Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kwa kupewa nafasi hii nami kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 20 Novemba, 2015. Nimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa yote aliyonijalia mpaka leo hii nikaweza kuwepo mahali hapa. Lakini pili, niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Lupembe kwa imani kubwa waliyoiweka juu yangu mimi wakanichagua na kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais ni nzuri sana na kwa kupitia hotuba hii wananchi wa Jimbo langu la Lupembe na wananchi wote wa Tanzania wameifurahia sana, kwani inaonyesha mwelekeo mzuri na matumaini mazuri ya kimaendeleo hasa kiuchumi lakini pia maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yake Mheshimiwa Rais ya tarehe 20 Novemba alieleza sana juu ya viwanda hasa viwanda vidogo vidogo ambavyo vinaajiri watu wengi sana. Viwanda hivi vimekuwa vikiajiri watu wengi na hivi viwanda ni vile viwanda vinavyohusika sana na usindikaji wa mazao mbalimbali kwa ajili ya kuongeza thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Lupembe tuna kiwanda cha muda mrefu sana, Kiwanda cha Chai Igombola ambacho hivi sasa ninavyoongea kwa takribani miaka zaidi ya nane kiwanda hiki kimefungwa, kilifungwa tarehe moja mwezi wa nane mwaka 2008, kutokana na mgogoro uliokuwepo kati ya Wakulima na Mwekezaji. Naomba Serikali ijitahidi au ifanye jitihada za kuhakikisha kwamba kiwanda hiki kinafunguliwa ili wananchi wale wa Lupembe waweze kuuza mazao yao ya chai, lakini pia tuweze kuimarisha uchumi na hatimaye Serikali ikaweza kukusanya kodi kutokana na mishahara ambayo itatokana na wafanyakazi watakaokuwa wameajiriwa pale, lakini pia iweze kupata tozo kwa maana ya kodi kwenye kiwanda kile na hatimaye kuweza kuinua uchumi wa wananchi wa Lupembe ambao umezorota sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kuelezea kidogo juu ya zao letu la chai. Zao hili limekuwa likilimwa maeneo yangu na ndiyo zao kuu tunalolitegemea sana sisi wana Lupembe. Lupembe ipo Halmshauri ya Wilaya ya Njombe, mnafahamu wote ni Halmashauri ya zamani sana hii, na Lupembe ilikuwa ni miongoni mwa maeneo hapa nchini yanayoongoza kwa ulimaji wa chai. Lakini zao hili la chai limekuwa likiuzwa kwa bei ndogo sana ukilinganisha na bei za uzalishaji wa zao hili. Sasa hivi linauzwa kwa shilingi mia mbili hamsini lakini bei ya uzalishaji, gharama za uzalishaji, ukijumlisha zote za kuuzia, gharama za uzalishaji wa kilo moja ya chai ni shilingi 450/=. Kwa hiyo wakulima hawa wanafanya hiki kilimo kwa hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweze kuziangalia kodi mbalimbali ambazo zimeingizwa kwenye zao hili ili ziweze kupungua na hatimaye wakulima wa Lupembe waweze kupata faida kutokana na zao hili la chai.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niweze kuongelea kidogo juu ya elimu, tumesema kwamba Serikali hii sasa kwanza wananchi wangu wamefurahi baada ya Mheshimia Rais kutangaza kwamba sasa elimu ni bure. Kwa hiyo, wananchi wengi waliokuwa wanashindwa kupeleka watoto wao shule sasa wataweza na wameshaanza kupeleka kwa wingi sana. Lakini kupeleka wanafunzi wengi haisaidii kama hatujatengeneza mazingira mazuri kwenye shule hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu moja wapo niiongelee kidogo ni kuhusu walimu hususani madaraja ya walimu, upangaji wa madaraja ya walimu ya mishahara, kumekuwa na tatizo kubwa sana, walimu wamekuwa wakilalamika. Utakuta kwa mfano, mwalimu amefanya kazi miaka saba, nane akiwa na level ya diploma anaenda kusoma degree, anaporudi anapewa daraja lile la “D” halafu anapewa daraja bila kupewa mshahara. Tunaita anapata dry promotion, sasa dry promotion zimekuwa zikikatisha sana tamaa kwa walimu kufanyakazi. Kwa hiyo, tusipoboresha kwenye upande wa walimu hasa madaraja wanapopata promotion ni vizuri