Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kizalendo na kijasiri wa kuzuia usafirishaji au utoroshaji wa madini nje ya nchi na makampuni haya ya madini. Nampongeza sana. Naomba Watanzania hasa Waheshimiwa Wabunge tunapokuwa kwenye mambo ya msingi yanayohusu nchi na maslahi ya nchi, ni muhimu sana kuungana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamepiga kelele hapa, wamelalamika kwamba wanaonewa, mara tutashtakiwa, lakini leo hii, mchana huu tumeshaona Mwenyekiti wa Makampuni ya Barrick amekuja kuomba msamaha kwamba fedha au madini waliyotorosha watarejesha hizo fedha na wapo tayari kujenga mtambo wa smelting wa kuweza kuyeyusha madini haya nchini. Kwa hiyo, nampongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi huo. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, tunapokuwa na mambo ya Kitaifa, tunapokuwa tunatetea jambo la kuhusu Taifa hili, kuhusu uchumi wa nchi hii na tunapotetea wanyonge wa nchi hii, ni muhimu sana kuungana. Tunapotengana Waheshimiwa Wabunge ndio tunapoteza na tunawakandamiza wale wenzetu wanaobaki kule ambao wametutuma tuwatetee. Naomba siku nyingine tujifunze kuungana na kuwa wazalendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuleta hotuba nzuri ya Wizara yake. Ni hotuba ambayo inatuonesha kwamba tunaenda sasa kwenye uchumi wa kati, uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kuondoa hizi kodi na tozo mbalimbali. Nimeona mmeshaondoa tozo na kodi mbalimbali kwenye malighafi ambazo zinatumika kutengenezea vifaa vya walemavu. Zinapoingizwa toka nje, kodi zimepungua na kuondolewa kutoka asilimia 25 na sasa itakuwa asilimia sifuri. Nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii hakuna asiyejua, walemavu tunao wengi na kila siku walemavu wanaongezeka. Hata sisi Waheshimiwa Wabunge tuliopo humu ndani ni walemavu watarajiwa. Kwa hiyo, kwa kupunguza hii kodi na tozo kutoka kwenye asilimia 25 mpaka sifuri kutawezesha sasa viwepo viwanda vya kutengeneza au kuunganisha vifaa vile ambavyo wanatumia watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutatoa ajira ambayo itasaidia vijana wetu waliopo hapa nchini, waweze kuajiriwa kwenye hivi viwanda vya uunganishaji au kwenye viwanda vile vinavyohusika na utengenezaji wa hivi vifaa ambavyo wanatumia walemavu. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu wako kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, napongeza pia kwa kazi kubwa mliyoifanya kwa kuondoa kodi hasa kwenye mazao wanayozalisha wakulima wadogo wadogo. Wakulima wamekuwa wakipata shida sana na bei ya mazao imekuwa haipandi kwa sababu ya kodi nyingi ambazo wanawekewa hawa wakulima. Kwa hiyo, napongeza kwamba mmeondoa hizi kodi, naamini sasa wataweza kuuza kwa bei nzuri na hatimaye kupata faida kutokana na shughuli zao za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo pengine tuliangalie vizuri. Kule Lupembe katika Jimbo langu, tuna kilimo cha miti; tunapanda miti na tunahamasisha watu wapande miti kama zao la biashara. Sasa inapofika wakati huyu mkulima ametunza miti yake, anaenda kuuza sokoni, anakutana na kodi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kodi anayolipa anatakiwa kulipa transit pass ambayo inalipwa Serikali Kuu Sh.15,000/=, anatakiwa kulipa TP katika Halmashauri ambayo ni Sh.3,000/=, anatakiwa kulipa ushuru wa mbao ambao ni Sh.200/= kwa kila mbao, lakini pia anatakiwa kulipa ushuru wa leseni ya biashara ambayo ni Sh. 261,000/= kila mwaka, anatakiwa alipe kodi ya mapato ambayo ni Sh.1,500,000/= kwa mwaka, anatakiwa alipe leseni ya uvunaji ambayo ni Sh.261,000/= na vile vile anatakiwa akodi gari kwa Sh.3,000,000/= ili aweze kufikisha mzigo wake pale Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hizi kodi ni nyingi mno. Anaambiwa kwamba unapokuwa amelipa hizo kodi mbalimbali ni lazima awe na risiti ya EFD. Huyu mkulima amelima miti yake, ameungana pengine na wenzake au yeye mwenyewe ameamua kuipeleka sokoni ili aweze kupata bei nzuri. Anapopeleka sokoni anakutana na hiki kikwazo kwamba lazima awe na risiti ya EFD; huyu mkulima hana mashine, atapata wapi risiti ya EFD zaidi ya ile risiti ambayo inakatwa na Halmashauri