Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa tukio hili ambalo linaendelea katika harakati zile zile za kutetea na kulinda maslahi ya Watanzania ili maslahi haya, rasilimali zetu ziweze kuwatetea na kuwasaidia hawa wanyonge hasa
akinamama ambao tuna shida ya afya na maji. Mungu ambariki sana Mheshimiwa Rais wetu achape kazi, tupo pamoja naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake kwa bajeti ambayo inatoa mwanga katika kumkomboa Mtanzania. Mambo hayawezi yakaja mara moja, ni taratibu, kwa hiyo, tuwape muda waweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nijikite kwa kuondoa upotoshaji. Nimesikiliza michango mingi, upotoshaji ni mkubwa kwa kusema kwamba Marais waliopita na awamu hii wanaendeleza umaskini, kwamba wamechangia kulipeleka Taifa hili kwenye umaskini na Chama cha Mapinduzi ndiyo kinachangia katika kuletea umaskini Taifa hili. Siyo kweli, huu ni upotoshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niwaambie wananchi, maendeleo yetu hadi yanafikia hapa, bajeti zetu hazitekezwi; mara asilimia 38, mara asilimia 40 ni kutokana na matatizo mbalimbali ambayo yamelikumba Taifa hili tangu tumepata uhuru hadi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi tu napenda nieleze kwamba viongozi hawa, tukimchukulia Baba wa Taifa amejitahidi sana kulitoa Taifa hili katika umasikini; juhudi zake wote tunazifahamu, lakini amekumbana na vikwazo vingi; vikwazo vya nje na vikwazo vya ndani. Kwa mfano, wakati tulipoanzisha Azimio la Arusha tumeona wafadhili wengi sana waki-withdraw misaada kwa sababu ya sera zetu. Wajerumani walitoa misaada na Waingereza walitoa misaada. Kwa hiyo, bajeti iliyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 1970, suala la oil bei yake ilikuwa kubwa sana. Export tulizotegemea zilishuka; kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, vita ya Kagera na mambo mengine yote hayo yameyumbisha uchumi. Wakoloni nao hawakutuacha huru, wakaendeleza ukoloni mambo leo; kila tunavyojitahidi kujikwamua na wenyewe wanatukwamisha. Kwa hiyo, haya yote yanachangia katika kufanya bajeti zetu zisiwe za kutekelezwa kiurahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 1980 tukaachana na sera zetu, tukayumbishwa tena; tukaletewa zile sera za structure adjustment policies, tulikuwa hatutajiandaa ndiyo masuala ya ubinafsishaji, uwekezaji na hii mikataba mibovu ilipoanzia. Kwa hiyo, siyo kwamba ni mtu mmoja, ni timu ya wataalam mbalimbali. Wataalam hawa wanatoka wapi? Wanatoka kwenye vyama mbalimbali. Kwa hiyo, tusilaumiane, tuangalie tatizo ni nini? What is the root cause ambayo imetufikisha hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuangalie tutawezaje kujikwamua kwa haya Mataifa makubwa na sera zake? Sasa hivi tunashindwa kutekeleza malengo yetu, tunatekeleza malengo haya ya kidunia; ile Millennium Development Goals, sijui kuna ile 2030, yote haya yanaharibu. Tunashindwa ku- concentrate kuwaletea watu wetu mahitaji ya msingi, tunafanya mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zote hizi ni propaganda za Kizungu, lazima tuzitambue ili tuweze kuleta mshikamano katika Taifa letu. Wameshatugawanya na mambo ya vyama vingi, mambo ya NGOs na nini; yote hii ni divide and rule ili waweze kutuharibia. Kwa hiyo, Serikali inapopanga, huyu anakataa, huyu anafanya hivi, kunakuwa na mvutano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni matatizo ya ndani. Tumeona mambo ni mengi lakini rushwa na ufisadi ndiyo imetupelekea Taifa hili kufikia bajeti ambayo tunashindwa kuitekeleza. Pesa zinatolewa, miradi haitekelezwi, miradi hewa na Watumishi hewa, kwa hiyo, mambo yanakuwa mazito. Je, fisadi huyu ni nani? Fisadi huyu siyo wa Chama cha Mapinduzi peke yake; sio Rais wala siyo nani; ni sisi Watanzania hasa viongozi ambao tumepewa dhamana ya kuongoza Taifa hili kwa umoja wetu ndio tumefikisha hili tatizo katika mkanganyiko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tufike mahali tujitambue. Hata kama wewe unakuwa kwenye Upinzani, hata kama wewe