yaendane na malipo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa hivi utakuta kwamba mwalimu anaporudi kutoka chuoni kwenda kufundisha wakati alikuwa amefanya kazi muda mrefu anaenda kuanza ngazi ya mshahara sawasawa na yule kijana au mwanachuo anayeanza kazi. Sasa hii inawakatisha tamaa walimu wengi sana na ndiyo maana utakuta tunasomesha walimu wengi lakini mwisho wa siku walimu wanaamua kuhama kada wanahamia kada nyingine, kwa kuwa wanaona kada hizi za walimu kidogo zinausumbufu na maslahi yake yapo duni. Naomba Serikali iangalie uwezekano wa kurekebisha utaratibu huo, mimi naamini kwamba ingekuwa ni vizuri kama mwalimu amefanya kazi ameenda kusoma anaporudi basi angalau aongezee ngazi ya mshahara nzuri zaidi kuliko wale wenzake waliobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa hivi utakuta kwamba wenzake waliobaki ambao hawajaenda kusoma wanakuwa na mshahara mkubwa zaidi, wanapewa daraja zuri zaidi kuliko yule aliyeenda kusoma. Kwa hiyo, kwa kada ya walimu kusoma sasa imekuwa kama ni adhabu. Tunaomba Serikali iweze kurekebisha jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme kidogo juu ya huduma ya afya. Jimbo langu la Lupembe ambayo ndiyo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mpaka leo hii haina hata hospitali moja na mpaka leo hii ina kituo cha afya kimoja, Halmashauri nzima, Jimbo zima na zahanati ndogo ndogo na vituo vya afya vingine viwili ambavyo bado vipo kwenye ujenzi. Wananchi wale wanapata shida sana ili waweze kujifungua hasa kwa operation kuna baadhi ya wananchi wanatembea kilometa mia moja arobaini na saba kwenda kutafuta Hospitali ya Kibena ili waweze kupata operation za uzazi. Naomba Serikali ijaribu kuliona hili jambo la muhimu sana tunaomba tupewe hospitali ya Wilaya lakini pia vituo vyetu hivi vitatu viweze kuboreshwa viwe na huduma ya operation kwa maana ya theatre ili akina mama wasiteseke kutembea umbali mrefu na wengine kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo juu ya wastaafu. Wastaafu waliostaafu kuanzia mwezi wa sita mpaka mwezi Disemba hawajalipwa mafao yao wanataabika huko, wanalalamika na wanailaumu Serikali. Kwa hiyo tunaomba Waziri mwenye dhamana aweze kuchukua jitihada ya kuhakikisha kwamba hawa wastaafu wetu waliofanya kazi muda mrefu, waliojenga Taifa hili wanapata mafao yao haraka ili waendelee kuishi vizuri na kufurahia kustaafu kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo juu ya jambo moja kuhusu umeme, Jimbo langu Halmashauri ya Wilaya ya Njombe sehemu kubwa halina umeme. Tuna vijiji 49 lakini vijiji tisa tu ndivyo vyenye umeme. Namuomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na sisi pia atufikirie kule kijijini tuweze kupata huduma ya umeme ili tujisikie na sisi ni miongoni mwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongee jambo kidogo kuhusu maji. Katika Jimbo langu la Lupembe na ndiyo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe vijiji vingi havina maji, mpaka sasa hivi ni vijiji nane tu ndivyo vyenye maji. Sasa kwa hali hii ndugu zangu au Serikali tunaomba mtuangalie na sisi tupate maji kama alivyosema Rais hii Serikali ni Serikali ya kuwatua kina mama ndoo ya maji, basi mtutue na sisi kule Wanalupembe na sisi tujisikie kwamba wake zetu, mama zetu, wanafurahia maisha kwa kutuliwa ndoo za maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisema kidogo juu ya Halmashauri yetu ya Wilaya ya Njombe ipo kwenye Halmashauri nyingine, ipo kwenye Halmashauri ya Mji wa Njombe. Sasa Watendaji wengi na wananchi wengi wanapata shida sana kupata huduma na ile ni Halmashauri Mama ni Halmashauri ya zamani sana. Sasa hivi ukienda hakuna hata gari moja……
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hongoli muda wako umekwisha.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, ahsante sana na naunga mkono hoja.