Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu pale ambapo rafiki yangu na ndugu yangu Mheshimiwa Nape alipoishia. Alipoanza kutoa takwimu nyingi za kuhusu wafugaji kunyanyaswa nchi hii, labda kukumbusha tu wiki mbili zilizopita Kamati hii ya Ardhi Maliasili na Utalii ilizuia Muswada ambao ulikuwa unakuja kwa ajili ya kuwaadhibu wafugaji tena ya kum-charge kila mfugaji, kwa mfugo mmoja kama ni ng’ombe au mbuzi shilingi 100,000 wanapoingia kwenye hifadhi ya wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi naipongeza sana Kamati hii kwa kufanya juhudi kubwa na kuzuia jaribio hilo baya kwa ajili ya wafugaji tena wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu nyingine, jana Mahakama ya Wilaya ya Same imetaifisha ng’ombe 36 wa wafugaji. Ni ongezeko la takwimu ambazo ametoa kaka yangu Mheshimiwa Nape na mimi naomba Bunge hili liangalie sasa kwa historia ya nchi hii wafugaji kunyanyaswa kwa muda mrefu. Hii imekuwa sasa ni too much! Naomba mtusaidie ili haya mambo yaishe, maana wakati Mheshimiwa Jaji Nyalali akihukumu ile kesi ya Mkomazi miaka fulani na hukumu yake naijua vizuri sana, mfugaji aliyehamishwa kwenye mbuga ile alilipwa shilingi 250,000; yaani haya ni manyanyaso ya miaka ya 1990 mpaka sasa hivi, wafugaji wanaendelea kutaabika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tu suala la Kamati, kwenye ukurasa wa 14 Kamati imeongelea suala la Ngorongoro na wanasema hivi: “Kuna uharibifu wa vyanzo vya maji, uoto wa asili unaosababishwa na ongezeko la binadamu Ngorongoro tangu mbuga ile iamuliwe kuwa mbuga mwaka 1956, maana wakati ule wakazi walikuwa 8,000 na sasa wako 93,000, kwa hiyo, kuna upungufu wa watalii kwenye Mbuga ya Ngorongoro.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni uongo mkubwa na mwendelezo wa Serikali hii kuwaumiza wafugaji. Kwa nini nasema hivyo? Mwaka 2014 takwimu sahihi zilizopo Ngorongoro ongezeko la mapato ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, imeongezeka shilingi bilioni 63 na mwaka 2017 ni shilingi bilioni 102. Hili hata Mheshimiwa Waziri Maghembe alikiri, Kamati inajua, imepewa mpaka taarifa na Chama cha Wafugaji wa Ngorongoro, lakini Kamati hii haijataka kunukuu kwa makusudi ya kutaka kupotosha kwa sababu hawataki kuwasaidia wafugaji wa Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu barua waliyopewa ya tarehe 8 Machi, 2017. Serikali hii inaingia kwenye record tangu Uhuru wa nchi hii kuwanyanyasa wafugaji na wakulima kwa vitendo. Naomba data hizi ambazo zipo na Kamati imekabidhiwa, wafugaji wa Ngorongoro wameonewa vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mwaka 2013 Hifadhi hii ya Ngorongoro, Mamlaka ya Ngorongoro iliibuka mshindi wa Umoja wa Mataifa baada ya maajabu ya saba ya asili inaitwa One of the Natural Wonders of Africa, kwa sababu wafugaji na wanyamapori wanaishi sehemu moja, lakini najua target ya Serikali ni kutaka kuwaondoa wafugaji wale. Tunaomba kwenye Bunge hili muwasikilize wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Nape kwamba kwa mara ya kwanza tuunde tume itakayoshughulikia masuala ya wafugaji na uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la mipaka. Kama hoja ya Kamati inavyosema, kuna maeneo mengi ambayo yalitolewa kwa wanyang’anyi wa nchi hii, kuna ranchi nyingi nchi hii zilitolewa kwa wafanyabiashara. Kwa nini msiwarudishie wafugaji ili tuendelee na sisi kupata maeneo ya wafugaji? Kwa mfano, kama mmechukua Tarangire sehemu fulani, mtupe mbuga yoyote au eneo lolote, kama ni Kongwa au Kilimanjaro na sisi wafugaji tupewe na maeneo ya kufugia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la maji. Inasikitisha sana, mamlaka inayodaiwa kuliko yote ni mamlaka za Serikali na ninyi mmeshindwa kuzilipisha. Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)