ni mwanaharakati, lakini kitu cha kwanza simamia maslahi ya Taifa hili, wasitugawanye. Kwa mfano, nilitegemea tungepongeza, maana wale wengine mnasema walikuwa wapole, walikuwa hivi; sasa tumempata Mheshimiwa Rais huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Bunge la Katiba kila mtu aliyesimama alisema tunataka Rais atakayethubutu, Rais sio mwoga, Rais mzalendo na anayesimamia watu na wengine mpaka wakatumia Rais mwenye kichwa cha mwendawazimu, maana yake haogopi; Rais huyo tumempata, ndio Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Anafanya kazi kutetea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitegemea kwa mfano, juzi wakati anapambana na hili suala la madini ambalo limechukua trillions of money kwenda huko nje, nilitegemea Watanzania wote bila kujali itikadi zetu tungemuunga mkono. Hapa tunashuhudia Wabunge wengine wanaunga mkono na wengine wanakataa. Kwa nini? Kwa sababu tumeshagawanywa. Kwa hiyo, hali hii ikiendelea haitatuletea tija katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea wanasheria wa nchi hii wangeungana kumsaidia Mheshimiwa Rais ili kuweza kuiangalia upya hii mikataba. Hivi kama Mwanasheria anaweza akaungaunga aka-forge akamtetea yule muuaji kwa kutumia hizo sijui technical nini, kwa nini wasiungane ili kumsaidia Mheshimiwa Rais kutengeneza na kutetea haki zetu ambazo zimepotea na tunazidai? Badala yake tunaanza kubeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili Taifa mimi nasema tukifikia mgawanyiko huu kwamba kwa sababu Serikali hii labda ni ya Chama cha Mapinduzi, mimi niko huku, hatutafika na hizi ni mbinu na propaganda za mabeberu ili watugawanye waendelee kutunyanyasa na kuchukua rasilimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wenzangu, tuamke tujitambue sasa ili tuweze kuhakikisha rasilimali zetu tunazilinda. Tanzania kwanza mambo mengine baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa kwa upande wa bajeti. Bajeti yetu ni nzuri, kwa mfano suala la kumkomboa mkulima na tozo mbalimbali. Mimi nitazungumzia suala la kodi ya majengo. Nia ni kuondoa umaskini, lakini sasa kidogo nina wasiwasi pale ambapo malipo yamewekwa kwa flat rate ya Sh.10,000/= na Sh.50,000/= kwa nyumba ambazo hazijathaminiwa. Naomba kuuliza, je, hizi zikithaminiwa ina maana kodi itakuwa juu zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kuhusu nyumba za kuishi; leo mtu yupo kazini au amefanya biashara au leo ni Mbunge umepata mkopo ukatengeneza nyumba nzuri, baada ya hapo huna kazi, biashara ilikufa halafu nyumba ile sasa imethaminiwa ulipe labda Sh.300,000/= auSh.400,000/=. Hii itaishia kwamba huyu mtu atanyang’anywa ile nyumba kwa sababu ile nyumba haizalishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, nyumba za kuishi zote, contribution ni lazima katika kuleta maendeleo; iwepo labda hata kati ya Sh.2,000/= kwa zile ambazo vigezo vyake ni vya chini, labda mwisho iwe ni Sh.50,000/= ili watu waweze ku-afford. Otherwise tutaenda tu kuuza nyumba za hawa wananchi ambao sasa hivi kazi hakuna. Unasema huyu ana mtoto, watoto wenyewe kazi hawana, tunao majumbani. Kwa hiyo, tutaishia kuendeleza umaskini. Bora mtu awe na nyumba yake, asubuhi anajua akagange vipi. Kwa hiyo, naishauri Serikali hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala maji ni muhimu sana katika ku-stimulate maendeleo, kwa hiyo, tunaomba sana, akinamama na watoto wetu wa kike wananyanyasika, wanapigwa, wanabakwa na ndoa zinavunjika kwa sababu ya maji. Kwa hiyo, naiomba Serikali, bajeti ya maji hii na nawaunga mkono wenzangu kwamba ile Sh.50/= iongezwe ili akinamama waondolewe hii adha, kwa sababu pia watapunguziwa muda. Time factor ni muhimu sana katika suala la maendeleo. Watapata maji jirani, lakini watafanya na shughuli nyingine za uzalishaji na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la mazingira. Suala la mazingira linatu-cost sana katika nchi yetu hii. Wote tunashuhudia mazingira sasa hivi yanaharibiwa mno. Tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)