Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa jinsi inavyotekeleza majukumu yake. Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri wote na Watendaji wote wa Serikali kwa kuwa na sense of duty.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha chai; zao la chai ni zao ambalo lilikuwa linaingiza fedha nyingi za kigeni miaka ya 1970 na kabla ya miaka 1990. Mfano, chai ya Lupembe ipate soko kubwa na ikawa namba moja kwa ubora duniani. Katika miaka ya hivi karibuni baada ya kukaribisha wawekezaji uzalishaji ukapungua na kupelekea kupoteza soko lake. Hii ni kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri wa zao hili. Tunaomba Serikali ione umuhimu wa kusaidia kufufua zao hili kwani kwa Mikoa ya Njombe, Mbeya na Tanga zao hili huajiri watu wengi sana mashambani na viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu kwa Serikali kufuatilia uzalishaji wa zao hili toka shambani mpaka sokoni, mchakato mzima toka uhudumiaji wa shamba, uchumaji, namna biashara inavyofanyika toka kwa mkulima na wenye viwanda na uzalishaji wa majani mabichi, kwa majani makavu na hatimaye soko lake la nje. Ilivyo sasa wakulima wadogowadogo wanadhulumika sana kupitia mizani wanayopimia mashambani. Chai ikizalishwa zaidi ya mahitaji ya viwanda, wakulima wanaambiwa chai ni chafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei ya chai. Bado bei elekezi ni ndogo sana, hivi karibuni bei iliyotangazwa ni ongezeko la Sh.35 hivyo kupanda toka Sh.230 mpaka Sh.250 na Sh.265 mpaka Sh.285 kwa majani mabichi. Bei hii haimnufaishi mkulima, gharama za uzalishaji ni kubwa kuliko gharama za kuzuia majani mabichi. Kwa sasa hivi, gharama za kuzalisha kilo moja ya majani mabichi takriban au wastani wa Sh.400 mpaka Sh.450 lakini bei ya kuuzia majani mabichi ni Sh.230 mpaka Sh.250. Bei hii ni bei nyonyaji kwa wakulima. Naomba Serikali hasa Wizara ya Kilimo kusimamia na kufuatilia bei ya zao hili la chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya kuelekea kwenye maeneo ya uzalishaji chai. Barabara zinazoelekea kwenye mashamba ya chai ni mbovu sana, barabara hazipitiki wakati wa mvua. Hii pia inachangia kupoteza ubora wa chai. Zao hili la chai huzalishwa kwa wingi wakati wa mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huu ili kupata ubora wa zao hili barabara zilitakiwa ziwe nzuri lakini mara nyingi zimekuwa hazitengenezwi. Serikali iangalie uwezekano wa kuwa na mfuko rasmi wa barabara za maeneo ambako chai inazalishwa kama ilivyokuwa zamani, wakati wa Mamlaka ya Chai, barabara za mashamba ya chai zilitengenezwa na fedha kutoka World Bank na ndipo chai ilipopata ubora mzuri katika soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbolea. Bado kuna tatizo kubwa katika usambazaji wa mbolea. Mfano, katika Mkoa wa Njombe bei ya mbolea pamoja na kutangaza bei elekezi bado kumekuwa na ujanja ujanja wa mawakala wadogo wa mbolea. Kilichotokea mbolea hizi zilifika kwa wakati katika Miji ya Njombe na Makambako na zimekuwa zikiuzwa kwa bei elekezi yaani Sh.44,000 (CAN), mpaka elfu Sh.52,900 (UREA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mbolea hizi hazijawahi kupelekwa vijijini na kuuzwa kwa bei hizo, wafanyabiashara wanasema hawawezi kupeleka maeneo ya Lupembe, Kichiwa na maeneo ya vijiji vilivyo nje ya barabara ya lami. Mbolea hizi zimekuwa zikiuzwa kwenye maeneo ya vijijini kwa bei zaidi ya ile bei elekezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi UREA ni Sh.61,000, wakulima wanatakiwa kununua mjini na kuisafirisha mpaka mashambani (vijijini) hivyo gharama kuongezeka mara dufu. Tunaiomba Serikali ipeleke mbolea hizi kwenye Makao Makuu ya Kata au Tarafa ili kuwarahisishia wakulima gharama kubwa za usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji. Tatizo la maji vijijini bado ni kubwa, mfano; katika Jimbo la Lupembe kuna zaidi ya vijiji 25 havina maji. Pamoja na Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuongoza Kitaifa kwenye usafi wa mazingira na vyoo bora lakini vijiji vyake havina maji safi. Njombe ni eneo ambalo limezungukwa na mito mingi na mito hii inamwaga maji yake katika Mto Rufiji, hivyo Njombe ni catchment area ya Mto Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia eneo hili kutokana na kutokuwa na maji milimani ambako ndiko yaliko makazi yao hulima mabondeni, hivyo ili kulinda vyanzo vya maji katika Mkoa huu ni muhimu kuwapelekea maji wananchi hawa ili waanzishe bustani za mbogamboga milimani (kilimo cha umwagiliaji) tusipofanya hivyo mipango ya kuwa na miradi mikubwa hasa ule wa Rufiji utaathiriwa na kilimo cha mabondeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ione umuhimu wa kuwapelekea maji safi ili iwe rahisi kuwashawishi wananchi kulima bustani zao milimani ambapo watatumia maji bomba kumwagilia bustani zao.