Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono taarifa hii ya Kamati, naomba kutoa yangu katika kusisitiza haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu kilimo cha matuta. Bado Serikali haijasimamia vya kutosha kilimo cha matuta kwenye sehemu za miinuko ili kuzuia upoteaji wa maji na mmomonyoko wa udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni matumizi ya mito. Serikali haijafanya juhudi kubwa kuweka ramani ya mito yote tuliyonayo Tanzania na kuona jinsi inavyoweza kutumiwa kikamilifu. Kwa mfano, Jimbo la Same Mashariki tuna mito mikubwa minne, lakini mito yote inaenda baharini na wakati huo huo inapita porini bila kunufaisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimeuliza maswali Bungeni pamoja na kuandika barua Wizara ya Maji na Umwagiliaji nikiomba Jimboni kwangu mito hiyo itengenezewe miundombinu ya mabwawa ya kukusanya maji na ya umwagiliaji. Wizara imelifumbia macho jambo hili. Je, usalama wa chakula utapatikana wapi kama hatutilii maanani kilimo cha umwagiliaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia maji ya Jimboni kwangu kutoka mito hiyo tajwa hayajatumiwa kikamilifu kwa ajili ya kupelekwa katika Mbuga ya Wanyama ya Mkomazi. Maji hayo yangeweza kupelekwa kwa njia ya mtiririko (gravity flow), badala yake wanachimba visima ambavyo baada ya muda mfupi mabwawa hayo hukauka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ufugaji wa kisasa. Ufugaji bado umeendelea kuwa wa kienyeji sana. Ningeshauri Serikali ianzishe Mashamba Darasa sehemu za wafugaji ili kuonesha ufugaji bora unatakiwa uweje. Jimboni kwangu wafugaji walitenga maeneo ili wafundishwe jinsi ya ufugaji wa kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kukubali kuwa wangeanzisha Shamba Darasa hilo ni takribani miaka miwili sasa bado Serikali haijaweza kusaidia wafugaji hao. Inasikitisha kila mara Serikali inawataka wafugaji wapunguze mifugo bila kuweka idadi ya juu sana inayokubalika kwamba mfugaji mmoja anatakiwa kuwa na mifugo mingapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ubovu wa barabara za vijijini. Kilimo hakiwezi kuwa na tija kama barabara za vijijini hazikuboreshwa kutokana na ubovu wa barabara hizo. Wakulima wengi huuzia mazao yao mashambani na hivyo kupata bei ndogo sana. Hivyo, naunga mkono hoja kwamba bila barabara nzuri, bila maji ya umwagiliaji na bila kuwa na mifugo iliyoboreshwa nchi yetu haitaondokana na umaskini kwani uchumi wetu unategemea sana hizo sekta tajwa hapo juu.