Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu lakini nipongeze sana Wizara, Waziri na Naibu wake kwa kutuletea bajeti nzuri ambayo inajali maisha ya Watanzania wa hali ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli ameonesha dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia Watanzania. Nimpe moyo tu hata Mitume nao wakati wanakuja walitokea watu ambao hawakuwaunga mkono lakini leo bado tunaendelea kuwaabudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yetu ni nzuri sana, kwa kweli inatufanya tutembee kifua mbele. Yako mambo machache ambayo nami napenda niyazungumzie. Nianze na eneo ambalo bajeti imelizungumzia na nipongeze sana Wizara kwa kuondoa kodi kwenye mazao ya biashara na kilimo. Kwenye eneo hili yametajwa mazao hapa kama vile chai, pamba na mengine lakini alizeti halijaangaliwa na Mkoa wa Singida sisi ni maarufu sana na ndiyo waasisi wa zao hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza nini hapa? Takwimu inatuambia Tanzania tunatumia karibu tani laki nne za mafuta, lakini tani laki mbili na themanini ni (importation) yanatoka nje, palm oil zinazobaki ndizo tani ambazo sisi tunatumia kama laki moja na ishirini. Serikali leo tunazungumza kuwekeza katika viwanda vyetu vya ndani na lazima tujikite katika kuwakomboa wakulima wetu na ni lazima tuhakikishe kwamba mazao ya kwetu tunayapa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mkulima akilima alizeti yake akishaisindika tu maana yake analipa VAT asilimia 18. Huyo huyo mkulima tunamtarajia aende akaongeze angalau heka moja, mbili hawezi, matokeo yake wakulima wote wa alizeti wanaiuza alizeti ikiwa shambani, ndiyo maana uzalishaji unakuwa mdogo. Mafuta ya alizeti tukiyaangalia na ndiyo mafuta bora yana cholesterol ndogo ya asilimia 17 kulinganisha na mafuta mengine yote ambayo yana zaidi ya cholesterol asilimia 60. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuta yanayoagizwa nje ni asilimia 70, yanayobaki ni asilimia 30 mafuta yetu ya ndani. Sasa kama Serikali ina lengo la ku-promote tuweze kutumia mafuta yetu ya ndani hasa alizeti tulikuwa na kila sababu ya kuhakikisha tunaondoa hii kodi ya VAT. Serikali imeongeza asilimia 10 kwenye importation ya mafuta yanayotoka nje, mwenzangu aliyepita amesema iongezwe iwekwe hata asilimia 15 na mimi namuunga mkono kwenye hilo, kwa sababu kama tuna lengo la kulinda viwanda vyetu vya ndani basi niiombe Serikali iondoe kodi hii ya asilimia kumi na nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwomb sana Mheshimiwa Waziri, sisi tunaotoka kwenye maeneo haya alizeti ndiyo zao kuu Mkoa wa Singida ambalo uzalishaji wake unashuka kila kukicha, kwa sababu wametuwekea VAT bila sababu ya msingi. Mwaka 2010 tulikuwa na zero rate lakini tumekwenda mwaka 2014 wametuwekea VAT lakini hakuna sababu ya msingi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri awajali wakulima hawa wa zao hili la alizeti ili tuweze kuwasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pale Singida tunalima sana kitunguu na kitunguu bora kinatoka Singida. Wakati nauliza swali mwanzoni Serikali iliji-commit kwamba itakwenda kutujengea soko la kisasa la vitunguu. Sisi tumekwishatenga eneo na Mheshimiwa Rais alianza ziara yake ya kwanza Mkoa wa Singida namshukuru sana na katika ziara ile aliwaahidi Wanasingida kwamba sasa anahitaji vile vitunguu tuweze kufanya packing pale pale Mkoani Singida badala ya kubeba kitunguu kikiwa raw kiende kufanyiwa packing Kenya na maeneo mengine. