Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kwa ushauri wao mzuri kuhusu utendaji kazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua hii niseme kwamba tumepokea ushauri na maoni ya Kamati yote yaliyotolewa na niahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tutayazingatia kwa sababu lengo la ushauri ambao umetolewa ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, namba mbili, tumepokea pongezi za Kamati kuhusu kazi nzuri inayofanywa na taasisi zetu kama walivyoona; TFDA, MSD, MOI, MNH na JKCI na kupitia hatua hii niahidi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuchukua jitihada hasa za kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibingwa, matibabu bobezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Taasisi yetu ya Moyo ya Jakaya Kikwete wameendelea kufanya kazi nzuri ya kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi kutoka rufaa za wagonjwa 89 mwaka 2016 hadi wagonjwa wawili tu kwa mwaka 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana ya kazi hii nzuri ambayo wanafanya taasisi zetu sio kwamba tu Serikali itapunguza gharama na kuokoa fedha, lakini maana yake Watanzania wote maskini au tajiri ana accessibility ya kupata huduma za matibabu bobezi, kwa hiyo ni suala la usawa kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge pia kwa kutambua kazi ya Muhimbili, bahati mbaya kwamba ile CT Scan ni siku mbili lakini inafanya kazi nzuri na tutambue kwamba Muhimbili wanafanya mabadiliko makubwa ya kutoa huduma za kibingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimwambie Mheshimiwa Mtolea tu kwamba tunafunga CT Scan kwenye Taasisi yetu ya Mifupa ya MOI kwa hiyo itakuwa ni backup, pale CT Scan ya Muhimbili itakapoharibika, basi ya MOI itafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa nijikite katika maoni yaliyotolewa na Kamati, kama nilivyosema ni mengi, lakini nizungumze mambo makubwa matano. Jambo la kwanza, ni kuhusu hali ya upatikanaji wa dawa. Tunashukuru Kamati kwa kuona jitihada ambazo zimefanyika ndani ya Serikali na tunakubali kwamba bado zipo changamoto chache katika upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme, changamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa ilikuwa inachangiwa na upatikanaji wa fedha, hakukuwa na fedha za dawa. Sasa hivi fedha za dawa zipo katika halmashauri zetu, zipo katika zahanati zetu, zipo katika vituo vya afya na zipo katika hospitali zetu za rufaa za mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Lubeleje changamoto ambayo tunayo, ukiangalia stock level ya MSD na lingine ambalo nilitolee ufafanuzi, hatuwezi kuangalia upatikanaji wa dawa zote, tunaangalia zile dawa muhimu (essential medicine) ambazo ziko 135, na kwa mujibu wa taarifa ya MSD dawa hizi zinapatikana zaidi ya asilimia 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyokuwepo ni suala la mfumo wa ugavi na usambazaji wa dawa. Nitoe mfano, katika maoteo ambayo tumeyapokea kutoka kwenye halmashauri inaonekana kwamba tunahitaji nchi nzima paracetamol kopo 7,000 lakini kiuhalisia tunauza paracetamol kopo moja yenye vidonge 1,000 kopo 16,000, kwa hiyo, huu ni mfumo ule ambao wa maoteo kutoka halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa ya amoxicillin, kwa mujibu wa maoteo ambayo tumeyapata kutoka halmashauri, inaonekana kwamba tunahitaji kopo 6,500 lakini kiuhalisia tunauza kopo 19,000. Kwa hiyo, niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge na Kamati tutaendelea kuzihimiza halmashauri kuleta maoteo halisi ya dawa ambazo zinahitajika katika halmashauri zao na kuleta maoteo hayo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tutalifanya, tumepata ufadhili, tumenunua magari zaidi ya 180 ambayo yatatumika kusambaza dawa katika sehemu mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa, tumezindua mfumo Standard Treatment Guideline, mwongozo wa matibabu na orodha ya dawa muhimu. Kwa sababu saa nyingine hali ya upatikanaji wa dawa unachangiwa pia na prescription, daktari anaandika dawa ambayo haipo kwenye mwongozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la kaka yangu anayesema kuna dawa za China, dawa za India, dawa za UK, Tanzania tunatumia generic medicine, tunatumia dawa ambazo ni generic na zimepitishwa na WHO. Kwa hiyo, saa nyingine mgonjwa anaenda pale anataka dawa ambayo anaitaka yeye haipo katika mwongozo. Kwa hiyo, tutaendelea kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya, hasa Waganga na Madaktari, kuhusu kuzingatia mwongozo wa matumizi ya dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la NHIF, niseme kwamba tumepokea pia ushauri wa Kamati kwamba tuharakishe mchakato wa kuleta Bungeni sheria itakayomlazimisha kila Mtanzania kuwa na bima ya afya. Nakubaliana na Kamati kwamba ni kweli ni Watanzania wachache ambao wako katika bima ya afya, NHIF kuna Watanzania milioni 3.3 sawa na asilimia saba, CHF ni asilimia
