Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye hoja muhimu hii ya bajeti ya Serikali. Kwanza nianze kumshukuru sana Mungu kwa yote kwa afya na haya yote yanayoendelea, naamini mkono wa Mungu unaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri. Napongeza kwa dhati kabisa na wakati hotuba hii inasomwa, Waheshimiwa Wabunge wengi tulishangilia na yale tuliyokuwa tunayashangilia, naipongeza pia Kamati kwamba imeyazungumza. Sehemu ya tano ukisoma utaona namna Kamati imejaribu kuchambua na kuweka kielelezo namna bajeti hii ilivyoweza kukidhi mambo kadha wa kadha. Hii ni pamoja na kuiangalia hii sura ya bajeti. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niseme kwamba unaweza ukaangalia mafanikio ya bajeti hii na hususani bajeti iliyopita kwa kuangalia yale matokeo (outcomes) kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo, lazima nishukuru sana kwa sababu Jimbo la kwetu ni jipya, Halmashauri ya kwetu ni mpya; hivi sasa tunaendelea kujenga Ofisi kwa kasi; fedha tunazo; tumejenga mashule; kuna maeneo ya maji, tunaendelea kupata huduma za maji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi siwezi kuyasema yote, nashukuru kwamba hii hotuba ni nzuri kwa sababu ukiangalia bajeti zilizopita ukilinganisha na bajeti hii, utakubaliana nami kwamba kwa kweli hii ni hatua nzuri. Nami naipongeza Serikali iendelee na mwendo huu, tutafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nizungumze hili suala muhimu la madini. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu tulikuwa na kiu ya kuyaona mengi na yako mengi ambayo pia yanakwenda kugusa Halmashauri zetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu kama ambavyo nilisema wakati uliopita nilipokuwa nachangia hapa, kwamba ile dhamira nzuri ya Mheshimiwa Rais ndiyo hasa itaweza kuleta msukumo huku chini ili tuweze kufika pale tunapotaka kwenda. Nina uhakika tunakwenda kwenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia baadhi ya figures za report hizi zilizotoka, nikawa najaribu kuona sisi kwenye Halmashauri zetu za Kahama tukiwa na Majimbo matatu ya Msalala, Kahama Mjini na Ushetu, utaona hapa service levy ambayo nikiitaja utajua tulikuwa tumepoteza mapato mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia kwenye dhahabu peke yake kwa report hii, kwa kile kiwango cha chini cha upotevu wa mapato, tumepoteza service levy ya shilingi bilioni 324 kwenye dhahabu peke yake; lakini tukawa na shilingi bilioni 549 kwa kiwango cha juu kwenye dhahabu peke yake. Ukiangalia kwenye madini mengine 13 yaliyoorodheshwa na Tume, utaona kabisa tulikuwa tumepoteza yapata kama shilingi bilioni 397 kwa upande wa madini yote na kwa kiwango cha chini; na kiwango cha juu tunakwenda kwenye shilingi bilioni 689. Nazungumza kwa upande wa hili zoezi lililofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kuangalia kwenye upande wa service levy tulizopoteza kwa wale waliotoa huduma kwenye migodi wakiwemo wale waliofanya insurance, wale waliofanya consultation, waliouza mafuta; naomba sasa hapa Mheshimiwa Waziri atusaidie kwa sababu tulikuwa na shida ya kupata information.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaweza kupata financial statement tangu migodi hii ilivyoanza itatusaidia nasi kwenye Halmashauri zetu kuona wale waliotoa huduma kwenye migodi kama tulipoteza. Tulishaanza hilo zoezi kutafuta hizo information. Tunajua kuna kiasi kikubwa ambacho kingeweza kusaidia Halmashauri zetu. Kuna kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uone kabisa kwamba Mheshimiwa Rais ameanza nasi huku tunaendelea kupigana. Hata alipotembelea Shinyanga wakati ule, nakumbuka ndugu yangu Mheshimiwa Kishimba, Mbunge wa Kahama Mjini alizungumza, tumwombe Mheshimiwa Rais atusaidie kwa sababu tunaona tumepoteza service levy nyingi. Kwa hiyo, kwa upande wa Serikali mnaweza kutusaidia ili tuweze kukomboa na kupeleka maendeleo kwa watu wetu. Sura ya Kahama ilivyo, sivyo inavyotakiwa kuwa kwa fedha nyingi ambazo tunatakiwa kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumze kwa ufupi ni kuhusu hizi takwimu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hata bajeti iliyopita nilikuwa nimeomba kwamba Ofisi ya Takwimu tuisaidie sana iwe na watu wa kutosha, iwe na vifaa vya kutosha ili tuweze kupata data muhimu za kutusaidia kuweza kufanya mambo mbalimbali, kwa sababu ukija kuona hapa, data nyingi ambazo tunazitumia kwenye records zetu za bajeti na kadhalika, nyingi tunatumia ambazo ni wastani, tunatumia average, lakini sasa tukitumia average