Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MCH. DKT. GETRUDE J. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Pia nashukuru kwa kazi yako nzuri sana ya kiwango unayoifanya, Mungu akubariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi adimu ya Rais wetu wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa kweli Rais Magufuli anastahili pongezi za dhati. Kama mtu haoni alichokifanya basi hana macho, huyu ni kipofu. Kama kweli yeye ni Mtanzania anasimama hapa siku zote anapinga ufisadi, anapinga mambo mabaya, halafu tena haoni alichokifanya, basi huyu mtu siyo Mtanzania halisi anajifanya tu. Inabidi tumwombee Rais wetu kwa hali na mali. Katika Isaya 54:17, unasema; kila silaha itakayoinuka juu yake isifanikiwe kwa Jina la Yesu. Kila ulimi utakaosimama kumpinga, tunaupinga wenyewe kwa Jina la Yesu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa fupi Jumapili ni Ibada Maalum ya kumwombea Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, kuombea Taifa letu na Bunge letu. Tutakuwa Mikocheni B, Kanisa la Mlima wa Moto, njooni jamani tukutane na Mungu aliye hai.
Hata kama unabisha lakini Mzungu si mmemwona, Mzungu si amekuja, amekuja mwenyewe bila kuitwa kwa tiketi yake. Amesema amekuja na ndege yake mwenyewe. Sasa kama amekuja kukubali yaishe kuna ubaya gani?
Si lazima tujipongeze. Hata kwa yale mazuri jamani pia tunapingana kwa vipi? Amekutana Ikulu, kumbe ulitaka akutane naye wapi Feri, Kariakoo au Buguruni au wapi? Nyumbani kwake si Ikulu amekutana naye, ni vizuri na wote tunashukuru, Mungu amejibu maombi.
Waseme wasiseme lakini hata nchi jirani wote wanasema, wanatupigia simu hongereni Tanzania, hongereni kwa kazi nzuri, hongereni kwa Rais mzuri. Kwa hiyo, lazima tumpongeze sana, amejitahidi kwa muda mfupi kaondoa wafanyakazi hewa, amegundua makontena ya mafisadi, amenunua ndege, amejenga barabara na kadhalika, si lazima tumshukuru. Mnataka nini jamani gunia la chawa au awabebe mgongoni? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ametoa vifaa tiba Wilaya zote na ambulance amejitahidi kama mwanadamu. Elimu bure, jamani kazi alizofanya ni kama miaka 60, mimi naongeza na 30 kama miaka 90, Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye bajeti yetu, napenda kuipongeza bajeti kuu ya Wizara ya Fedha chini ya Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri wake, kwa kweli ni bajeti ya kihistoria iliyoacha simulizi mitaani. Ni bajeti iliyomjali hata mtu wa chini, mnyonge hadi mama lishe hadi mfanyakabiashara ndogo ndogo, wote wameguswa. Nje wenzetu wanafurahia lakini hapa ndani watu wanabisha. Sasa walengwa wamefurahia lakini wewe kwa sababu siyo mlengwa ndiyo maana hata wala huoni umuhimu wake, pole. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama jinsi alivyoweza kufuta road licence, tazama jinsi ilivyoweza kupunguza kodi mbalimbali yaani ili mradi wamefanya walichoweza. Jamani kuna mabadiliko mabwa mwaka huu. Watu wanasema ni mwaka wa neema, ni bajeti ya neema wamefanya kile ambacho walichoweza kufanya, lazima tuwapongeze. Mheshimiwa Dkt. Mpango hongera sana, pongezi nyingi na mama pale, pongezi nyingi na Wizara nzima kwa kazi nzuri na mabadiliko makubwa waliyoyaleta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie jambo moja ambalo ni kodi kwa ajili ya shule binafsi nikisema kwamba mimi pia ni mdau mmojawapo, na- declare interest. Mheshimiwa Waziri Dokta Mpango kodi katika shule binafsi zimezidi. Kuna kodi zaidi ya 25, mpaka unashangaa sisi nasi tunachima madini au nini, wakati sisi tunafundisha watoto wenu. Waangalieni sana kodi ni nyingi hata akikaa na timu yake ingetakiwa wafute kodi zote katika shule kwa sababu shule ni huduma siyo biashara na huduma tunazofanya ni kwa faida ya Taifa zima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa walikuwa wanakwenda Kenya, Uganda na nchi nyingine za jirani lakini sisi tumefanya hawa watoto wasome Tanzania, waweze kujifunza historia yao, wajifunze jiografia yao, wajue viongozi wao, lakini zamani walivyokuwa wanakwenda nchi jirani utakuta akiulizwa wewe Rais wako nani, inabidi aseme Uhuru Kenyatta. Kwa sababu akisema mimi Rais wangu Dokta John Pombe Magufuli atakoseshwa, japo yeye ni Mtanzania yuko nchi ya kigeni, lakini sisi tumeleta fikra za watoto kubadilika kwa kusoma wakiwa wadogo ndani ya nchi baadaye wakiwa wakubwa ndiyo waende siyo mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi mtusaidie yaani jamani tunachajiwa hata majengo, tunaambiwa property tax, hasa yale majengo si ya shule, si watoto wenu ndiyo wanasoma? Mbona shule za Serikali hawatozi kwa nini sisi tu ndiyo mtutoze? Unaambiwa hata vile viwanja tumejenga shule wanakuambia bwana lazima ulipe kodi kama vile kiwanja cha biashara yaani kama kiwanja umefanyia biashara kubwa fulani. Hakika wakitusaidia katika hilo itakuwa ni unafuu kwa ajili yetu na hata kwa ajili ya watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakiangalia wenyewe ile karo tunayotoa ni ndogo mno. Watoto hawa wanakunywa chai asubuhi, saa nne wanakunywa tena na wenzao wa day scholars, mchana wanakula chakula, jioni wale boarders wanakula mlo kamili, sasa hivi vyakula vyote ni gharama. Vilevile wanapewa magodoro na vitanda, wana matron na patron wanaowalinda, kuna daktari na manesi wanaowatunza watoto wetu ili wakae vizuri. Waangalie watuhurumie, watusaidie tufanye kazi pamoja kwa sababu hapa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja mia kwa mia.