Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenifanya niweze kusimama hapa mbele yenu leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge pomoja na viongozi wa Bunge kwa kuweza kunifariji kwenye msiba ulionipata wa kuondokewa na mama yangu mzazi. Nawashukuru sana, Mwenyezi Mungu awabariki. MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba pia, kumpa pongezi Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Pongezi pia kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kazi anayoifanya pamoja na Naibu na watendaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kwenye bajeti. Ni kweli kabisa wote mnaamini kuwa pesa tunazopitisha sizo zinazotolewa. Naomba sana kama kweli tunakipa kipaumbele kilimo, pesa tunazozipitisha ziweze kutolewa zote. Kila mmoja anajua kilimo, mifugo pamoja na uvuvi ndiyo uhai wa mwanadamu, kwa hiyo, naomba sana kitiliwe mkazo kwa upande huu wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kilimo ni sayansi. Kwa hiyo, naomba sana kwenye upande wa utafiti hela zinazotengwa ziweze kuongezwa. Tuna vyuo vikuu, kwa mfano Chuo Kikuu cha Sokoine wanafanya utafiti, tunazo research centres mbalimbali, Ilonga, Uyole, Ukiliguru, Maruku, zote zinafanya utafiti pamoja na vyuo vingine vya uvuvi. Naomba sana hela ziweze kutolewa kwa watafiti wetu. Pia pamoja na utafiti unaofanyika tuweze kupata mrejesho kwa wakulima wetu kusudi waweze kuutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Kilimo imeanza kazi, ni kweli, lakini mpaka sasa hivi bado iko Dar es Salaam. Kwa mfano, kwa Mkoa wangu wa Morogoro ni wakulima wazuri sana, mikoa mingine iko mbali sana kama Ruvuma, Kagera, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Waziri alivyosema ningeomba sana matawi yaweze kufunguliwa haraka iwezekanavyo kwa mikoa hii yote kusudi waweze kutumia hii Benki ya Kilimo kwa mikopo kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye pembejeo na hasa naongelea kuhusu mbegu. Inaonekana kuwa asilimia kubwa ya mbegu zinatoka nje na hazitozwi kodi, narudia tena hazitozwi kodi lakini mbegu zinazozalishwa hapa nchini zinatozwa kodi. Naomba ufafanuzi kama nimeeleweka. (Makofi)
Jambo lingine ni kuhusu viwanda vya mbolea na vyenyewe inaonekana kuwa mbolea inayotoka nje inafikiriwa zaidi kuliko mbolea inayotoka hapa nchini. Kwa mfano, tunacho Kiwanda cha Minjingu, naomba sana viwanda ambavyo vipo hapa nchini viweze kupewa kipaumbele na ruzuku yake iweze kutolewa vizuri iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu na inawezekana, kama tunaweza mambo mengine kwa nini hiki kisiwezekane? Mheshimiwa Waziri naomba tujitahidi sana kuzalisha mbegu hapa nchini Tanzania kwa sababu kwanza kabisa mbegu inayozalishwa hapa inaendana na hali ya hewa ya hapa lakini ukitoa mbegu za nje ndiyo maana unapata viotea na vibua. Kwa hiyo, naomba sana tujitahidi kuzalisha mbegu zetu hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine naomba kuongelea utaratibu au mfumo mzima wa ruzuku. Namshukuru Mheshimiwa Waziri anaendelea kusema kuwa mfumo huu utabadilishwa, utabadilishwa lini? Serikali mnafanya vizuri, naomba sana huu mfumo wa voucher uweze kubadilishwa kusudi iwepo system ambapo mkulima yeyote yule mdogo na mkubwa unakwenda dukani unapata mbolea na mbegu wakati wowote kama unavyokwenda dukani kununua majani ya chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko. Ni kweli mazao mengine hayana masoko lakini hatutamaliza tatizo hili la masoko mpaka tuwe na viwanda, mnyororo wa kuthamanisha mazao. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Kilimo iweze kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kuanzisha viwanda ili kusudi hizi malighafi ya kilimo ziweze kutumika kwenye viwanda hivi.
Ni kweli Afisa Ugani hawatoshi lakini mimi naamini Vyuo vya Kilimo kila siku, kila mwaka vinazalisha wataalam hawa. Naomba Serikali ione jinsi ya kuwaajiri Maafisa Ugani hawa wote. Kama kweli kilimo, uvuvi na mifugo tunakipa kipaumbele na wenyewe waweze kuajiriwa mara moja mara wanapomaliza masomo yao maana wako wengi.
Jambo lingine ambalo naweza kuongelea hapa ni kilimo cha mkataba. Kilimo cha mkataba ni kizuri kwa sababu kinakupa pembejeo zote na kinatoa service za Afisa Ugani kwa kila jambo. Kwa hiyo, naomba kiweze kufikiriwa kiendane pamoja na uwekezaji. Wawekezaji na wenyewe tuweze kuwakaribisha waweze kuwekeza kwenye upande wa kilimo, uvuvi na mifugo kusudi tuweze kutatua jambo hili la masoko kwa kuwekeza kwenye viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha mboga na matunda. Naomba kuwataarifu kuwa Mkoa wangu wa Morogoro ni moja ya mikoa ambayo inalima sana mboga na matunda pamoja na mikoa mingine kama Tanga. Kwa hiyo, naomba sana tuone jinsi ya kuthaminisha mazao haya ya mboga pamoja na matunda kusudi yaweze kupata thamani kwa sababu karibu asilimia 32 zinapotea hivihivi. Kwa hiyo, naomba tuliangalie sauala hili. Hata hivyo, hapohapo tujikite na tuwe na mkakati wa kuwasaidia vijana na wanawake kwenye kilimo cha mboga na matunda. Kwa kulima mboga na matunda unaweza ukapata kipato kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha miwa Mkulazi. Eneo limetengwa lakini kwenye kitabu Mheshimiwa Waziri sikuweza kuona vizuri kama limezungumziwa. Kama lipo, ningeomba kupata ufafanuzi kwa sababu wakulima wa Mkulazi, Morogoro tayari wamejitayarisha, wametenga eneo lao kwa hiyo naomba liweze kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea mbegu za mafuta kwa mfano, ufuta, alizeti, pamoja na karanga. Naomba sana zipewe kipaumbele, Serikali tuangalie namna ya kupunguza kuingiza mafuta hapa nchini kusudi tuweze kutumia mafuta tunayotengeneza wenyewe. Haya mafuta ya alizeti yanayosambaa barabarani yanakwenda under rancidity yaani yanaharibika. Kwa hiyo, naomba sana na haya mafuta tunayotengeneza hapa nchini yaweze kuwekwa vizuri kusudi wananchi waweze kupenda kuyatumia. Naomba Wizara ya Viwanda iweze kushirikiana pamoja na Wizara ya Kilimo kwenye mambo mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuzaji wa viumbe majini, mabwawa ya samaki ni jambo zuri sana, unakwenda hapo unatoa samaki wako, unaingia ndani unapika unapata lishe. Kwa hiyo, naomba sana kama Mheshimiwa Waziri alivyosema tukazanie huu uzalishaji wa viumbe vya majini ili tuweze kupata lishe pamoja na kipato kwa kutumia bahari na mito yetu. Nimefurahi sana kuona kuwa watatoa ruzuku kwa wavuvi wadogo wadogo, hicho ni kitu kizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza, naomba sana kuongelea kuhusu mifugo. Wafugaji na wenyewe tuwaangalie kwenye kuwawekea miundombinu.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.