Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo.

Nachukua nafasi hii kuwashukuru Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na wafanyakazi wote wa Wizara hii wakiongozwa na Katibu Mkuu wao. Nachukua nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa nguvu na juhudi kubwa anazozifanya katika kuokoa mali ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili iko dhana inajengwa hapa kwamba Rais Magufuli anafanya kazi yake bila kuhusisha Chama cha Mapinduzi. Sasa leo nimekuja hapa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuonesha wenzetu kwamba Rais hafanyi mambo yake, anafanya ya Chama cha Mapinduzi. Baadaye kama kuna mtu anahitaji Ilani hii tutampa aisome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kunukuu maandishi ya Chama cha Mapinduzi kwa ujumla wake. Na. 4 inasema:-

“Katika miaka mitano ijayo 2015 - 2020, CCM ikiwa madarakani itaelekeza Serikali zake kutumia nguvu zake zote kuendeleza na kupambana na changamoto kubwa nne.

(i) kuondoa umaskini; kupambana na makinikia, kuzia wizi ni kupambana na umaskini;

(ii) Kupunguza tatizo la kukosefu wa ajira hasa kwa vijana wetu. Kutafuta fedha zinazoibiwa ni kuleta ajira ambayo tutaitumia baadaye kwenye viwanda; na

(iii) Kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hii ni ilani inayozungumza mambo hayo, maana yake CCM tunaelekeza kwamba Rais wa kwetu atakayepatikana atatekeleza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikutosha tukasema, sambamba na kupambana na tatizo la rushwa, Serikali pia zinaelekezwa na CCM, zinatakiwa kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu na wizi wa mali ya umma. Kwa hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John PombeMagufuli anatekeleza yale tuliyomwelekeza Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ile dhana inayojengwa kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli anafanya yake, siyo kweli na yako mengi humu ndani. Mkitaka tutawapa mwendelee kusoma hayo mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo nayashangaa humu ndani, nayashangaa sana. Leo duniani kote, Korea Kusini pamoja na vita waliyonayo na Korea Kaskazini wamemfukuza Rais wao kwa sababu ya ubadhirifu; leo Brazil pamoja na umaskini ambao umekithiri, wamemfukuza Rais wao. Leo Urusi pamoja na juhudi kubwa za Putin lakini leo wanaandamana kwamba anakula rushwa. Sasa leo Rais wetu anapopambana kutoa rushwa na ubadhirifu, Venezuela nao wamemtoa Rais, naambiwa hapa. Rais wetu anapopambana kwenye mambo ya ubadhirifu, tunashindwa kumshangilia na kumpa na pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba siyo jambo jema, ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wote tukaungana pamoja, tukashughulikia ubadhirifu huu na bahati nzuri sasa taarifa zilikuwa hewani kwamba wale watu ambao mlikuwa mnasema watatupeleka Mahakamani, wameshakubali kulipa. Sasa shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelekezo haya sasa, niende kuchangia, nijielekeze kwenye mambo ya viwanda na kilimo. Tunapozungumza viwanda maana yake tunazungumza kilimo; tukiendeleza kilimo chetu, ni lazima tubadili kilimo chetu cha mazao mbalimbali ili kupata nakisi ambayo itasaidia kwenda kuendeleza viwanda. Ni lazima ufugaji wetu tuubadili ili tuweze kupata mazao bora kwa ajili ya kupata viwanda. Malighafi itakayopatikana katika kilimo na katika mifugo isaidie kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji kwenye Jimbo langu la Bunda ni tatizo kubwa sana na namshukuru Mheshimiwa Rais kwamba anapopambana na ufisadi huu hela zitapatikana ili zije kwenye maji katika Jimbo la Bunda. Tuna miradi mitatu ya maji; kuna mradi wa Nyamswa wa World Bank, mradi wa Kiloleli na Salamakati. Miradi yote hii haijaenda kwa sababu fedha hazijaenda kwenye maeneo yangu. Mheshimiwa Waziri anapokuwa kwenye bajeti yako, naomba ufikirie namna ya kupeleka fedha Bunda kwa ajili kuendeleza miradi yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya barabara. Tuna barabara ya Nyamswa – Bunda, barabara ya Makutano
