Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hasa maeneo yanayohusu Wizara yangu ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Kamati ambayo tumefanya nayo kazi, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, imetuongoza vizuri miaka miwili hii. Mwenzangu aliyenitangulia wameshirikiana naye vizuri na mimi nilipofika nimepata ushirikiano katika miezi hii minne ambayo nimefanya nao kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushukuru kwa pongezi zilizotolewa na Kamati kwa vyombo vitatu vinavyofanya kazi katika Wizara yangu, kwa maana ya TASAF, MKURABITA na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Kamati inakubali kwamba wanafanya kazi nzuri, wanaomba tu ikiwezekana wawezeshwe ili waweze kufanya kazi nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa upande wa TASAF, kwamba tupo TASAF Awamu ya Tatu, utekelezaji tumefikia walengwa asilimia 70, bado walengwa asilimia 30. Tunafanya utafiti sasa kujiandaa kwa utekelezaji Awamu ya Pili ya TASAF ya Tatu na lengo la Serikali ni kuwafikia walengwa wote ili Watanzania wote wanaohitaji msaada wapate kusaidiwa na Mfuko wa TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lilikuwepo swali hapa kuhusu ajira ya wataalam, ilizungumzwa wataalam katika afya, lakini kwa sababu Bunge hili hushughulika na ajira kwa watumishi wote, ningependa kusema yafuatayo kuhusu ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kuwa zoezi la uhakiki wa watumishi limeleta upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo watumishi wa kada ya ualimu na afya, Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 15,000. Hao 15,000 tumekwishwa waajiri katika hao 4,000 wako afya, 4,000 wako elimu na hasa elimu ya sekondari kwa walimu wa sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatoa ikama iliyoidhinishwa kwa mwaka 2017/2018 ambapo jumla nafasi zilizokubaliwa 52,436 wanatarajiwa kuajiri, tulikuwa tunaziba pengo la wale ambao wametolewa kwa ajili ya vyeti fake, sasa tunataka kuingia katika mchakato wa ajira zile 52,000 ambazo zilikwishaidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niseme, nimesikia hapa ndani na baadhi yao wameniandikia vikaratasi, kwamba zipo Halmashauri zahanati imefungwa au kituo cha afya kimefungwa kwa kukosa muhudumu.

Mimi naomba endapo kuna mtu yeyote, Mbunge au mwananchi yeyote anayenisikia ambako katika Halmashauri yake zahanati imesimama kwa kukosa muhudumu nipewe taarifa, tutamuajiri mara moja ili huduma za afya ziweze kuendelea. Maeneo mengine tunaweza tukasubiri, lakini kwa afya ya binadamu hatuwezi tukaendelea kusubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limegusiwa hapa suala la utawala bora na mimi ni Waziri wa Utawala Bora. Nisingelipenda kubishana sana, lakini nataka niseme hivi, utawala bora maana yake nini? Utawala bora maana yake ni watu kuishi katika jamii kwa kufuatana kwa sheria na taratibu walizokubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tanzania sheria na taratibu walizokubaliana zinatoka hapa katika Bunge, kwa hiyo mtu anayekwenda kinyume na yanatoka hapa katika Bunge huyo anakwenda kinyume na Utawala Bora na anapaswa ashughulikiwe kwa sababu anakwenda kinyume na sheria za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niseme, magazeti ya leo kama mmesoma Daily News wameandika, gazeti la Habari Leo wameandika, kiswahili wameandika lile la kiswahili Tanzania yang’ara katika utawala bora, tumeambiwa katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ni ya kwanza; Rwanda wanatushinda katika fighting corruption wao wa kwanza, sisi wa pili, lakini ile utawala bora ikiunganishwa, akina Mpango mnasema uchumi shirikishi, Tanzania ni ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno hayo yanaungwa mkono na TWAWEZA, maneno hayo yanaungwa mkono na Transparent International, maneno hayo yanaungwa mkono na REPOA, maneno hayo yanaungwa na World Economic Forum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba yale mambo yetu mengine si vizuri tukalumbana. Mimi sikuona mahala, nimefatilia na bahati kipindi hicho pia nilikuwa Waziri wa Utawala Bora, sikuona mahala aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arumeru katiwa hatiani na Mahakama ya nchi hii. Kwa hiyo, unavyosimama hapa ukasema kapewa promotion mtu ambaye ametenda kosa hili, hili, hili nchi hii chombo peke yake chenye mamlaka ya kutafasiri sheria ni Mahakama, hakuna mahala yule mtu ametiwa hatiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ambayo yamezungumzwa hapa ni kuhusu bomoa bomoa. Siwezi kujibu yote, lakini nataka niseme tunataka kutengeneza reli standard gauge, tunataka kupeleka barabara iwafikie watu, nyumba yako ipo barabarani tuiache? Mimi nasema Serikali hii haina double standard, nyumba za watu binafsi zilizoko barabarani zimevunjwa, sasa hivi jengo la TANESCO mali ya Serikali linavunjwa. Linavunjwa kwa nini, kwa sababu liko barabarani. Hii Serikali haina double standard. Habari …
(Makofi)

T A A R I F A . . .

AZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa jinsi nilivyobobea katika siasa sikusudii kubishana naye, nakusudia niendelee tu kujenga hoja niliyokuwa naijenga. Yeye hakai Arumeru, mambo ya Arumeru hayajui. Mwenyekiti Mao Tse Tung anasema no research, no right to speak, anajua hao Madiwani wameingiaje? Hivi mimi inanihusu nini hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimalizie katika hilo suala la utawala bora. Mmegusia katika habari ya kufungia magazeti, nataka niseme hivi, katika utawala wa nchi hii hakuna vacuum, Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ilikuwa inampa Waziri kufungia magazeti, baadae tumebadilisha Sheria katika vyombo vya habari kuna committee inayoitwa Content Committee, wale wanafuatilia kama gazeti au redio au luninga imekwenda kinyume wanamshauri Waziri Kamati (Content Committee) wanamshauri Waziri kwamba hawa hapa wamekwenda kinyume na sheria za nchi, Waziri anachukua sheria, hatukurupuki tu hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ile Sheria ya Vyombo vya Habari tulikuja tukairekebisha, tukaipitisha hapa. Kwa hiyo mimi nataka niseme kwamba suala la good governance (utawala bora) ni kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi ambazo tumekubaliana katika jamii. Inawezekana wewe ulitaka sheria iwe hivi, iwe hivi, bado hujawa na majority ya kutunga sheria, fuata wale walio wengi walivyotunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, palikuwapo na hoja kwamba watu wanakaimu muda mrefu bila kudhibitishwa. Nataka kusema kwamba ulitolewa mwongozo unaosema kwamba kabla hujamkaimisha, kabla hujamfukuza, wasiliana na Utumishi, Utumishi watambue kule kukaimu kwako ili utakapokuwa unaomba kwamba yule adhibitishwe liwe lisiwe jambo jipya kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine watu wanakaimishwa bila Utumishi kuhusishwa, watu wengine wanafukuzwa hata bila Utumishi kupewa taarifa. Tunaomba tu kwamba taratibu tu zifuatwe na taratibu zikifuatwa sisi tukiletewa majina hata kama ni upekuzi tunasimamia na zoezi linaenda kwa jinsi ambavyo limekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu pale Mollel kauliza maswali mawili ya msingi sana. Tunawafanyaje darasa la saba wale? Tunafanyaje wale ambao tumewafukuza kwa sababu ya vyeti fake? Niseme lile la vyeti fake na hilo la watu wa darasa la saba; Serikali imekaa na TUCTA (Chama Huru cha Wafanyakazi), ni mambo ambayo tumezungumza, tunaendelea kuzungumza nao, tumepeana muda ili jambo hili tuweze kulimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niseme lile la vyeti fake, Serikali ilishasema kwamba kama mtu wakati wa kutafuta ajira alipeleka vyeti fake na yeye akaingia mkataba na Serikali maana yake mkataba wake ule ni null and void. Maana mwajiri alimtaka apelike cheti ambacho ni sahihi, cheti ni halali. Yule ambaye aliyepeleka cheti fake maana yake mkataba nao ni fake. Swali linakuja je, unamu-award mtu ambaye ana cheti fake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, TUCTA wameiomba Serikali na Serikali imeshasema, kama ni kuwashitaki wale wangeshtakiwa na TAKUKURU, wangeweza kushtakiwa na Kanuni za Utumishi, Serikali imetoa msamaha. TUCTA wametuomba kwamba tunaomba Serikali iwe na jicho la huruma kwa hawa watu wa darasa la saba, kwa hawa watu wa vyeti fake na Serikali inalifanyia kazi jambo hilo, muda utakapofika Serikali itatangaza uamuzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui nimebakiwa na dakika ngapi, maana yake mambo yapo mengi ambayo yalikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, naounga mkono hoja ya Kamati tunazozijadili, ahsante sana.