na risiti nyingine za ushuru ambazo nimeziorodhesha hapa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuliangalia hili. Kwa kweli wakulima wa miti wa Njombe, Lupembe na maeneo mengine ya Njombe tunaozalisha miti, imekuwa ni kero kubwa sana kwao. Hebu Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango ajaribu kuziangalia hizi kodi ambazo wakulima wetu wamekuwa wakitozwa wanapokuwa wanasafirisha huu mzigo wa mbao ambao wameuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijaribu kusema pia kodi moja ambayo ni kero kwenye maeneo mengi lakini pia na kwenye eneo letu sisi. Kuna hii kodi ya SDL (Service Development Levy) ambayo inatozwa kwa kutoa huduma; wanalipa kwenye mashule lakini pia wanalipa wafanyabiashara. Hebu tujaribu kutoa ufafanuzi mzuri na tujaribu kuwaelimisha na kutoa elimu ya kodi vizuri ili waweze kuielewa, maana ilivyo sasa hivi hawaelewi vizuri. Kwa mfano, kwenye shule wamekuwa wakitoa hizi kodi nyingine nyingi lakini pia wanalipa na hii kodi ya Service Levy na wakati huo huo wanatakiwa warejeshewe fedha zile kwa ajili ya kuendeleza mafunzo ya ufundi, lakini shule zimekuwa hazipewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tujaribu kuziangalia hizi kodi na ikiwezekana tukae na hawa wenye shule na wafanyabiashara ili wasione kama ni kero. Waelimishwe vizuri, naamini wakielewa vizuri wataweza kulipa hii kodi vizuri bila tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi nyingine ambayo ni kodi ya uanzishwaji wa maduka ya madawa. Nawapongeza sana, imeshaondolewa, nayo ilikuwa ni kero kubwa; lakini mmesahau kodi ya uanzishwaji wa maabara. Maana duka la madawa linaendana na maabara. Kwa sababu kuwa na duka la madawa maana yake kuna Daktari ambaye kabla ya kutoa prescription anatakiwa aende kwenye maabara huyu mgonjwa akapime na akishapimwa arudi kuandikiwa dawa. Sasa kwenye maabara hamjatoa hizi kodi. Mpaka sasa hivi wanalipa kodi kwa maana ya uanzishwaji wa maabara Sh.330,000/= kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama basi ajaribu kuaingalia hii kodi pia, maana wenye maabara wanalalamika kwamba kwa nini wao wamesahaulika wakati wenzao wamepewa hilo punguzo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme juu ya maji vijijini. Wote tunajua Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakipiga kelele sana juu ya tatizo la maji vijijini. Maji yamekuwa yakipoteza muda mwingi sana wa akinamama na mabinti zetu kwenda kutafuta maji. Naomba katika ile Sh.40/= basi fedha hiyo iende kwa ajili kuongezea kwenye Sh.50/= ya zamani ili iwe Sh.90/= ili usambazaji wa maji uweze kuongezeka na hatimaye mama zetu hawa wasipoteze muda mwingi kwenda kutafuta maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anaweka mambo haya sawa tujue hii Sh.40/= inaenda wapi? Wengine wamelalamika kwamba Sh.40/= ni kubwa inaongezea wananchi gharama. Wamesema wasafirishaji hapa kwamba haiongezi chochote kwa maana ya gharama za nauli. Kwa hiyo, kama haiongezi chochote na watumiaji wa mafuta ya dizeli na petroli ni watu wenye magari au ni watu ambao wana bodaboda, naamini kwamba wana uwezo wa kustahimili kulipa hii Sh.40/= ambayo imeongezwa kwenye tozo za mafuta ili wananchi wetu waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya miradi ya umeme kwa maana ya REA. Naipongeza sana Serikali kwa kuanzisha utaratibu huu kuhakikisha kwamba kila kijiji sasa kinapata umeme. Nashukuru, nimeona kwenye mpango katika vijiji vyangu vyote; Vijiji vya Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe vimeshawekwa kwenye mpango wa kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba watakapofika wasisahau maeneo au kusiwepo na vitongoji vitakavyopitilizwa bila kuwa na umeme au havishushiwi umeme kwenye eneo fulani ili kusiwe na ugomvi au kusiwe na malalamiko ya wananchi ambao hawajapata umeme kwenye Vitongoji. Kwa hiyo, naamini Serikali yangu, naamini Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini yupo, basi mtahakikisha kwamba kila kijiji na kila kitongoji kinakuwa na umeme ili wananchi wetu waweze kutumia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo…
(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)