Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali. Kwanza kabisa nimpongeze Dkt. Mpango na watu wake kwa kuleta bajeti ya kihistoria katika Bunge lako Tukufu, bajeti ambayo tunaamini kwa kiwango kikubwa itakwenda kutoa majibu ya mapambano dhidi ya umaskini ambao umekithiri miongoni mwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda hotuba yangu ya leo itajikita katika kuwaelimisha wenzangu ambao pengine wanadhani wao ndiyo wanajua sana mambo kuliko wengine ili tuweze kuelewana na Watanzania waweze kutuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa na hotuba aliyoitoa rafiki yangu Mheshimiwa David Silinde ninayemheshimu sana katika ukurasa wa 158 wakati anahitimisha alisema, nimalizie kwa kuwakumbusha Watanzania kuwa Serikali hii ya CCM inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa John Pombe Magufuli imekuwepo madarakani miaka mingi toka Taifa letu lipate uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa sana kama kweli hii kauli ndiyo ya bajeti mbadala. Mheshimiwa Magufuli tunayemzungumzia leo ni tofauti kabisa na Mheshimiwa Magufuli aliyekuwepo jana. Mheshimiwa Magufuli wa jana alikuwa ni Waziri tu katika Serikali ya Awamu ya Nne lakini Mheshimiwa Magufuli wa leo tunamzungumzia Kikatiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamzungumzia Magufuli ni mtu wa namna gani. Ukienda Ibara ya 33 (2) inasema Magufuli ni Rais ambaye ni Mkuu wa nchi, ni Kiongozi wa Serikali, ni Amiri Jeshi Mkuu. Hiki pekee yake kinaonesha utofauti wake na alivyokuwa Magufuli wa jana, inakuwaje leo watu wawe na mashaka juu ya maamuzi na utendaji wa Rais John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Menyekiti, Mheshimiwa Magufuli wa leo kwa mujibu wa Katiba hii ana madaraka ya kutangaza hali ya hatari katika nchi Ibara ya 32. Magufuli wa leo ni tofauti na Magufuli wa jana, Magufuli wa leo Ibara 44 ya Katiba ana madaraka ya kutangaza vita dhidi ya nchi nyingine ambayo inaweza kuvamia mipaka yetu. Magufuli wa leo ni tofauti na Magufuli wa jana, Magufuli wa leo ana uwezo wa kutoa misamaha, Magufuli wa leo ndiye ambaye ni mlinzi mkuu wa rasilimali za nchi yetu. Inakuwaje ndugu zetu kama mnasoma Katiba hii leo mumlinganishe Magufuli wa jana na Magufuli wa leo? Huyu ni Magufuli tofauti na ndiyo maana ameanza na kushughulika na rasilimali za Watanzania na Watanzania sasa tunapaswa kumuunga mkono Rais wetu ambaye amejitoa muhanga ili Watanzania tuondokane na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa rafiki yangu Tundu Lissu ninayemheshimu sana wakati tunampongeza Rais hapa, mimi nilidhani yeye kama Rais wa TLS, angetuambia kwamba sasa ameshajipanga kupitia TLS kuleta mapendekezo mazuri hapa ambayo tutakwenda sasa kutazama mikataba na lile agizo la Rais ambapo amemwambia Spika kwamba inawezekana akatuongezea muda ili Sheria hizi ambazo zina wizi ndani yake tuje hapa tuzibaddilishe. Badala yake Mheshimiwa Lissu anasema kwamba hakuna chochote na yeye sasa hajajiandaa. Anaonesha vitabu hapa vya Kamati zilizopita, nilitazamia pia aoneshe na book lililosheheni la Wanasheria kwamba tayari sasa wana kitu kizuri watakachotuletea hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rafiki yangu Mheshimiwa Lissu anapenda sana kukimbilia MIGA (Multilateral Investment Guarantee Agency). Mimi ninayo hiyo Convention hii hapa, ambayo Mheshimiwa Lissu kila wakati anaisema tu lakini hana mimi ninayo hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii convention ukiangalia article ya 12(3) ambacho kinazungumzia Eligible Investments kinasema hivi:
“Uwekezaji wowote utakuwa eligible pale ambapo utakuwa na yafuatayo:- Namba 3 unasema compliance of the investment with host Countries laws and regulations.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu uwekezaji wa wezi hawa hauko eligible, kwa hiyo MIGA hii haitawatetea hata siku moja, wanatakiwa...
TAARIFA . . .
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lissu ambaye namheshimu sana na ambaye ni msomi, atalifanya Bunge hili lishindwe kuamini kauli zake. Mheshimiwa Tundu Lissu huyu kila wakati yeye ndiye alikuwa anazungumzia hii MIGA na MIGA hii ndiyo nimemletea ili nimwelimishe, katika kumwelimisha nimemsomea kipengele cha tatu ambacho kinasema wazi kwamba wale Wawekezaji lazima wafuate sheria za nchi, kama hawafuati sheria za nchi, matokeo yake MIGA haiwezi ikawaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Walimu huwa wanafundishwa na Walimu wengine, mimi leo ni Mwalimu wa Tundu Lissu akae kimya ili niweze kumfundisha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Rais wa nchi yangu katika hilo, kwa kuwa hawa watu, ripoti imesema bayana ikiwa na Wanasheria na Wachumi kwamba hawa watu vitu vitatu; moja ni wezi, mbili wametoa taarifa za uwongo na tatu ni wahujumu uchumi. Mheshimiwa Rais wangu John Pombe Magufuli bado anasubiri nini kuchukua hatua juu ya wezi hawa na nashangaa Mawaziri wanaomsaidia Mheshimiwa Rais yeye tayari amekwishawapa majukumu haya, leo ningetarajia Mheshimiwa Mwigulu kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani angekuwa anashughulika na kule Buzwagi kule Bulyanhulu. Nilitarajia Mheshimiwa Mwinyi ambaye yuko kwenye Majeshi, angekuwa anashughulika na maderaya yanayoenda kwenye migodi kwa sababu migodi hawa watu ni wezi, wanasubiri nini mpaka Rais ndiye aende tena Bulyanhulu kule. Tungesubiri sasa wakati huu akina Majembe Auction Mart wameshakwenda ku-cease ile migodi kwa sababu hawa ni wezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao bado wanahangaika na hawa wawezeshaji tu, vinginevyo mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuamini report hii, kama hawa watu ni wezi, bado tunasubiri nini, kama kweli hawa watu ni wahujumu uchumi, tumekwisha kuwa na Mahakama ya Mafisadi, matokeo yake popo wanakojoa mle, hakuna washtakiwa, mafisadi tumewapata leo, bado hawapelekwi. Nitashangaa sana! Kama wananchi hawana maji, wananchi wa Mwibara wanasota, leo tumepata matrilioni bado tena tunataka ku- negotiate tuna-negotiate na wezi, mwizi tuna-negotiate naye kwa sababu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hapa, sasa hivi tunapeleka mzigo wa Sh.40/= kwenye mafuta kwa ajili ya wananchi wapate maji ilihali matrilioni ya pesa tumekwishayapata kwa wawekezaji hawa, lakini bado tunasema tunataka ku-negotiate, tunataka ku- negotiate, ku–negotiate huku watakuwa nao Bahari Beach au Kilimanjaro Hoteli kwenye viyoyozi, wanakunywa juice na wakati hawa ni wezi! Namwomba Mheshimiwa Rais aende mbele zaidi ili achukue hatua kwa ajili ya watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hii tozo ya Sh. 40/= kwenye mafuta, ndugu zangu tusitake kuwadanganya na kuwapotosha Watanzania. Kwanza tumefuta road license, road license tumeifuta haipo tena, tulichofanya ni kuhakikisha tunaongeza Sh.40/= kwenye lita ya mafuta ili Watanzania wote waingie gharama ili Serikali yetu iweze kutupatia maji, kwa hiyo mtu anaposema kwamba Sh.40/= haimsaidii mtu ambaye hana gari, hatuzungumzii gari pale, tunazungumzia kukusanya pesa kwenye mafuta ili zile fedha tuzipeleke kwa Watanzania wote ambao wanahitaji maji. Kila mtanzania lazima achangie na hata nauli hizi wanazosema zitapanda Serikali yetu inavyo vyombo vya kudhibiti nauli, SUMATRA wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba Mheshimiwa Rais huyu SUMATRA ambaye hasimamii nauli hizi zinazopanda kiholela, SUMATRA ndiye mtu wa kwanza kutumbua huyu. Sisi tunaongeza pesa kwenye mafuta, hatumaanishi kwenda kupandisha nauli kwa wananchi bila kupitia SUMATRA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie hili la mwisho, kuna suala ambalo limetusumbua kwa muda mrefu, hili suala la ukusanyaji wa mapato. Kila wakati Mheshimiwa Mpango, mapato haya tunaambiwa wanakusanya vizuri wamefika kwenye trilioni lakini mapato haya hatuyaoni, sasa kama hatuyaoni na leo tunaenda kwenye trilioni 32 na zaidi, tunataka atakapokuja kuhitimisha hapa, atuondolee wasiwasi na sisi tusiwe tunaendelea kila wakati, tunapitisha bajeti za makaratasi, tunapokwenda kwenye utekelezaji pesa haziendi, pesa hazionekani halafu wanakuja na lugha nyingine vilipanda, vilishuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitakuwa mtu wa mwisho sasa, bajeti ya mwaka jana ilikuwa ni ya kwanza ya Mheshimiwa Rais, alikuwa anajipanga, sasa imekuja bajeti ya pili, bajeti ya pili namhakikisha Mheshimiwa Mpango kama hatapeleka pesa kwenye Halmashauri zetu za Wilaya, kama hatuta–finance miradi, nitakuwa mtu wa kwanza bajeti yake inayokuja kuikataa kwa sababu nitaamini ni wale wale waliokuwa wanatusumbua kwenye Serikali ya Awamu ya Nne kwa hiyo fedha hizi zikakusanywe, fedha hizi zipelekwe kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri hajaziondolea uwezo wa kuendesha Halmashauri zao, haya makusanyo ambayo wanayafanya sisi kama Wabunge hatuwezi kuwa sehemu ya kuua Halmashauri, kwa hiyo anayesema Halmashauri tunakwenda kuziua si sahihi. Halmashauri zitaendelea kuwepo, Halmashauri wataendelea kutekeleza miradi, hata hizi kodi ambazo tunasema kwamba wanaenda kutozwa watu kwenye nyumba za tope, huu ni uwongo wanataka kuwadanganya wananchi, hakuna mwananchi ambaye nyumba yake ya tope inaenda kutozwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba ambazo zinaenda kutozwa kodi tumeanza na mjini na hizi nyumba za mjini kwenye Halmashauri baadaye ndiyo tutaenda kule vijijini kuangalia zile nyumba ambazo zina viwango, siyo kila nyumba ya mwananchi ambaye amejenga nyumba ya tope na yenyewe inaenda kutozwa, huu ni uwongo ambao wanataka wenzetu kutuchonganisha na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili ni Bunge la kihistoria, hili ni Bunge ambalo Rais wetu tunayemfahamu kwa mara ya kwanza wakati anapiga pushapu, Watanzania wengi hawakumwelewa hizo push-up alizopiga alikuwa anamaanisha yeye ana nguvu, yeye ana afya njema, yeye ana uwezo, ndiyo maana anasema tumwombee Watanzania. Mheshimiwa Rais tuko nyuma yako tutaendelea kukuombea na ndiyo maana nawaomba Wabunge kupitia Bunge hili tusimame tumwombee. Eee Baba yetu uliye Mbinguni tunakuomba Rais huyu ambaye ulituletea umuwekee mkono wako, umwepushe na ajali, umwepushe na mikono ya watu ambao wanamnyemelea, wengine wako humu... (Makofi/Kicheko)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)