda unatosha, tuko tayari kuishauri vizuri Serikali kwa minajili ya faida ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.