tunaacha group kubwa la watu nje ya hizo data ambazo tunazipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati mwingine tunahitaji wataalam wasaidie Ofisi yako kwenda kwenye measures nyingine. Waangalie measures of dispersion ili tuweze kuona tunavyozungumza kwamba wastani wa kipato ni shilingi milioni mbili, lakini tumewaacha watu wangapi nje ya msitari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiria kwamba Ofisi hii iboreshwe, itatusaidia pia kuweza kufanya decision nyingi, tuweze kuona pia tuna income gap ya namna gani? Bajeti iliyotangulia, tuliona pia hata Mikoa ambayo iliyokuwa chini ya mstari wa umaskini. Kwa hiyo, nashauri tu Mheshimiwa Waziri, hii Ofisi ni muhimu sana kuiangalia kwa jicho la kipekee itusaidie kupata information za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo suala la kodi kwenye assessment. Nataka nizungumze tu kwa sababu Commissioner naamini anaweza kuwa yuko hapa. Kwa miaka mingi tumechukua hii kwa kutumia band, tunachukua blanket tu kwenye maeneo fulani. Sasa nafikiri tuendelee kufanya analysis ili mlipa kodi alipe fair kodi kulingana na kipato chake. Kwa sababu utakuja kuona kuna maeneo mengi tunatoza kodi kutokana na eneo, hatuendi kutoza kutokana na uhalisi wa mtu anavyopata kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, twende zaidi kuboresha taarifa zetu ili tutoze kwa usahihi. Kwa hiyo, utaona maeneo mengine kwa mfano, kwenye Mji tunasema labda wafanyabiashara wanaofanana kwenye Mji fulani watozwe kiasi hiki kwenye kodi ya mapato. Kwa hiyo, nafikiri twende zaidi ili tuweze kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hili kwenye zoezi la utozaji wa kodi ya majengo, tukisema tunakwenda kumtoza mtu mwenye ghorofa la Sh.50,000/=, lakini mwenye ghorofa kuna mwingine anaweza akawa ametengeneza kwa leisure tu. Kwa mfano, ndugu zangu Wangoni kule nilikuwa nikienda naona wana maghorofa ambayo wameezeka kwa nyasi. Nilikuwa nakwenda Mbinga, nilishuhudia kuna watu wametengeza maghorofa hayo. Kwa hiyo, tuangalie ili tutoze kutokana na thamani. Vile vile wako watu wengine wana nyumba zao wamepangisha; tukitazama vizuri, tutaona kuna watu ambao wanaweza wakatupa kodi nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa sababu ya muda, nataka nizungumzie juu ya sura ya bajeti. Naona kabisa kwamba upande wa madeni hasa deni la Taifa, tuki- manage vizuri hili deni, utaona kabisa kwamba makusanyo yetu ukiwianisha na hali halisi ya matumizi, kidogo kuna uwiano mzuri. Kwa hiyo, tunakusanya shilingi trilioni 19.2 kwenye mapato ya TRA, kwenye non-tax revenue pamoja na Halmashauri, lakini matumizi yake bila kutoa madeni ambayo tunakwenda kulipa, tuko kwenye shilingi trilioni 22. Kwa hiyo, kuna gap kidogo la shilingi trilioni kama 2.9 hivi. Kwa hiyo, tunahitaji ku-manage vizuri hili deni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona sasa hivi tunakwenda kulipa deni lakini utaona tunakopa shilingi trilioni 11 mkopo wa ndani na nje, lakini tunakwenda kulipa shilingi trilioni tisa. Kwa hiyo, hili gap la deni litaendelea kuzidi. Kwa hiyo, naomba tufanye effort kupunguza hili deni ili siku za usoni tukope kidogo, tulipe kidogo ili tuweze kujenga uwezo mkubwa wa kupeleka fedha nyingi kwenye eneo la maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuzungumzia juu ya upande huu wa nakisi ya bajeti. Nilikuwa najaribu kuangalia hapa kwamba tumepata nakisi ya bajeti ya 3.8 lakini hapa tumezingatia mapato ya mikopo nafuu kutoka nje, tumewianisha na GDP. Tumeacha pia hii mikopo mingine ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara ambayo ukijumlisha na mikopo ya ndani tunakuwa na shilingi trilioni
11. Sasa nikiwianisha na pato la Taifa, tunaona kwamba ule uwezo wetu wa ku-deal na government spending unakuwa uko short kwa asilimia 11.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiria lazima tutazame yote kwamba tuna uwezo wa kukusanya kodi, tuna uwezo wa kukusanya mapato ya ndani mengine yale pamoja na Halmashauri zetu, lakini ule uwezo wa sisi kupata fedha kutoka nje ya makusanyo yetu tunapungukiwa asilimia 11.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri tulitazame kwa sababu tukitazama upande huu wa mapato ya mikopo nafuu kutoka nje pake yake ya shilingi trilioni tatu, nafikiri siyo sahihi kuweza kuiona hii nakisi ya bajeti. Kwa sababu nilikuwa najaribu kuangalia nchi mbalimbali, nimeona Uholanzi wana- shoot kutoka 2.8 hadi 2.5, Marekani wana 3 - 3.5. Ukiona range, iko within lakiniā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)