Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALMAS A. MAIGE – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA
MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kufanya majumuisho ya taarifa ya utekelezaji wa majukumu na shughuli za Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kipindi cha Januari 2017 mpaka 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi mengi yameongelewa na mimi nilibakiza na kipande kidogo tu katika kumaliza kuhitimisha hii taarifa yangu.
La kwanza, nataka Wabunge wenzangu humu ndani na wananchi waelewe kwamba kimsingi kazi ya Kamati yangu sio kutoa adhabu kwa Waheshimiwa Wabunge na kwa raia yeyote bali ni kuhakikisha kuwa nidhamu, ustahimilivu, heshima, utulivu na uzingatiaji wa kanuni za majadiliano ndani ya Bunge unazingatiwa kwa ukamilifu ili kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake kikatiba kwa manufaa ya wananchi tunaowawakilisha na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo haki na madaraka ya Bunge, Kiti cha Spika, shughuli za Bunge ni lazima vilindwe kwa mujibu wa sheria na kanuni dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kupotosha, kudhalilisha, kuingilia na kushusha hadhi ya mhimili wa Bunge. Lakini pia watu na raia na Waheshimiwa Wabunge mjue kwamba mhimili huu ni moja ya mihimili mitatu ya dola hapa nchini kama inavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimepokea kwa maandishi michango ya Waheshimiwa Wabunge, naomba niwataje Mheshimiwa Mary Muro, Mheshimiwa Rhoda Kunchela na Mheshimiwa Lucia Mlowe. Lakini pia nimepokea mchango wa Mheshimiwa Mwakasaka na Mheshimiwa Dkt. Ishengoma wote wameongelea maboresho ya kanuni, lakini pia wameomba uwepo usawa katika maamuzi hasa tunaposhauri Bunge. Na mimi nawaambia kwa sababu Kamati hii inafanya kazi chini ya maelekezo ya Mheshimiwa Spika nitafikisha yote niliyoyapokea kwa maandishi kama ambavyo mmetaka.
Waheshimiwa Wabunge wenzangu na jamii kwa ujumla nasema asanteni sana kwa ushirikiano mlionipa mimi na wajumbe wote wa Kamati ya Haki na Madaraka ya Bunge. Ushirikiano huo ulitupa hamasa na nguvu ya utekelezaji hasa jinsi ya kutekeleza majukumu na shughuli za Kamati kwa ufanisi mkubwa. Nasema ahsanteni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wa Kamati hii wamepata taabu kwa baadhi ya Wabunge wameacha kutusalimia, tukiwasalimu hawajibu na wengine wanaona kama sisi tunafurahi sana tunapofanya maamuzi. Naomba nikiri kwamba hatuko hapa kwa sababu ya kuwakomoa Wabunge; hapana, hatuko hapa kwa sababu ya kuwakomoa raia hapana, tuko hapa kulinda maslahi ya muhimili wa Bunge kama ambavyo ipo katika Katiba na kama hivi ilivyo katika Kanuni ya Bunge za mwaka za 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa hoja kwa Bunge lako, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja sasa Bunge lako lipitishe taarifa yangu hii ya mwaka ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, asante sana.