Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo kwenye hii mada iliyoko mezani. Kwanza naomba tu niungane na Waheshimiwa Wabunge na hasa Wajumbe wa Kamati hizi mbili kwa taarifa walizotoa na kimsingi nakubaliana na mapendekezo yao kwa maana ya maazimio ambayo wameyaweka kwenye ripoti zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, na mimi naomba ni-register masikitiko yangu kwa jinsi ambavyo mambo yanakwenda kwenye sekta hii. Mwaka 2017 nilifanya ziara kwenye jimbo langu kujionea hali ya mazao kwa wakati ule, nilikumbana na tatizo kubwa la funza. Nilichukua kumbukumbu na niliwasiliana na Wizara kueleza kwamba kuna mdudu ambaye ametokea kipindi kile ambaye anaharibu sana mazao ya wakulima na tukaomba kwamba ni vizuri Serikali ikatoa mwongozo wa dawa gani itumike kukabiliana na mdudu huyu. Hatua hazikuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu 2018 mdudu yule amesambaa mikoa karibu 10 sasa nasikia taarifa, mpaka maeneo ya Kilimanjaro amefika, wakulima wa mahindi karibu wote ambao wamelima hii awamu ya pili, hizi mvua za pili zinazoendelea kwa mfano, katika Mkoa mzima wa Shinyanga, hawatapata mazao yao vizuri. Nilikuwa naomba sana, siyo vizuri kugombana hasa kwa watu mnaoheshimiana kama ambavyo sisi Wabunge tunavyoheshimiana na Mawaziri wetu na Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapopata nafasi, aeleze ni hatua gani ambazo zimechukuliwa kukabiliana na mdudu huyu. Pamoja na kwamba mwaka huu na mwaka 2017 tumeshapoteza mazao, lakini angalau tatizo lisiwe endelevu kutokea tena mwaka unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu tatizo la pembejeo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alipokuja na pendekezo hapa la kuanzisha bulk procurement ya mbolea, lilikuwa ni jambo ambalo Wabunge wengi tulilikubali, lakini maelezo aliyoyatoa wakati ule hayajatekelezwa kikamilifu katika level ya implementation. Mheshimiwa Waziri alituahidi kwamba atakuwepo mnunuzi mmoja wa mbolea atakayepata kazi ile, atakayetoa bei ya chini kuliko washindani wote na atakuwa na mawakala kwenye maeneo yote na mawakala wale watatangazwa, watajulikana na bei elekezi zitatolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama atuambie, Wakala wa Mbolea au wa Pembejeo kwa Wilaya ya Kahama ni nani, anauza mbolea kwa kiasi gani kwa kila mfuko? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inavyoonekana ilikuwa ni gear kwa ajili ya hoja ile ikubalike, lakini utekelezaji wake umeachiwa njiani. Nilikuwa naomba sana maeneo haya Mheshimiwa Waziri aje atusaidie. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono mapendekezo ya Kamati zote mbili. Ahsante sana.