Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mwanakwerekwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema nami kupata fursa hii kuchangia katika bajeti hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika mambo manne ambayo zaidi ya haya yatakuwa yanahusiana na mambo yale ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 133 inaeleza kwamba kunatakiwa kuwe na Kamati ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia katika Ibara ya 134 ikaeleza majukumu ya Kamati hiyo, lakini pia kulitakiwa kuwe na Akaunti ya Pamoja ya Fedha baina ya Zanzibar na Tanganyika ili kuweza kuthibitisha mapato ya Muungano katika Akaunti hiyo ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukichukua Katiba hii mwaka 1977, mpaka leo hii ni miaka 40 sasa hivi na hii imepelekea Zanzibar kukosa fursa zote za kufanya maendeleo ya visiwa vya Zanzibar kwa sababu ya tatizo hili la kutokupatikana account ya pamoja, kuweza kuyajua mapato halisi ya Muungano na mgao halisi kwa nchi mbili hizi. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie kwamba sasa ni lini Akaunti hii itafunguliwa kwa ajili ya kuweka mapato yote ya Muungano ili upatikane mgao sahihi kwa ajili ya nchi hizi mbili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuchangia hapa katika Wizara ya Fedha kusema kwamba ukiangalia Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaonesha mambo yote ni ya Muungano. Leo ukimwangalia Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Nyumba, anaitwa ni Waziri Waziri wa Ardhi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; lakini ukija huku ndani tunawatafsiria watu tunasema kwamba ardhi siyo mambo ya Muungano, jambo ambalo Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano inakataa inasema kwamba yule ni Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ina maana mapato na ukiangalia kwamba kodi ya Mashirika, watu binafsi, ushuru wa forodha; haya yote ni mambo ya Muungano. Kwa hiyo, ukitazama kwamba kodi hizi zinapokusanywa kabla hazijaanza kutumiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano inakua ni mapato ya Jamhuri ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa muda wote huu, imepelekea kulifanya Taifa la Zanzibar kuwa Taifa dhoofu, kuwa Taifa ambalo halijui mustakabali wake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa leo atuambie sasa ni lini Akaunti hii inafunguliwa kwa ajili ya kudumisha mustakabali wa nchi hizi mbili?
TAARIFA . . .
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nafikiri Mheshimiwa hajaisoma Katiba vizuri. Katika Muungano huu mwanzo kulikuwa hakuna kitu kinaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kulikuwa na nchi ikiitwa Zanzibar ambayo mpaka leo inaitwa Zanzibar na nchi ambayo inaitwa Tanganyika. Tanganyika na Zanzibar ndiyo zimefanya kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa leo akitoa taarifa hiyo nitamshangaa sana. Kwa hiyo, naomba niendelee na mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, atueleleze hii akaunti ambayo imesemwa kwamba lazima kuwe na akaunti itakayothibitisha mapato ya Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, tuambiwe ni lini akaunti hii itaanzishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Visiwa ni tofauti na uchumi wa nchi ya Bara kama Tanganyika. Uchumi wa Visiwa siku zote ni uchumi wa huduma. Leo naomba nitoe mfano. Tuchukulie mfano wa nchi ya Singapore; Singapore ni Kisiwa kidogo, yaani kisiwa cha Unguja ni karibu mara mbili ya Singapore. Kisiwa hiki hakina resources za aina yoyote, isipokuwa wao wanatumia bandari na huduma ambazo wanatoa kwa Taasisi mbalimbali za kibiashara na kifedha duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo imekuwa kwamba Singapore, unapotaka huduma ya aina yoyote ya kifedha ama ya kibiashara unaipata Singapore. Ukiangalia leo Singapore wamewekeza katika bandari tu ya Singapore peke yake kwa siku inapokea makontena 91,000 ambayo ni sawa sawa na meli 60 zinazofunga kwa siku Singapore; na Kijiji chenyewe ni kidogo. Kama hiyo haitoshi, Singapore leo ndio wenye destination kubwa ya utalii. Meli zote za Kitalii ambazo zinakwenda katika sehemu mbalimbali duniani zinaanza safari zake kutoka Singapore.