Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. KEMILEMBE J. LWOTA - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuja kuhitimisha hoja yetu ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuwashukuru Wabunge wote kwa kuweza kutusikiliza na nina imani Wabunge wote mmeunga mkono hoja zetu za Kamati, na pia niwashukuru sana Wabunge wote waliochangia, kwa sababu ya muda sitataja Wabunge wote, ila nitataja tu idadi. Wachangiaji waliochangia kwa maandishi ni Wabunge 17 na wachangiaji waliochangia kwa kuzungumza Bungeni ni Wabunge 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiongelea suala la Wizara ya Ardhi, nadhani Mheshimiwa Waziri ameongelea na amejibu hoja nyingi za Waheshimiwa Wabunge na mapendekezo pia ya Kamati ameyaafiki, kitu ambacho pia sisi tunaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho tunasisitiza kama Kamati ni Serikali itenge fedha za kutosha ili mambo yote, na mipango yote mizuri ambayo Wizara ya Ardhi inayo ya upimaji na urasimishaji wa ardhi nchini kote ufanyike ili kuweza kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi ambayo inaendelea sehemu tofauti tofauti katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Waziri, amejibu lakini hajajibu hoja za Kamati kama tulivyopendekeza. Lakini tushukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi anazoendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo kadhaa kwenye Kamati tuliyaona na ni vema nikayasemea hapa pia. Sheria Namba 5 ya Wanyamapori ya mwaka 2009 imeainisha baada ya Sheria hiyo kuanza kutumika mwaka 2009, ilikuwa ndani ya miezi 12 itangaze upya mapori tengefu, maeneo oevu na hifadhi zote za Taifa, hii ilikuwa mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masikitiko kwa Kamati kwa sababu mpaka hivi leo tunaongea mwaka 2018, hii kazi haijafanyika na kufanyika kwa kazi hii kungeweza kusaidia mambo mengi sana ambayo yanaendelea hivi sasa. Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anachangia amekiri kuwepo vijiji ndani ya Hifadhi, hili suala lipo na kwa kweli tungeiomba Serikali itenge fedha ili hili suala liweze kumalizika na jinsi inavyoendelea kuliacha ndivyo linavyoendelea kuwa kubwa. Hii kazi ingefanyika mwaka 2009 ingekuwa tofauti sana na kama itakapokufa kufanyika mwaka 2018/2019 au 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na Wajumbe wengi wamechangia suala la migogoro ya mifadhi na wafugaji. Hili suala ni kubwa na karibia kila Mjumbe aliyezungumza na aliyeandika kwa maandishi wote wameliongelea hili suala, sasa tunaiomba Serikali hili suala likamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mheshimiwa Yussuf ameongelea suala la ushirikishwaji, sisi kama Kamati pia tuliliona ni vyema Serikali inapotaka kufanya jambo ishirikishe wananchi, ishirikishe wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Serikali ikitaka kufanya jambo lake bila kushirikisha wananchi na wawekezaji linaweza likakwamba. Vilevile mwekezaji akitaka kufanya jambo lake bila kushirikisha wananchi na Serikali ni dhahiri litakwama. Kwa hiyo, ni vema huu mtiririko huu ukafatwa na ukawa unafanyika ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala limeongelewa la uharibifu wa misitu, sisi kama Kamati pia tumeliona. Uharibifu wa misitu ni mkubwa sana unaoendelea nchini kwetu na hii yote inasababishwa na kazi na shughuli za kibinadamu, kuna ukataji miti hovyo ambayo miti tunayokata na tunayopanda ni vitu viwili tofauti kabisa.

Kwa hiyo, kama Kamati tunaishauri Serikali, kwanza kabisa ni kuelimisha hawa wananchi umuhimu wa kupanda miti na vilevile kuna suala la kuchoma mkaa, hili suala ni kubwa. Watanzania zaidi ya 80% wanatumia mkaa majumbani kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza kulisaidia hili suala na kuokoa miti yetu, ni vema Serikali ikaja na mkakati na mpango mzuri wa nishati mbadala na kupunguza gharama ili wananchi waweze ku-afford. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongelea pia suala la kuweka alama kwenye hifadhi, ili pia ni suala ambalo linatakiwa kufanyika mapema. Tumeona kuna matatizo kwenye shoroba, lakini kwa sababu hakuna mipaka na wala hakuna Sheria ya maeneo haya. Kwa hiyo, ni vema Serikali ikajipanga na kuja na huo mkakati na ukafanyika haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeongelea suala la Utalii ambao Mheshimiwa Waziri naye amelijibu, ni dhahiri kwamba Serikali yetu inapata mapato ya Taifa takribani 17.5% na vilevile fedha za kigeni kwa 12%. Kama Kamati tunataka tukushauri na kusema Wizara hii ni zaidi ya kidiplomasia, mahusiano ya nchi na nchi yanatakiwa. Tumeona forex hii inakuja kutokana na wageni wanaotoka nje. Kwa hiyo, kama Kamati tunaomba na tunaitaka Serikali kama inawezekana iweze kuwa na mahusiano mazuri na watalii vilevile na wawekezaji nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kuunda Kamati Ndogo kama Kamati pia tulilipendekeza na napenda kulisisitizia. Mheshimiwa Lukuvi amejibu, amesema Kamati Ndogo ilifanyika na kina Lembeli na ndiyo inafanyiwa kazi mpaka leo, lakini sisi kama Kamati hatujawahi kuona majibu hayo. Kwa hiyo, kwa sababu hatujawahi kuyaona tumeona kama Kamati yetu sisi ni vema pia ikaifanya hii kazi upya na tukaja na mapendekezo hapa Bungeni na tukaona tunaanzia wapi kutokea hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naliomba Bunge lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa mwaka 2017 pamoja na maoni na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii.

Waheshimiwa Wabunge, naomba kutoa hoja.