Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti,Bismillah Rahman Rahim.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza na Mwenyezi Mungu anijalie hilo nitakalolizungumza liwe ni haki na ukweli. Tukisimamia haki tutafikia mahali ambapo nchi hii tutaitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge inabidi turudi Majimboni kwetu tukawaombe radhi wananchi wetu. Bunge hili ndilo tulipitisha haya mambo, lakini leo wanaichukulia hii hoja kuwa ni hoja ya sehemu moja, kuona wao ndio wana hoja hii, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie kitu na Wabunge wote wanielewe, tuliapa kwa kushika Quran, tuliapa kwa kushika Biblia, hivi vitabu ni vya Mwenyezi Mungu na vitabu hivi havitakiwi kudanganya na kuvifanyia uwongo, mbele yetu kuna Mwenyezi Mungu. Unapoishika Biblia ukasema naapa na kumtanguliza Mungu katika Biblia halafu ukaja hapa ukazungumza uwongo ni dhambi kubwa, inabidi tukaombe radhi hiyo kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unashika Quran, ukasema naishika Quran kwa kuahidi na kuilinda kwa mujibu wa Sheria na Katiba halafu baadaye ukaja kuibadilisha kwa kuzungumza vingine hii ni laana kubwa. Kila siku unasema tumerogwa na nani? Imeturoga Quran, imeturoga Biblia. Mara nyingi ukiwa mkweli, unakuwa hukubaliki mahali popote pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi ni Mwenyekiti kipindi cha tatu hapa ndani na baadhi ya Wabunge tupo ndani kwa muda mrefu tunayaona haya.

Hata hivyo, kuna wakereketwa na wanaharakati walionyesha hii hali kuwa hali ya madini ni ngumu, nataka niwataje kwa majina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla Ubunge wake ulikuwa wa tabu kwa vile aliyasimamia kwa dhati kuhakikisha madini haya hayaharibiwi wala hayachakachuliwi, alipigwa mabomu, akadhalilishwa inabidi aombwe radhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kafulila alisimamia kwa dhati akaitwa tumbili humu ndani. Mheshimiwa Zitto Kabwe alikuja na hoja nzito ambazo zina mashiko lakini siku ya mwisho ndio inakuwa hapana na hapana inakuwa ndiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Rais ameonesha ushujaa kwa kukubali maamuzi na matakwa ya Wanaharakati hawa na akayafanyia kazi ndiyo hayo unayoyaona maamuzi mazuri yanakuja sasa hivi. Hivyo siyo hoja ambayo imeletwa na upande mmoja, hii ni dhambi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, jina nililopewa ni jina la sura pana, mnalikumbuka au hamlikumbuki Wabunge? Maana yake nilikuwa nasema kuna baadhi ya Wachina walikamatwa Arusha na madini ya Tanzanite ikasemekana hawajui Kiswahili na Kiingereza, wakaachiwa yale madini. Tulikuja kuhoji hapa ndani mwisho wa siku tukasema ndio akapita Mchina akaenda zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikamatwa Wachina na pembe za ndovu Rukwa, shahidi ni Mheshimiwa Jenista Mhagama nilikuwa naye katika ziara. Lori la pembe alilokamatwa nalo yule Mchina ikasemekana hajui Kiswahili na Kiingereza, Mheshimiwa Jenista ni shahidi na tulikuwa na Mheshimiwa Lekule Laizer, lakini mwisho wa siku tukasema ndio na hapana ikawa hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifikie mahali, juzi nilitoa taarifa nikasema mtakuwa tayari wenzetu penye ndio kusema hapana? Maana yake msiburuzwe kwa ndiyo wakati kuna hapana ndani yake. Kulikuwa na baadhi ya Wabunge walikuwa wanaona hiki kama tunachokifanya hiki ni dhambi kwa wananchi, sasa leo mnailetaje hoja hii ikawa ni hoja ya upande mmoja? Haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja ni ya Magufuli na wanaharakati na msiichukulie kama hoja ya kisiasa Wabunge wote iwe wa Upinzani, iwe wa CCM tushirikiane kwa hili. Unapoleta uchumi bora, huleti kwa upande mmoja ni kwa Watanzania wote, leo tunaiona Bulyankhulu watu ni maskini, unaiona Geita watu ni maskini, lakini umaskini huu umesababishwa na mikataba yetu mibovu na sisi wenyewe kusema ndio wakati ni hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tumeumbuka, kwa aibu hii hatuna haja ya kufumba macho na kupepesa macho, tuwaombe radhi wananchi. Narudia tena Wabunge tumeumbuka kwa hili, hakuna haja ya kupepesa macho, wala kumwambia mwenzako kumkodolea kwamba ni hoja ya CCM au hoja ya CUF au hoja ya CHADEMA, ni hoja ya Wabunge wote tumekosea humu ndani. Watu wengi walikuwa wanaangalia conflict of interest na conflict of interest ikajengea hoja tunaitana pembeni jamani tukubali, wakati unajua kabisa hiki ni hapana, hizi ni dhambi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa idhini ya Sheria za Bunge tutoe hii Kanuni ya kushika Quran na Biblia itatulaani humu ndani. Tunashika Biblia wakati Biblia haitamki uwongo, tunashika Quran haitamki uwongo, leo tunatamka uongo halafu baadaye tunakula matapishi, tunageuza leo, tunabeza na kukebehi na kuona wenzetu hawana hoja. Nani humu ndani atamwomba radhi Mheshimiwa Kafulila? Nauliza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba radhi Kafulila kwa vile Mheshimiwa Kafulila ameonewa wakati alikuwa analeta hoja ya kuisadia nchi hii. Tulikuja na hoja ya Tanzanite,

Tanzanite inatoka Tanzania, mimi nilikuwa New York pale karibu na UN nje kuna maduka ambayo yanauza madini, Wallah Tanzanite hiyo inaonekana inatoka Kenya, inatoka India, inatoka South Africa, niliuliza kwani hakuna Interpol? Jibu halipatikani, lakini leo hapa watu wanataka kufumua mapafu kuzungumza uwongo, dhambi kubwa sana na itatulaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimshukuru na nimpongeze Rais Magufuli kwa vile amethubutu na sisi wote tuungane kwa pamoja bila unafiki kumpongeza kwa kazi anayoifanya kubwa na inahatarisha maisha yake. Hivyo kila Mtanzania amwombee huruma kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo nakuja katika hoja iliyopo mezani. Leo tunasema tunataka uwekezaji wa viwanda, katika viwanda tumeona A to Z imekuja kufanya semina ngapi hapa ndani? Wanakuja wageni wanaingiza vyandarua bure, hawana tozo, yeye analipa bilioni 17 wale watu wameachiwa vilevile waingize vyandarua hakuna mahali palipobadilishwa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri wa Fedha tulikuwa naye katika semina ,akasema atalifanyia kazi, lakini nimeangalia katika vitabu hawa A to Z wameachwa hivi hivi, kiwanda chao kinakufa, wanalipa kodi, wana madeni na marekebisho hayajafanywa. Naomba Serikali hii kama tunavyosema ni Serikali sikivu iangalieni A to Z ili angalau yale maombi yao yasikilizwe yafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko humu ndani ya Bunge miaka mingi tumezungumzia suala la Dinosaur. Dinosaur yupo Ujerumani sisi hatutaki mjusi aje Tanzania lakini je, hata mrabaha haiwezekani? Tunakimbizana na mama lishe, tunakimbizana na watu wa mitumba, leo kuingia ndani ya exhibition unatoa Euro 24 kwa watu wazima na Euro 12 kwa vijana lakini watu wa ndaniā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)