Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii, hongereni sana na nianze na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambapo katika ukurasa wa 113 anasema, naomba kunukuu; “Mikoa na Wilaya zenye maeneo tete ya chakula mwaka 2015/2016. Mkoa wa Shinyanga na Wilaya zake zote zilikuwa na hali mbaya ya chakula.”
Kwa taarifa hii tu ilikuwa inatosha kabisa kuona ndani ya kitabu cha bajeti cha Waziri, Shinyanga wameitizama kwa jicho gani. Kwa masikitiko makubwa baada ya miaka mfululizo Shinyanga kuwa na hali tete ya chakula hakuna mpango wowote ambao Serikali imeupanga kutuondoa katika hali hiyo. Ukiusoma ukurasa ule Mkoa wa Shinyanga na Wilaya na Majimbo yake yote hali ilikuwa tete. Nilitegemea basi katika bajeti hii ningeona kuna kitu tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa bajeti 2015/2016, Wabunge wote wa Mkoa wa Shinyanga tuligomea bajeti ya Wizara ya Kilimo na Waziri aliposimama kujibu alisema kuwa Wizara itatekeleza ahadi aliyoitoa aliyekuwa Waziri Mkuu kwenye ziara yake Wilaya ya Kahama kwamba Wilaya ya Kahama itakuwa Wilaya ya kimkakati kuuokoa Mkoa wa Shinyanga kwa kilimo kwa sababu ndiyo Wilaya pekee inayopata mvua za kutosha. Nilitegemea kuona Wilaya ya Kahama kuna jambo limefanyika, sijaona kitu chochote.
Naomba Waziri utakaposimama kuhitimisha uniambie ile ahadi iliyotolewa kwenye bajeti mwaka 2015/2016 ya kuifanya Wilaya ya Kahama kuwa ni Wilaya ya kimkakati kwa ajili ya kilimo kuokoa Mkoa wa Shinyanga iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii hii ya Kilimo, nilitegemea basi, Mikoa kama Mkoa wa Shinyanga ambao tunategemea maji ya juu, ningeona kuna bajeti ambayo imetengwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Sijaona hata Wilaya moja kwamba tunajikwamuaje na kilimo hiki kutoka kutegemea maji ya juu na kuwa tunavuna maji; sijaona ni wapi walipoonesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kwa mara nyingine naiamini Serikali yangu, hebu naomba muutazame Mkoa wa Shinyanga kwa macho mawili. Hatuwezi kuwa tunasoma kwenye vitabu tu, lakini utekelezaji hauonekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, katika Mabwawa ya Umwagiliaji, kuna bwawa ambalo lilikamilika mwaka 2015, Bwawa la Ishololo katika Jimbo la Solwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga; lakini nasikitika kusema bwawa lile sasa hivi limeshakatika, maji yote yametoka. Kwa hiyo, kwa mwaka huu bwawa lile hatujavuna maji. Sasa hawa wakulima tunaotegemea kwamba tumewatengenezea bwawa na hatimaye waweze kulima kwa umwagiliaji, bwawa hili limekatika na maji yote yametoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema kwa mara nyingine, nilishasema tuna miradi mingi ya umwagiliaji, naomba tuitengenezee mikakati miradi hii iweze kuhifadhi maji kwa wingi ili tuwe na kilimo chenye tija. Naomba nipate maelezo, miradi yetu ya umwagiliaji kwa nchi nzima, Wizara ya Kilimo mmejipanga vipi kuhakikisha miradi hii inavuna maji ya kutosha na kuwa na kilimo cha umwagiliaji chenye uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na Mikoa au Wilaya ambazo hazina mvua za kutosha isiwe sababu ya kutuadhibu tunaotoka katika maeneo yale, kwa sababu inavyoonekana wale wanaopata mvua mara mbili kwa mwaka ndio pia wanaotengewa fedha nyingi katika mradi wa kilimo. Naomba mtutazame, mwone tunawezeje kutoka hapo tulipo na kuweze kuwa na chakula cha kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye mifugo. Nasikitika kwa mara nyingine, Mkoa