– Sanzati – Nata na tuna barabara ambayo inakwenda kukasimiwa kuwa barabara ya TANROAD ya Mgeta – Siolisimba – Mikomalilo. Kwa hiyo, naomba maeneo haya tuzingatie wakati tunapokuwa tunafanya bajeti hiyo waone namna gani mnasaidia miradi yangu kwenye Wilaya ya Bunda na Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Hospitali yetu ya Kongwa Mkoa wa Mara, ni ya muda mrefu sana na tumeisemea sana. Tunaomba kipindi hiki cha bajeti waikumbuke Hospitali ya Kongwa ambayo ni Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Bandari yetu ya Musoma, hii ni bandari ya muda mrefu sana na kwa sasa hivi imechakaa. Tunaomba waitengee fedha na niliona wanaenda kuishughulikia. Kwa hiyo, waone namna gani ya kusaidia ili Mkoa wa Mara nao upate bandari na iweze kutumika vizuri. Bahati nzuri kuna meli ya MV Butiama ambayo iko Mwanza inatengenezwa. Kwa hiyo, ikitengemaa tuone namna ya kuifikisha Musoma kwa ajili ya kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna reli ya kutoka Tanga – Arusha – Musoma, tumeizungumza sana. Pamoja na kwamba tuna reli ya kati ambayo tunaipigia upatu, lakini hata reli hii inayotoka Tanga – Arusha – Musoma inaweza kusaidia katika maeneo yetu na kuendeleza uchumi wa watu wetu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tunazungumzia mambo ya wakulima, lazima tukubaliane namna ya kuboresha zao la pamba. Katika Mkoa wa Mara hakuna zao lingine la kibiashara, ni zao la pamba ambalo liko pale. Kwa hiyo, tunapokuwa tunazungumza haya mambo, ni lazima tuone ni namna gani tunapandisha bei ya pamba. Miaka mingi sana tumekuwa tukitegemea Soko la Dunia, lakini lazima tutegemee viwanda vyetu vya ndani ili tuweze kukuza bei ya pamba katika Mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya wafugaji. Tumekuwa na Kamati mbalimbali; kuna Kamati zimeundwa kwa Wizara tatu. Tunaomba zile Kamati zifike Mkoa wa Mara na hasa eneo moja linaitwa Kawanga kwenye Jimbo langu la Bunda ambako kuna migogoro mikubwa sana ya wafugaji kati ya Pori la Akiba la Ikorongo na eneo langu na Vijiji 15 vilivyopo kwenye maeneo haya ili tuweze kuona namna gani tunaweza kusaidia katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo mengi sana ya ndovu kwenye maeneo yetu. Tunaomba zile fidia ambazo zinahitajika kwenye maeneo haya; kuna Kijiji kimoja ama Vijiji vitatu vimebaki vya Maliwanda, Mgeta na Kyandege. Tuone namna ya kuvisaidia hivyo vijiji ambavyo havikupata fidia ya kifuta jasho ambapo vijiji vingine vimepata lakini vyenyewe havikupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda viwili vidogo vidogo vya maziwa, havifanyi kazi muda mrefu sana; kimoja kipo Kyandege na kingine kipo Mgeta. Kwa hiyo, tunaomba waone namna gani hivyo viwanda vinaweza kusaidiwa ili viweze kutoa mazao yao kwa ajili ya kuwapa faida wakulima wa maeneo hayo. Hivi viwanda vilijengwa enzi hizo za miaka ya nyuma tukiwa na Kiwanda cha Maziwa Musoma ambacho kimekufa, sasa tuone namna gani ya kuvifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vya pamba viwili; Ushashi na Bramba. Kwa hiyo, tunaomba tuweze kusaidiwa kuvifufua viwanda hivi kwa ajili pia ya kuongeza zao la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii zana inayozungumzwa ya tozo ya road license. Gharama za mafuta kwa miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikishuka sana, lakini hatujawahi kuona nauli ya kutoka Bunda kuja Dodoma inapungua. Kwa hiyo, hata tukipunguza habari ya mafuta, wala hawa watu wanaofanya biashara ya usafirishaji hawapunguzi gharama zao za nauli. Kwa hiyo, naona kwamba hii Sh.40/= tuliyoiweka tungeongeza Sh.10/= ili tuipeleke kwenye maji kwa ajili ya kusaidia akinamama wanaohangaika na maji kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tukiwa tunazungumza suala la walemavu, ni vizuri tukaona namna gani ya kupunguza baadhi ya gharama. Pamoja na kwamba zimepungua, lakini bado. Tuwasaidie walemavu katika maeneo mbalimbali na hasa wale watoto wanaotakiwa kusoma ili wapewe vifaa bora kwa ajili ya kujifunza na kwa ajili ya kupata manufaa katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapa ni kuhusu umiliki wa akinamama katika suala la ardhi. Sasa ni vizuri tukiwa tunazungumza hapa, tuone kama bajeti hizo zinawekwa kwenye maeneo haya ili tuweze kuona, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)