Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia japokuwa sikuwa najua nachangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango nina mambo matatu ya kuchangia. Jambo la kwanza linahusu development budget ambayo kwa miaka yote tumekuwa tunapata development budget kidogo na tunakuwa na maoteo makubwa na ni kwa nini Mheshimiwa Mpango hatuwezi ku-budget maoteo realistic ambao haiwezi kuwa na tofauti kubwa, hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu property tax. Nilipokuwa nachangia majuzi kwenye bajeti ya Wizara nililizungumzia hili la property tax na bado nalizungumzia kwa sababu kuchukua property tax ya Local Government tunaziua Local Government na dhana ya D by D inadhoofishwa kwa sababu maendeleo yote yako katika Local Gorvenment, ndiko kuliko na shughuli za jamii, elimu, maji, barabara na afya. Ikiwa property tax inachukuliwa basi hizi huduma za jamii zitakuwa hazipatikani kwa wakati na kukaa kusubiri return kutoka Serikalini inachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka jana Mheshimiwa Kamala alizungumza akasema kwamba D by D siyo lazima mtu akusanye mapato, lakini dhana ya D by D ni lazima upeleke resources za pesa ni lazima upeleke resources za watu kuiwezesha Local Government iweze kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo property tax ambayo imezungumzwa pia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu zile nyumba ambazo hazijathaminiwa, ghorofa Sh.50,000/= nyumba zingine ambazo ni siyo za ghorofa ni Sh.10,000/=. Kwa kweli, kwenda kutoza Sh.10,000/= kwa nyumba za tope na majani ni sawasawa na kuwaongezea wananchi wetu umaskini. Kwa sababu wengine kwanza wako kwenye TASAF, sasa unampelekea pesa za TASAF, halafu unamtoza Sh.10,000/=, hiyo ataitoa wapi kama yeye hela yenyewe anaisuburi ya TASAF? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda wenzetu wa CCM wanatoka kwenye vijiji vina maendeleo sana lakini mimi nikiangalia kule kwangu Arusha kwa mfano, utakwenda kwenye vile vijumba vya majani unakuta huyu Mama watoto ni vumbi, ni nguo zilizochanika hizo shilingi 10,000 watazitoa wapi? Naona tutarudia kama wakati wa kikoloni ule wanapokuja watu wa kodi wazee wanaingia porini, hicho ndicho kitakachotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, napendekeza Mheshimiwa Mpango hiyo Sh.10,000/= ya kutoza nyumba za matope na nyumba za majani tafadhali sana iondolewe tuwapunguzie wananchi wetu umaskini. Napendekeza pia katika zile tozo za nyumba ya Sh.50,000/= kwa za ghorofa na zingine ambazo wanaishi wazee wastaafu au wazee wenye zaidi ya miaka 60 na kuendelea wasitozwe hiyo kodi ya Sh.50,000/= kwa ajili ya kurahisisha maisha yao, kama wanavyofanya watumishi wastaafu wa Serikali ambao hawalipi property tax katika nyumba wanazoishi. Kwa hiyo, wazee hawa wa miaka 60 na wenyewe kama ni nyumba ni ya ghorofa ni Sh.50,000/= haijathaminiwa kama anaishi humu ndani asitozwe hiyo kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi hii ya mafuta kwa kweli nasikitishwa kwa sababu tumetoa mzigo kutoka kwa upper class na middle class tumepeleka kwa watu wa chini. Kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya kupunguza umaskini basi hiyo Sh.40/= ya mafuta itolewe kwenye mafuta ya taa. Kwa sababu hao tunaokwenda kuwadai Sh.40/= kwenye mafuta ya taa ni watu ambao kwa kweli maisha yao ni duni sana. Haiwezekani Shangazi yangu yuko kule yuko kwenye kile kijumba anatumia mafuta ya taa halafu tunamtoza Sh.40/= wakati huo mzigo ungetakiwa kubebwa na upper class na middle class.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kama kweli tuna dhamira ya kweli ya kuwajali wanyonge hiyo Sh.40/= itolewe kwenye mafuta ya taa, wananchi wetu kule mikoani na vijijini waweze kutumia mafuta ya taa. Natofautiana na Mheshimiwa Mbunge aliyezungumza
akasema sijui utaleta gesi, hiyo gesi itakuja lini? Ni kama alivyozungumza Mbunge mwenzangu mmoja atakuwa kama yule First Lady wa Ufaransa, watu wanataka mkate yeye anasema wapeni keki. Kwa hiyo, ninayo hayo mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, tukiangalia pia hata katika suala la mafuta japo wengine wanasema kwamba ooh! bei haiwezi kupanda lakini haiwezi ikaenda bure kuna mahali watu watalipa zaidi au kwa kusafirisha mizigo au kwa usafiri wa kawaida na wataendelea kulipa, nasisitiza ile Sh.40/= ya mafuta ya taa iweze kuondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naomba Mheshimiwa Mpango achukue mawazo yangu kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya kuwaondolea wananchi umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.