wa Shinyanga tulikuwa na Kiwanda cha Kusindika Nyama. Kiwanda hiki mpaka leo hakifanyi kazi, kiwanda hiki kilibinafsishwa. Mheshimiwa Waziri naomba uniambie, toka mlipobinafsisha kiwanda hiki, mpaka sasa hivi kuna hatua gani? Maana zimekuwa ni hadithi. Kitaanza kazi mwezi ujao, kitaanza kazi kesho kutwa, hatuoni kazi inayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Shinyanga tuna ng‟ombe wa kutosha, lakini ng‟ombe hawa wamekuwa wakinunuliwa kwa bei ya chini kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, hali ambayo inawafanya wafugaji wetu kutokufuga kwa ubora na kupata fedha ambayo haistahili kwa mifugo yao. Mimi nadhani ni muda muafaka sasa, tuangalie kwa maeneo ya wafugaji, basi viwepo viwanda ili mifugo hii iweze kuwa na thamani. Nilikwishawahi kusema, hata kwenye minada ambako ng‟ombe zetu zinanunuliwa, basi kuwepo na utaratibu wa kuweza kuuza mifugo hii iwe na thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huo naomba basi na naishauri Serikali angalau ng‟ombe hawa wawe wanapimwa kwa kilo ili wafugaji waweze kunufaika na kuuza ng‟ombe hao wapate faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa mifugo, katika hotuba ya Waziri sijaona popote ambapo kuna mabwawa au malambo ya kunyweshea mifugo yetu katika Mkoa wa Shinyanga. Ninapata shida, tunapowaambia wafugaji wasihame, tumewaandalia mazingira gani ya kuweza kukaa na hii mifugo ili wasiweze kuhama? Naomba Waziri aniambie, tunapotoa tamko wafugaji wasihame, ni mazingira gani tuliyowawekea ili wasiendelee kutangatanga na mifugo hii? Naomba sana mniambie, kwa Mkoa wa Shinyanga ni malambo mangapi ambayo mmepanga na ni mabwawa mangapi kwa ajili ya wafugaji? (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, naendelea kujikita katika Mkoa wangu wa Shinyanga. Katika hotuba ya Waziri na katika Kitabu cha Maendeleo pia. Nilijaribu kutazama hata viwanda vya kutengeneza/vya kuchakata ngozi, Mkoa wa Shinyanga hatuna hata kimoja. Sasa sijui mmetuweka katika fungu gani. Naomba myatazame muone kama kweli mnatutendea haki au kuna jambo gani la ziada ambalo mnaona litastahili kwetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema mvua za mwaka huu zimekwa ni nyingi, za kutosha lakini haitoshi kuwa na mvua nyingi, hatukuwa na miundombinu ya kujiandaa ili mvua zile ziwe na tija kwetu. Kwa kiasi kikubwa mazao mengi yameharibiwa na mvua, maji mengi tuliyoyapata yamepotea bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali na kuishauri, hebu kakaeni mjipange vizuri, hatuna sababu ya kuwa tunayapoteza maji haya bure, tutafute namna ya kuyahifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Kilimo itoe tamko. Pamoja na chakula kidogo walichokipata wananchi wetu, kuna wafanyabiashara ambao wanatoka nje wanakwenda mpaka mashambani kununua zao la mpunga kwa wakulima wetu. Wananunua mpunga ambao hata haujavunwa kwa bei ya kutupwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inakatisha tama! Wananchi wetu wanauza kwa sababu wana shida. Yote hii ni kwa sababu soko la mchele limekuwa likishuka mara kwa mara na hivyo mpunga wao umekuwa ukinunuliwa kwa bei ya chini, kwa bei ya kutupwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi niseme ni mkulima wa mpunga, kwa hiyo hili ninalolisema nalitambua vizuri na inanisikitisha sana kuona wakulima wenzangu wananunuliwa zao lao likiwa shambani kwa bei ambayo ni ndogo, baada ya miezi miwili watakuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)