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, tumeshaandaa eneo, tuna vitunguu vya kutosha, waje mtusaidie kujenga lile soko liwe soko la kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali imewatambua wafanyabiashara wadogo wadogo, mama lishe, Wamachinga na wengine. Hata hivyo, nilikuwa najaribu kuangalia hawa bodaboda na bajaji ni wafanyabiashara wa namna gani? Mkoa wa Singida hususan Singida Mjini tunao vijana wengi sana na eneo hili la usafirishaji wameturahisishia sana sisi, lakini jambo la kushangaza, Mheshimiwa Waziri vijana wangu leo wanatozwa (income tax) kodi ya mapato ya Sh.150,000/= kwa mwaka bila sababu ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naanza kulalamika kwa nini wanatozwa nilimwandikia barua Meneja wa TRA, nashukuru sana kijana yule ni msikivu, lakini ananijibu kwa pikipiki moja bwana tutaacha lakini mmiliki wa pikipiki mbili atalipa Sh.150,000, tunakwenda wapi? Tunataka vijana hao wajiajiri na ajira Serikalini hamna, sasa leo kama watalipa income tax maana yake vijana wale watafanya kazi usiku, madhara ya usiku tunayajua, akishindwa kupata fedha ya kununua mafuta maana yake ataanza kufanya shughuli nyingine. Naomba tusiwaweke kwenye majaribu, Mheshimiwa Waziri hili ni eneo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Sheria ya Mapato mwaka 2014 ya kukusanya kila mahali sidhani kama ina tija kwa vijana wa bodaboda. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri vijana wangu pale mjini wako wengi, wamejiajiri na mimi ni sehemu ya shughuli zao na mimi ni mlezi wa eneo lao, niombe sana hili eneo kwa kweli kwangu wanatozwa Sh.150,000/= bodaboda na bajaji, hebu tuiondoe kodi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo lingine la maji. Nami niungane na wenzangu kwa kuongeza Sh.50/= kwenye maji lakini tunayo miradi ya vijiji 10 ambayo imekuja Singida lakini utekelezaji wake ni hafifu sana. Niombe eneo hili pia mtaenda kuliangalia kwa sababu ya muda nisieleze sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye milioni 50, kila Mbunge anasimama na vitabu vinaandika milioni 50 kila kijiji. Mheshimiwa Waziri hebu tuliweke vizuri hili sisi wengine tuna mitaa, sasa ukizungumza milioni 50 kila kijiji, mimi naenda kusimama naambiwa naletewa milioni 50 na sheria imekuja inasema milioni 50 kila kijiji, mitaa haipo. Naomba tuiweke vizuri wala hapa hakuna mgogoro, tuweke milioni 50 kila kijiji na kila mtaa ili wananchi wangu kote wapate, kwa sababu hii categorization ya vijiji na mtaa ni ya Kiserikali wala siyo ya kwetu, Watanzania ni wale wale tu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hili pia nalo aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la REA, tunazungumzia umeme vijijini. Sisi tunaoishi mjini maana yake ni kama unaambiwa wewe unaishi mjini umeme hauwezi kuja. Mimi nina vijiji 20 na mitaa havina umeme, Mheshimiwa Waziri hebu na jambo hili tuliangalie, tutazungumza lugha gani? Kama tunasema Serikali inaleta umeme lakini umeme unakwenda vijijini sisi tunaishi mjini, hatukuzaliwa kuishi mjini ili tukose hizi fursa ambazo Serikali inazitoa, wote tunaishi maisha sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni lazima Wizara iliangalie vizuri ituletee umeme, tusiwe watu wa kulalamika kwenye maeneo haya. Kama wenzetu wanapata umeme na sisi tupate umeme bila kujali vijijini wala mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida una rasilimali ya madini, eneo la Singida Mashariki, Singida Magharibi hali kadhalika Iramba kuna madini. Wako wawekezaji wanaitwa Shanta Gold Mine, wananchi kwa ridhaa yao wamepisha eneo lakini hawajalipwa fidia. Bahati mbaya sana kaka yangu Mheshimiwa Tundu Lissu hili hakuliona lakini naomba mimi niliseme kwa sababu mimi naishi mjini nahitaji waje wawekeze mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wale wawekezaji, Shanta Gold Mine sasa wana miaka mingi, wananchi wangu sasa wamebaki kuvamia kuanza kuchimbachimba kidogo kidogo yale madini yako ya kutosha, wanahitaji kulipwa fidia na ule uchimbaji uweze kuonekana. Mheshimiwa Rais keshatuonyesha njia sasa hatuna sababu ya kurudi nyuma. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.