Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Serikali. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipatia afya na kuweza kuchangia kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa sana anayoifanya. Kwa kweli, ni mtu anayestahili kufanya mambo anayoyafanya. Mheshimiwa Rais akisema anatenda, Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi kwa muda wa miezi 18 tu. Mheshimiwa Rais kwa kweli, kila mmoja anastahili kumpongeza kwa mambo yote anayowafanyia Watanzania. Amejitoa yeye mwenyewe na siyo yeye mwenyewe ni mkono wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana na namwombea Mwenyezi Mungu azidi kumlinda na azidi kumwongoza aweze kuishi maisha marefu. Hasa tendo hili la makinikia na kweli amelifanyia mambo mazuri, wengine wameanzisha lakini yeye mwenyewe nadhani atamalizia. Sasa hivi akikaa hivi karibuni mezani na hawa watu, fedha zitakuja, kila mmoja atatamani kuzitumia kwenye miradi yake. Kwa hiyo, naomba wote tuwe kitu kimoja, nchi yetu ni nzuri, nchi yetu ya Tanzania ina amani, naomba tuwe kitu kimoja hasa kushughulikia mambo haya yaliyo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Fedha pamoja na Makatibu wa Fedha na Manaibu wake. Kwa kweli, bajeti hii ni nzuri sana, inawajali Watanzania, inawajali wakulima, inawajali watu wote kwa wastani. Kwa hiyo, tunashukuru kwa bajeti hii nzuri ambayo mmetueletea ya shilingi trilioni 31.7 na kati ya hizo wamesema asilimia 38 ni fedha za maendeleo. Naomba hizi fedha za maendeleo ziweze kuja zote kama walivyozipanga kusudi miradi ya maendeleo ile ambayo ni viporo na ile ambayo bado iweze kutekelezeka. Kwa hiyo, naomba kitu kama hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati kwa ujenzi wa standard gauge, tunashukuru sana imeanza na wakandarasi wako tayari pale na itajengwa kwani tayari mkataba umeshawekwa saini ya kutoka Dar-es-Salaam mpaka Morogoro. Wamesema bado mnatafuta wafadhili kwa reli kuanzia Morogoro – Makutupora – Kigoma - Mwanza, naomba wafanye bidii sana kwa sababu reli hii inawasaidia watu wote. Reli hii haitachagua chama gani itawabeba watu wote wa kanda hizo hizo, kwa hiyo, naomba Serikali waifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalopenda kuliongelea ni tatizo la maji, kila mmoja humu anazungumzia tatizo la maji.

TAARIFA . . .

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu hata Mheshimwa Lowassa na yeye amemkubali Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia tatizo la maji, uwe Mbunge wa chama chochote kila mmoja anakiri kuwa ana tatizo la maji. Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasema kuja kufikia mwaka 2020 asilimia 85 vijijini wawe wamepata maji safi na salama na asilimia 95 mijini nao wawe wamepata maji safi na salama ili kusudi tuweze kuwatua ndoo kichwani wanawake. Kwa hiyo, naomba sana tena sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha hii ahadi iweze kutimilika maji yaweze kwenda vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana kwa kufuta leseni ya magari. Hii bajeti imepokelewa na watu wengi…

TAARIFA . . .

