Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi. Naipongeza Wizara ya Fedha, nimpongeze Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wenzake kwa bajeti nzuri sana. Kwa kweli ukiangalia bajeti ya mwaka jana na bajeti ya mwaka huu tofauti naiona ni kubwa. Bajeti hii wametusikiliza vizuri sana, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, China wameanza miaka mingi sana, maendeleo unayoyaona leo China yameanza mwaka 1978 baada ya Deng kuchukua ile nchi. Deng amechukua nchi lakini kwenye Serikali zilizopita alikuwamo. Brazil unayoiona leo maendeleo yameanza mwaka 1998 baada la Lula kuchukua ile nchi, kabla ya hapo alikuwa ni Kiongozi. Malaysia unayoina leo maendeleo yameanza mwaka 1980 baada ya Mahathir Mohamad ambaye kule nyuma alikuwa ni kiongozi alipochukua nchi. Sohat wa Indonesia baada ya kuchukua nchi ndio tuameanza kuona maendeleo makubwa ya Indonesia. Ethiopia unayoina ya leo yameanza mwaka 1992 baada ya Meles Zenawi kuchukua nchi, naweza nikataja Mataifa mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na hili kwa sababu gani Waheshimiwa Wabunge. Lazima Taifa lolote yuko mtu ambaye atakuja ndio atasababisha Taifa hilo liendelee. Nami naomba leo niseme kwamba ninayo hakika Rais Dkt. Magufuli atatupeleka kwenye uchumi wa kati.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Marais wote hawa nimewataja ambao wamefanya vizuri sana kwenye Mataifa yao wana sifa kubwa tatu, wote kwa maana ya Singapore Malaysia, Indonesia kote, kazi ya kwanza walifanya waliwekeza kwenye elimu, unaona Rais Magufuli ameingia kazi ya kwanza aliwekeza kwenye elimu. Wote kazi ya pili ni kusimamia nidhamu ya utekelezaji wa kazi, tunaona leo Serikalini kuna nidhamu kubwa sana. Sifa ya tatu ya Marais hao waliobadilisha nchi zao ni suala la kusimamia mapato na rasilimali za nchi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Dkt. Magufuli ameamua kusimamia kwa uthabiti kabisa rasilimali na mapato ya nchi yetu kwa sababu naamini Rais anatupeleka kwenye Taifa la maendeleo. Hata hili la makinikia, hili la madini ni katika ule mwendelezo wa kusimamia mapato na kusimamia rasilimali za Tanzania. Nilisema siku ile Rais Magufuli, anaenda kubadilisha namna ambavyo uchimbaji wa madini duniani utakavyofanyika. Kwa hiyo, yeye ndio atakuwa chachu alichofanya Rais Magufuli atazisaidia Kenya, Mali, Guinea atasaidia nchi zote kwa sababu sasa wote wanakwenda kwa kuamka na ninayo hakika sasa tutapata share yetu na tutaendelea kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimewasilikiza sana Wapinzani. Hakuna hata Mpinzani mmoja ambaye amesema Rais Magufuli anakosea, hakuna! Hata hivyo, Wapinzani kama walivyo Wapinzani wao wameamua kuwa Thomaso. Wanataka waone yatapotokea. Kwa hiyo, nawaelewa, mashaka yao nayaelewa ni mashaka ya Thomaso. Yesu amefufuka, Thomaso anamwambia Yesu naomba niangalie mahali palipochomwa mkuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaelewa wenzetu na ndiyo maana nasema, wao wanaonesha wasiwasi lakini hawasemi kama tumekosea. Nami naamini kazi anayofanya Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, anafanya kazi nzuri sana na Rais Mheshimiwa Magufuli anaendeleza pale walipoacha wenzake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kule nyuma kila Rais ataandika kitabu chake, Rais Dkt. Magufuli anaandika kitabu chake na kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Magufuli kitakuwa kitabu ambacho nina hakika kwenye historia ya nchi yetu ndio Rais tutakayesema alitutoa third world kutupeleka kwenye uchumi wa kati kama Taifa. Jukumu letu kama wanasiasa, tumuunge mkono ili aweze kufanya vizuri zaidi huko anakokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa nirudi kwenye bajeti. Naipongeza sana Serikali kwenye kubadili mfumo wa kukusanya Road License. Wako watu wanasema Road License imeondolewa; hapana, haijaondolewa. Road License imeletwa ili iwe rahisi kuikusanya na iwe rahisi kwa sisi tunaochangia lakini pia itozwe kwa magari yanayofanya kazi. Naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naiomba Serikali tulikazanie, ni suala la deni la ndani. Leo hii ukienda nchini, malalamiko ni kwamba pesa hazipo, wanasema liquidity haiko kwenye market. Liquidity haipo kwa sababu watu wengi ambao wamefanya biashara na Serikali wanatudai. Naiomba Serikali ije na mkakati wa kulipa madeni ya ndani. Tukifanya hivyo, uchumi wetu utaanza kukua kwa kasi kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa suala la asilimia 18 ya VAT kwenye auxiliary. Sasa mnaisaidia bandari yetu, lakini naomba suala la single custom na DRC tuliondoe ili single custom itusaidie na watu wengi watumie Bandari za Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Rais ameamua kwa dhati kufufua Shirika la Ndege la Tanzania na amenunua ndege kubwa. Zile ndege kubwa zitakuwa zinasafiri kwenda kwenye Mataifa makubwa duniani. Moja ya gharama kubwa ya ndege ni mafuta ya ndege. Tumeamua wenyewe kama Serikali; kama Afrika Mashariki, mafuta ya ndege yasitozwe kodi yoyote na yasitozwe RDL. Sisi bado tunang’ang’ania kuweka tozo hiyo. Tukiweka tozo hiyo, tunaongeza gharama za ndege. Tukiongeza gharama za ndege, tunaiumiza tourism yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho naomba leo niseme, shirika ambalo linatoa mafuta haya ya ndege ni Puma. Puma, Serikali ina asilima 50. Ukiliongezea gharama maana yake ni nini? Maana yake, profit and loss yao inakuwa kubwa, maana yake dividend itapungua, corporate tax itapungua na yote haya yatapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali; na bahati nzuri Kamati ya Bajeti kwenye ukurasa wa 41 mmeliandika hili jambo; nawaombeni sana mwende kwenye Finance Bill. Hii ni element ndogo sana, tukaliondoe ili nasi tuweze kuwa competitive na sisi ndege nyingi ziweze kuja kunywa mafuta hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuikumbusha Serikali, kila wanapoongelea reli ya kati wanaongelea Dar es Salaam
– Mwanza. Naombeni mkumbuke ni Dar es Salaam – Kigoma na matawi yake ya Mpanda na Mwanza lakini central line ni kwenda Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji ni kubwa sana, naombeni sana tuweke bajeti kubwa ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la soko la dhahabu. Musukuma amelisema hapa, tulisema mwaka 2016 na Bwana Kishimba, naombeni tuweke soko la dhahabu, halafu kwenye soko lile tuwaambie kila atakayeleta dhahabu msimwulize ameitoa wapi? Isipokuwa watakaokuja kununua ndio tuweke export levy. Tutakusanya pesa nyingi sana kama Taifa. Wala siyo hii asilimia tano ya wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo watakwepa, hatutoikusanya hii hela; lakini tukiwafanya waje kwenye soko, wanunuzi wakaja, tutapata fedha nyingi sana kama Taifa. Naombeni mwende mkalifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ten percent ya crude oil. Jamani, Kenya na Uganda hawana crude oil. Kitakachotokea, sisi tutakuwa soko la Kenya na Uganda, nasi hatuna mafuta mengi sana nchini jamani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kigoma tuna michikichi, lakini angalia mafuta ya michikichi yanayozaliwa Kigoma, huwezi kutumia hata kwa mwezi mmoja, ni machache. Nawaombeni sana tuwekeze kwenye mbegu na utafiti ili tuweze kuzalisha michikichi mingi na tuweze kuzalisha alizeti nyingi sana. Bila hivyo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)