11.7 na bima za afya binafsi ni asilimia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika Watanzania 100 ni Watanzania 32 tu ndio wanapata huduma za matibabu bila kutoa fedha cash, maana yake wanapata changamoto katika kupata huduma, lakini pia mtu anayetumia papo kwa papo analipa zaidi kuliko mtu mwenye kadi ya bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niithibitishie Kamati ya Bunge kwamba, Serikali tayari tumeshapata uzoefu wa nchi mbalimbali, WHO wametusaidia, World Bank wametusaidia, tunajua kipi kimefanya kazi Rwanda kipi hakijafanya kazi Ghana, lakini tunakubali kwamba tutaenda kutembelea, lakini kabla ya kwenda kutembelea nchi hizo tunapanga kuitisha semina ya wadau ili waone Ghana wamefanya vipi, Rwanda wamefanya vipi, Philippines wamefanya vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali ni kwamba bima ya afya ndiyo mwelekeo, ndiyo mhimili wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la afya ya uzazi na mtoto ni suala la kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Nne na niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge suala la kutoa elimu ya uzazi hasa kwa wasichana tumelipa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulikuwa na kikao mimi na Waziri wa Elimu na Waziri wa TAMISEMI, tumeamua kwamba tutaangalia mitaala kuhusu masuala ya afya ya uzazi ili watoto wetu waweze kujua maumbo yao na waweze kujikinga na magonjwa. Vile vile tumeongelea suala la kuwa na Walimu walezi katika shule zetu na tayari pia mwongozo wa kuwafundisha Walimu unaangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo pia tunalifanya katika huduma ya afya ya uzazi ni kwamba Wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi za dharura na nithibitishie Serikali ni moja, Wizara ya afya tutatafuta fedha lakini fedha hizi sisi tutazipeleka TAMISEMI na ndiyo maana tumepata fedha kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya 100 katika Halmashauri mbalimbali. Tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya vituo 100, Ubalozi wa Denimark wametupa fedha kwa ajili ya vituo vya afya 39 na basket fund tumepata fedha kwa ajili ya vituo 19. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Wizara ya Afya haitajenga vituo vya Afya au Zahanati, kazi hiyo ni ya TAMISEMI sisi tunaingia katika suala la kuimarisha ubora wa huduma na hasa katika kuimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto. Kwa hiyo, hela sisi tutazipeleka TAMISEMI lakini tunafanya vizuri na Mheshimiwa Jaffo, vituo vyote vya afya wanakaa wataalam wetu kwa pamoja na wanasema fedha hizi tuzipeleke wapi na hizi tuzipeleke wapi. (Makofi)

MheshimiwaMwenyekiti, suala la fedha za WDF ni kwamba Hazina tumeshafanya majadaliano lakini niwaimize Waheshimiwa kwamba suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi ziko kwa kiasi kikubwa ni ile asilimia tano ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vitambulisho kwa wazee, niseme kwamba tumefanya kazi na tumewatambua wazee takribani milioni 1,600,000 na wazee takribani laki 462 tumeshawapa vitambulisho. Ufafanuzi vitambulisho hivi havitolewi na Wizara ya Afya. Vinatolewa na Halmashauri na kuna Halmashauri zinafanya vizuri; Kigamboni, Msalala, Ubungo, Ikwiriri nitumie fursa hii kuwataka Wakurugenzi wote kuhakikisha wanawapa wazee vitambulisho vya matibabu bure. Pia niweke wazi hii ni hatua ya mpito lengo letu ni wazee wote kupata Bima za Afya pale ambapo tutaanza Bima ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea malalamiko kuna baadhi ya Halmashauri zina waambia wazee wachangie hela ya picha Sh.1,000. Tukimgundua Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo anawachaji wazee kwa ajili ya kitambulisho cha matibabu bure tutapeleka jina lake kwa Mheshimiwa Rais iliaweze kuchukua hatua. Hatutakubali wazee wetu kudhalilishwa kunyanyaswa na sisi sote ni wazee watarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni human resource for health watumishi katika Sekta ya Afya tunakubali kwamba changamoto ipo lakini tayari Serikali imeanza hatua tumeajiri mwaka huu watumishi takribani 3,152 na tumewasambaza katika vituo mbalimbali. Naamini kwamba na Waziri wa Utumishi ananisikia lengo letu ni kuhakikisha kwamba hakuna kituo au zahanati ambayo itaongozwa na mhudumu wa afya au mtu ambaye hana sifa. Tunataka Kama zahanati lazima awe ni Clinical of Assistant au Clinical Officer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hili suala la watumishi dada yangu Benardetha Mushashu kuhusu hospitali za rufaa za mikoa na dada yangu Nuru Bafadhili kuhusu hospitali ya rufaa ya Bombo Mheshimiwa Rais ametukabidhi kuziendesha hospitali za rufaa za Mikoa tumesha-identify, tumeshachambua, tunafundisha Madaktari Bingwa katika fani saba za kipaumbele na Daktari Bingwa wa akinamama na magonjwa ya wanawake ya uzazi, Daktari Bingwa wa watoto, Daktari Bingwa wa upasuaji, Daktari Bingwa wa usingizi na Wanadiolojia wa mionzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeshapata fedha kutoka Global Fund na tunaanza mwaka huu kusomesha zaidi ya madaktari 150, tunawachukua ndani ya Serikali kwa sababu ina kuwa rahisi baada ya kumaliza kurudi kufanya kazi katika mazingira haya, lakiniā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mwisho niseme kwenye watumishi tunategemea kuwa na Community Health Workers hawa wataweza pia kuimarisha masuala ya lishe na masuala ya uzazi wa mpango. Kwa hiyo, tunategemea kuwa nao wawili kila kijiji na tayari Mheshimiwa Mkuchika anakaribia kumaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Waheshimiwa Wabunge tunawashukuru sana.