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siikubali hiyo taarifa, kama hajui kusoma aende akasome aangalie ni kitu gani kinatendeka huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia kufutwa kwa leseni ya magari. Nendeni kwenye mitandao ongea na watu wote, ongea na wasomi, ongea na kila mmoja, hii kweli anaiunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kutoa ushuru wa Sh.40/= kwa kila lita ya mafuta, nashauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha hizi hela ziweze kwenda kwenye Mfuko wa Maji. Nikiwa mwanamke nasisitiza hilo kwa sababu najua shida ya wanawake ambao wanatafuta maji pamoja na watoto wao, hizi hela ziweze kwenda kwenye Mfuko wa Maji. Nasisitiza kuwa asilimia 30 ya hizi fedha ziweze kwenda mjini pamoja na asilimia 70 ziende vijiji. Nasema hivi kwa sababu mjini inaweza kutokea taasisi zingine zikasaidia kugharamia maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, asilimia 65 ya wananchi wanategemea kilimo na malighafi nyingi zinatoka kwenye kilimo. Kwa hiyo, namwomba sana sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, fedha zilizotengwa kwenye kilimo ahakikishe zote zinakwenda kwenye kilimo kwa sababu bila ya kilimo hakuna viwanda, chakula na lishe ni duni. Kwa hiyo, naomba sana hizi hela ziweze kutoka zote tuweze kuinua pato la familia pamoja na pato la Taifa na hasa tukazanie kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa sababu wameweza kutoa tozo mbalimbali kwenye pembejeo na ushuru wa mazao asilimia tatu kwa bidhaa za biashara na asilimia tatu kwa bidhaa za chakula. Hata hivyo, katika mikoa mingine, kwa mfano, Morogoro tunalima mahindi, mpunga na viazi yote yanafanana ni biashara pamoja na chakula. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri tozo iwe moja kwa zao moja, iweze kufanana kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo tani moja ambayo wamesema kuwa kama unasafirisha kutoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine ushuru umefutwa. Mheshimiwa Waziri akija kuwa-wind up hapo aweze kulifafanua kwa sababu kuna wakulima wengine kwa mfano nakaa Manispaa ya Morogoro lakini nalima Halmashauri ya Morogoro Vijijini na ukisema tani ni magunia kumi, magunia kumi kwa wakulima wa kisasa wanavuna mpaka magunia ishirini, je, tozo itakuwaje na mimi ni mkulima siyo mfanyabiashara, nimevuna magunia yangu ishirini utanitoza ushuru? Naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie kusudi aweze kutushauri vizuri kama ushuru utakuwepo au hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye ufugaji, wafugaji kusamehewa malighafi ambayo inatengeneza chakula cha kuku, naishukuru sana Serikali na naipa pongezi. Wananchi wote ambao wanafuga kuku na hasa wanawake itawasaidia sana katika kufuga kuku na itasaidia kuongeza kipato, lishe pamoja na ajira hasa kwa vijana ambao wanamaliza shule na hawana kazi. Ushauri wangu, naomba waangalie mazingira mazuri ya kukopa na hasa Benki ya Kilimo pamoja na Dirisha la TIB, hela zote hizo walizozitenga ziweze kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mayai yanayototoleshwa na yenyewe inasaidia sana wafugaji. Wale wafugaji vifaranga vilikuwa bei ya juu sasa kwa kufanya hivyo bei ya vifaranga itapungua na gharama pia itapungua, pato litapanda na lishe pia litapanda. Ushauri wangu ni kama huo huo waangalie mazingira mazuri ya ukopaji na hasa Benki ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea kuhusu shamba la kilimo Mkulazi na Mbigiri ambayo tayari yako kwenye mchakato wa kujenga viwanda vya sukari na kilimo cha sukari. Nashauri waangalie out growers, hawa wakulima wetu wa Morogoro ambao wanazunguka mashamba hayo watafaidikaje? Naomba waangalie kusudi na wenyewe waweze kuwa kwenye mpango wa kupata na ajira itaongeze kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapato, kwa kweli nashukuru kuwa Sh.10,000/= ambayo wameiweka kwenye nyumba ambayo haijathaminishwa pamoja na Sh.50,000/= kwa nyumba ya ghorofa itasaidia kuongeza mapato yetu na hasa mapato ya ndani ambapo itasaidia kufanya mipango yetu ya maendeleo. Ila Mheshimiwa Waziri kama maswali yalivyokuwa yanaulizwa akija ku-wind-up aelezee kuwa tumeanza na hizi za Manispaa na Halmashauri ni lini na ni nyumba ya aina gani ambayo itatozwa Sh.10,000/= kama Wabunge wenzangu walivyouliza.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.