Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami nipongeze Kamati zote mbili lakini nitajikita kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na naomna nianze na suala la Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali kuihuisha Sheria ile ya mwanzo ya mwaka 1959, Ordinance Na. 413 ya mwaka 1959, nasema imepitwa na wakati kwa sababu zifuatazo:-

Kwanza, tukumbuke kipindi kile cha mwanzo wenyeji katika eneo hilo walikuwa ni 8,000 lakini kwa sensa ya hivi karibuni wenyeji wamefikia 93,851. Kama haitoshi, kiwango cha kutojua kusoma ni zaidi ya asilimia 70 kwa maana ya takwimu za mwaka jana. Pale ndani kuna shule 21 za msingi na mbili za high school, hiki ni kigezo cha kuonyesha kwamba watu hawa wanakuwa masikini. Pamoja na kiwango hicho cha elimu kule ndani magonjwa yameongezeka na kuna ukame na kwa sababu hiyo naendelea kujenga hoja ya kwamba hii sheria imepitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, naomba nije kwenye suala zima la utalii. Kumuunga mkono Rais wetu ni kwa maana ya kuunganisha mawazo ya kuiletea nchi mapato, napenda kusema kwamba eneo hili la utalii ni sensitive, nikimuongelea mtalii kwa ujumla wake maana yeye anaweza asije Tanzania akaenda sehemu nyingine yoyote. Ndiyo maana eneo hili la utalii kwa lugha ya kigeni wanaita ni hospitality industry.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunatakiwa kuwa watu rahimu, tukicheza watalii hawa wanayo nafasi ya kwenda maeneo mengine, mbuga ziko maeneo mengine. Kwa hiyo, naomba sana na katika hili niendelee kumshauri Waziri husika tunatakiwa kuwa watulivu kwa maana hatuko peke yetu katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoke hapo, niende kwenye eneo la matangazo kwa maana ya TANAPA na TTB. Ndiyo maana kwa mfano wenzetu wa Coca Cola sehemu nyingine kubwa wameingiza fedha kwa maana ya matangazo. Nami niombe, kazi nzuri ambayo imeendelea kufanywa kwa maana ya matangazo waiendeleze ndugu zetu wa TANAPA na TTB.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaunga mkono, najua mara ya mwisho kulikuwa na kitu kinaitwa SITE (Swahili International Tourism Expo) waliifanya mwaka jana na ilikuwa nzuri kwa sababu imeendelea kuwaita tour operators kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la matangazo naendelea kuisihi Serikali yangu, inatia huruma kuona kwa mfano, majirani wana-take advantage ya vyanzo tulivyonavyo. Mtu aseme njoo sehemu fulani utauona Mlima Kenya, kwa nini na sisi Watanzania tusiendelee kuchangamkia fursa hii, kama vyanzo ni vya kwetu kwa nini watu wengine watumie nafasi ya vyanzo vyetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo la wazawa waendelee kusaidiwa kwa maana ya biashara nzima ya utalii na uwindaji lakini naomba kuboresha najua ukanda wa Kaskazini tunaendelealea kuboresha maeneo hayo lakini watalii kwa ujumla wake kulikoni tukawapoteza tuendelee kuwafanya waje nchini kwa kuboresha na kanda nyingine kama Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo ukisema Kanda ya Magharibi, Mbuga kama ya Katavi tunayo nafasi ya kutoka Ruanga na Burundi wakipita Kigoma, wakaja kushangaa mbuga yetu nzuri ya pale Katavi. Kwa hiyo, naomba ukanda huo uendelee kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusijikite tu kwa maana ya suala la mbuga hizi, tufungue vyanzo vingine kama fukwe, masuala ya utamaduni na mapango. Tulikwenda kuyaona mapango ya Amboni pale Tanga. Watanzania kwa ujumla wake tuna vyanzo vingi ni suala tu la kupanga tunaanza na nini tunamaliza na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Olduvai, naomba suala la maabara pamoja na maktaba ziendelee kufanywa za kisasa ili wanafunzi wetu waendelee kwenda pale kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho kabisa, eneo la Saadani. Hii Mbuga ya Saadani kwanza wanasema unakwenda katika eneo ambalo nyika zinakutana na fukwe. Kwa hiyo, ina sura ya pekee sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mgogoro wa kijiji kimoja kilichopo pale, naomba Serikali ifanyie kazi ili ile Mbuga ya Saadani iendelee kutoa mafao makubwa kwa maslahi mapana ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa maana ya Sera ya Taifa ya Misitu, naomba tuendelee kuiboresha hiyo kwa sababu pasipo kuwepo na misitu hata huu utalii wote tunaouzungumzia haupo. Vilevile pasipokuwa na misitu hata masuala mengine mipango mingine tunayoikusudia kuifanya kama ya umwagiliaji na mambo mengine itakuwa ni kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.