Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII : Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa Kamati zote mbili kwa kuleta hizi taarifa na hasa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na michango yote ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameitoa. Kwa sababu ya muda nitakwenda haraka haraka, najaribu kuchangia katika maeneo machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imezungumzia juu ya utunzaji bora wa misitu yetu. Ni kweli kabisa kwamba tumekuwa na changamoto nyingi sana zinazoendana na misitu na kwa ujumla hatuna mamlaka ya kusimamia misitu yetu yote. Sasa hivi utakuta asilimia 35 inasimamiwa na Serikali Kuu, asilimia 45 inasimamiwa na Serikali za Vijiji; Serikali za Mitaa zinasimamia 7% na watu binafsi wanasimamia 7%, general land ni 5% na mengineyo ni 1%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali ya namna hii na kwa kuwa misitu ni kitu muhimu sana, lazima kweli tuje na mamlaka moja ambayo italeta usimamizi bora wa misitu yetu na ndiyo maana Serikali tunakusudia kwamba sasa hivi tumepitia Sera ya Misitu iliyokuwepo na sasa hivi tuko katika hatua ya mwisho ya kuja na sera mpya ambayo pamoja na mambo mengine tunafikiria kwamba lazima tuwe na mamlaka moja ya kusimamia hifadhi za misitu yetu, ili angalau kuleta manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nilitaka nitoe ufafanuzi kidogo, Kamati imezungumzia juu ya migogoro mbalimbali pamoja na Wajumbe mbalimbali pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia sana kuhusiana na migogoro. Ni kweli kabisa kuna migogoro mingi katika maeneo mengi na hasa katika hifadhi zetu. Migogoro hii imesababishwa na mambo machache yafutayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni ongezeko la watu. Ongezeko la watu sasa hivi, tuko karibu milioni 52 na zaidi. Wakati tunapata Uhuru tulikuwa milioni tisa tu; ardhi ilikuwa hii hii haijaongezeka. Kwa hiyo, hii imekuwa ni changamotio kubwa na imekuwa pressure katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kwenye uwekaji wa mipaka yetu katika maeneo mengine mengi Waheshimiwa Wabunge wamedai kwamba kulikuwa hakuna ushirikishwaji. Inawezekana ni kweli, lakini nataka niseme, mambo yaliyogundulika katika hii migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumegundua kuna vijiji 366 vimepimwa kwenye hifadhi, vimo kwenye hifadhi. Katika Misitu yote iliyopo, vijiji vilivyopo ndani ya misitu viko 228, hifadhi zenye migogoro ziko 191, wakati huo huo hifadhi zetu kama TANAPA kuna migogoro kama 21, TAWA kuna 23, Mali Kale kuna mmoja na migogoro mingine mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana baada ya kuona kuna migogoro mingi, Serikali ikaamua kwamba tuwe na Kamati ya Kitaifa ambayo inajumuisha Wizara kadhaa kwa ajili ya kuja na ufumbuzi wa migogoro hii yote ambayo imejitokeza katika eneo moja. Kwa sababu, hii migogoro ni mitambuka, haihusu Wizara ya Maliasili peke yake, ni maeneo mengi.

Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba hii Kamati itakapokamilisha hii taarifa sasa, itakuja na mapendekezo mazuri kabisa ambayo yatapunguza kwa kiwango kikubwa migogoro ambayo ipo katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo nataka nizungumzie, linahusu masuala ya mapito ya wanyama. Katika mapito ya wanyama, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia sana. Ni kweli kabisa, hifadhi zetu sasa hivi kwenye maeneo ambayo yalikuwa ni mapito ya wanyama, shoroba, zimevamiwa na wananchi kwa sababu ya ongezeko la watu na shughuli za kibinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara yake kutokana na uvamizi huo, labda niseme kuanzia Oktoba, 2016 mpaka 2017, ekari zaidi ya 42,562 ziliharibiwa na wanyamapori kwa sababu walikuwa wanataka kupita katika maeneo. Maeneo yamevamiwa, watu wanashughulika na kilimo, kuna mambo mengi yakiendelea pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa matokeo yake ekari kadhaa zimeharibiwa. Watu waliopoteza maisha mwaka mmoja tu 484; mifugo iliyopotea 191, fedha ambazo Wizara tunatakiwa kulipa kama kifuta jasho, siyo kama fidia, kama kifuta jasho ni zaidi ya shilingi milioni 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utakuta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)