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa 2017 Singapore imefanya location ya meli za kitalii kwenda sehemu mbalimbali duniani 63. Crew Ship ambapo katika meli hizi watalii wanatoka Australia, Marekani, Ulaya na sehemu nyingine duniani wanakwenda Singapore. Wakifika Singapore wanapanda meli wanakwenda kwenye utalii wao, wakirudi wanarudi Singapore wanachukua ndege wanarudi makwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo cha ajabu, nashangaa, Mheshimiwa Waziri wa Utalii hapa kwetu, anashindwaje kuitumia fursa ya Zanzibar pamoja na Mbuga ama vivutio vya kiutalii vilivyopo Tanzania kuweza kuihuisha nchi hii kiuchumi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia Tanzania imekuwa maskini kwa sababu imeinyima fursa tu Zanzibar. Wakati aliyekuwa Waziri Mkuu wa Malaysia Dkt. Abdallah Mahadhir naye pia alikuwa na nia kama ambayo aliifanya Baba wa Taifa, kuifanya Singapore na Malaysia iwe ni nchi mmoja. Singapore wakakataa wakasema sisi tunataka tujiendeshe wenyewe na matokeo yake leo Singapore kwa kujiendesha wenyewe na kujitegemea imechochea maendeleo katika nchi ya Malaysia kwa haraka sana. Leo Malaysia ni miongoni mwa nchi ambazo zinakuwa kiuchumi kwa…
TAARIFA . . .
HE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu tafadhali. Inaonekana Mheshimiwa Keissy alikuwa hajasikia nazungumza nini, kwa sababu mwanzo nilinukuu hii Katiba. Hii Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inasema kwamba Waziri wa Utalii ni Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa sijui yeye anavyosema anafuata Katiba ipi? Kwa hiyo, inaonekana hata yeye mwenyewe hafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Singapore imechochea ukuaji wa kiuchumi wa nchi ya Malaysia na leo kila mtu anafananisha kwa kusema kwamba Malaysia inaendelea kiuchumi kwa haraka zaidi. Hii ni kutokana na Kisiwa cha Singapore kuweka uchumi wa huduma na kuiacha Malaysia iweze kujiendesha katika uchumi wa mazao na kibishara kupitia Singapore.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunampongeza Mheshimiwa Rais kwamba amefanya kazi nzuri ya kusimamia rasilimali za nchi hii ili watu ambao walikuwa wanazipora, sasa nchi hii iweze kunufaika. Nachukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Rais kwamba kama ambavyo amechukua juhudi kwa ajili ya kuzuia makinikia, sasa umefika wakati sasa wa kupata suluhisho katika Muungano wetu. Mwisho hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitujibu kwenye bajeti yake kwamba jambo hili bado lipo kwenye mazungumzo baina ya nchi mbili hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ikiwa leo tumeungana na sisi tunasema ni ndugu, miaka 40 hatujapata maelewano ya nchi hii kupata Akaunti ya Fedha ya Pamoja ya Jamhuri ya Muungano? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona sasa ifike mahali, kama ambavyo mmekubali kwamba mlifanya makosa katika mikataba ya madini, basi na hapa mkubali kwamba mliwakosea Wazanzibari na sasa tunaelekea katika mwanzo mpya kwa ajili ya kutafuta mustakabali wa Muungano wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ilikuja mifano mbalimbali. Mheshimiwa Rais Mstaafu alipendekeza, aliunda Kamati ya kutengeneza Katiba mpya; na tuliamini kwamba alikuwa na nia njema na Kamati hii ikafanya kazi ya Jaji Warioba, matokeo yake ilipokuja hapa Bungeni kwa sababu ile nia na dhamira ilikuwa bado, Katiba ile imekataliwa na matokeo yake watu wakatayarisha Katiba nyingine pendekezwa ambapo yale maoni ya wananchi yakakataliwa na yakatupwa pembeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alivyotokea Mheshimiwa Warioba, kutaka kutoa maelezo ya mambo yalivyokwenda, kilichofanyika, alitumiwa watu wa kwenda kumvamia na asitoe ule uhalisia wa mambo. Leo hii watu wale wale wameonekana ni watukufu, wametukuzwa kwa ajili ya kuonekana ni watu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.