Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kabisa nianze kwa kuzipongeza Kamati zote kwa uwasilishaji mzuri. Pili, ningependa pia kuipongeza Kamati ya Maliasili ambayo imeona umuhimu wa mapango ya Amboni na kuishauri Serikali kuyafanyia ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Tanga una vivutio vingi sana ambavyo vilikuwa vinausaidia mkoa wetu kuinuka zaidi kiuchumi, lakini kwa sasa vivutio hivyo vimekuwa kama vimetelekezwa. Hivyo, ninaishauri Serikali kupitia upya vivutio hivi na kuona inafanya nini ili kurudisha ile hadhi ya Mkoa wetu wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine napenda kuchangia kuhusu migogoro ya ardhi. Hapa katika migogoro ya ardhi, ukiangalia sana chimbuko linakuwa ni Serikali ambazo ziko kule vijijini hasa viongozi wa Serikali za Vijiji. Viongozi hawa wamekuwa wakiuza ardhi za wananchi bila kuwashirikisha na kusababisha migogoro mikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekuwa wakikosa ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, hivyo kupeleka wenyewe kwa wenyewe kugombana na kusababisha uhasama mkubwa baina ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie na kudhibiti hivi vyanzo vya migogoro ya ardhi hasa kwa hawa Wenyeviti wa Serikali kwa kuwachukulia hatua ambazo zitasababisha waache hii tabia ya kuuza ardhi na kusababisha wananchi kushindwa kuendeleza kilimo chao ambacho ndiyo sehemu kubwa ya utegemezi ya kukuza uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine na mimi naomba kuchangia kuhusu maji. Wewe mwenyewe umekuwa shahidi hapa, kila Mbunge anayesimama analia kuhusu maji katika eneo lake. Maji ni kama uti wa mgongo, hakuna shughuli yoyote inayoweza kuendelea bila uwepo wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia viwanda, lazima kuwe na maji, tukizungumzia afya, lazima kuwe na maji na hata kilimo hakiwezi kuendelea bila uwepo wa maji. Mathalani mkoa wetu wa Tanga una vyanzo vya maji kama Ruvu na Pangani, lakini bado tatizo la maji limekuwa ni kubwa sana. Naishauri Serikali ingalie sehemu zile ambazo zina vyanzo vya maji iweze kuvitumia ili kupunguza haya matatizo ya maji kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna miradi mikubwa ambayo bado Serikali inaitekeleza, nilikuwa naishauri Serikali, wakati inatekeleza miradi hiyo, iangalie njia mbadala za kuwasaidia wananchi kama kuchimba mabwawa na visima ili waweze kujikimu wakati wanasubiri utatuzi wa kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niongelee kuhusu kilimo. Kipindi cha nyuma tulikuwa tunaona watu ambao wanajikita kwenye kilimo zaidi ni wazee, lakini kwa sasa tunaona asilimia kubwa ya vijana nao wameamua kuingia kwenye kilimo. Kwa hiyo, naishauri Serikali iwape motisha hawa vijana ili wasirudi nyuma kwa kuwapatia mitaji, kuwasaidia kupata masoko, kuangalia miundombinu, kuwapatia elimu ya nini walime na kwa wakati gani na kutokana na ardhi iliyoko katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda ni muhimu sana. Kwa mfano, Mkoa wetu wa Tanga, vijana wanalima matunda kwa wingi, lakini yale matunda yamekuwa yakiozea mashambani kwa sababu hakuna viwanda vya kuweza kusindika yale matunda. Iwapo watakuwa na miundombinu mizuri, watapatiwa viwanda vya kuwasaidia kusindika mazao yao, nina imani wale vijana hawatarudi nyuma na tutaondoa Taifa la wazembe na tutakuwa na Taifa la wachapakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba Serikali iangalie kuhusu suala la pembejeo. Wakulima wawezeshwe kuhusu pembejeo, pia zipatikane kwa wakati ili waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zinapotokea ahadi, kwa mfano, kama kipindi walichoambiwa walime mbaazi na kwamba zitakwenda kuuzwa India na ikashindikana, Serikali ni lazima ije na mpango mbadala kuliko kuwaachia wananchi ule mzigo wa mazao kuwaaharibikia mikononi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante.