Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOEL J. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja katika mjadala huu wa bajeti ya Serikali mwaka 2017/2018. Nianze kabisa kwa kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu wake pamoja na timu yao nzima kwa uandaaji wa bajeti nzuri kabisa waliyoiandaa hapa na walivyoiwasilisha kwa umahiri kabisa hapa ndani. Nianze kwa kuiunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuudhihirishia umma kwamba bajeti hii imedhihirisha nia thabiti ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda kwa maana ya Tanzania ya viwanda. Bajeti hii inatilia mkazo ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge. Reli hii itakapojengwa kwa kiwango cha standard gauge itasaidia mambo kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa itasaidia kutupatia pesa za ziada kwa maana ya kusafirisha mizigo ya nchi jirani. Pili, itatusaidia kupunguza gharama ya uzalishaji ya viwanda vyetu tulivyonavyo na viwanda tunavyovitegemea katika kuingiza nchi yetu katika uchumi wa kati. Mwisho, itatusaidia sana kutuondoa na tatizo kubwa la utumiaji mkubwa wa pesa katika kufanya matengenezo ya mara kwa mara kwenye barabara zetu kwa sababu ya kupitisha mizigo mizito ambayo inapitishwa sasa kutokana na ukosefu wa reli madhubuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii vilevile imejikita kumwangalia Mtanzania wa chini kabisa kwa maana ya ile asilimia kubwa kati ya asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania ambao ni wakulima. Tunaiona bajeti hii imeamua kumwondolea mzigo wa kodi kero mbalimbali mwananchi, imepunguza kodi za mazao ya chakula na kupunguza kodi za mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile bajeti hii imeonesha wazi kabisa kumjali Mtanzania wa kawaida na wa chini kwa kuhakikisha kwamba anapata umeme kule aliko kijijini kupitia mpango wa REA awamu ya tatu. Katika hili, kupitia uchangiaji wa bajeti hii niombe kabisa wahusika wahakikishe kwamba ukamilishaji wa REA awamu ya tatu unafanyika ili wananchi waweze kufaidika na mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bajeti hii inajikita katika kuwasaidia Watanzania kuingia kwenye viwanda. Kwa mfano, inajikita kuanzisha mashamba ya miwa ili kuanzisha viwanda vingine vya sukari vitakavyowasaidia wananchi kupata uchumi kwa maana ya kulima miwa. Katika hili niombe kabisa juzi nilipata fursa ya kuongea na Waziri wa Ardhi kwamba katika Jimbo langu la Chilonwa, Kata ya Dabalo Serikali imeweza kuongea na wananchi pamoja na wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amepatikana mwekezaji ambaye yuko tayari kuanzisha kiwanda pale, mazungumzo yalishafanyika na wananchi walishalima miwa, miwa imefika kiwango cha kuvunwa sasa lakini mwekezaji huyo bado kuna tatizo dogo la kupatiwa hati ya kiwanda ili aweze kujenga kiwanda na zoezi la wananchi kuanza kujipatia fedha kwa ajili ya biashara ya miwa ianze kuwafaidisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni nzuri sana kwetu na tunaposema bajeti ni nzuri tunakuwa na vigezo. Kitu kizuri au kibaya unapokilinganisha na kingine lakini kama ndio kwanza unakipata hakiwezi kuwa kizuri au kibaya ni kwamba umeanza. Tunaposema bajeti hii ni nzuri tunailinganisha na bajeti za miaka kadhaa iliyopita, tunaona na tunashuhudia wenyewe jinsi bajeti ilivyosimama katika kumsaidia Mtanzania wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wenzetu ambao wanajaribu kuibeza hii bajeti, waone kwamba bajeti hii tunakwenda mbele hatua moja baada ya nyingine, ni sawasawa na mtu katika maisha yako ya kawaida. Leo unapokuwa mtu wa kawaida huna hata baiskeli unatamani sana uwe na baiskeli, huwezi kutamani uwe na ndege hata siku moja, lakini ukipata baiskeli kesho utatamani uwe na pikipiki, huwezi kutamani kuwa na gari wakati huna pikipiki, ukipata pikipiki kesho utatamani uwe na gari. Kila jambo linakwenda kwa hatua, hapa tulipofikia ni hatua muhimu sana na tuna uhakika tuko kwenye njia sahihi ya kutufikisha kwenye Tanzania ya uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii sasa kwa umakini kabisa, niiombe Serikali itusaidie wananchi wetu vijijini waweze kusaidiwa katika matatizo ya maji waliyonayo. Tumesema kutakuwa na michango ya Sh.40/= katika kila lita kwa maana ya replacement ya road license, lakini tunajua kabisa kwamba pesa hiyo inapokusanywa kutoka kwenye chanzo chochote cha Serikali inakwenda kutumika katika sekta mbalimbali ambazo zinakwenda kuwasaidia Watanzania. Vilevile katika suala la ahadi za viongozi, niombe sana Serikali izingatie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanajisikia kama viongozi wanatoa ahadi na ahadi zile zinatekelezeka. Kwa kweli naishukuru Serikali hii sikivu, juzi nilikuwa na swali kuhusu ujenzi, nikamchukua Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tukaenda naye kwenye daraja ambalo Mama Samia alitoa ahadi wakati wa kampeni na nashukuru kwamba Serikali imetenga fungu kwa ajili ya kuanza kulishughulikia safari hii. Vilevile niseme, isiishie hapo tu, kuna daraja linalounganisha Kijiji cha Msanga na Kijiji cha Kawawa, vilevile ni kati ya ahadi zilizoahidiwa na Serikali wakati ule, naomba zote zitiliwe maanani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo mfupi, naomba kuunga mkono hoja tena. Ahsante.