Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bumbuli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MAZINGIRA NA MUUNGANO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru tena, lakini pia naishukuru Kamati kwa maoni mazuri waliyoyatoa na ushauri tutauzingatia wote. Pia napenda kumshukuru Mheshimiwa Ally Saleh Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwenye masuala ya Mazingira na Muungano. Bahati nzuri yeye ni mwanamazingira mzuri, ametoa mawazo mazuri na tutayazingatia hasa la kushirikisha wadau zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika,ia suala la baadhi ya vipengele ambavyo vimezungumzwa kwa ujumla na hakuna ufafanuzi kuhusu utekelezaji wake. Nataka nimweleze tu kwamba majadiliano bado yanaendelea kuhusu namna ya utekelezaji wa makubaliano haya. Kwa hiyo, mambo mengine aliyoyazungumza yatapatiwa majawabu na ufumbuzi mara pale mazungumzo kuhusu utekelezaji wa mkataba huu yatakapokwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kujibu karibu mambo yote yaliyozungumzwa na kwa kwa ufasaha kabisa na kwa kweli zaidi ya hapa nampongeza, mwanzo nilisahau kumshukuru kwa mchango wake na kazi nzuri anayoifanya katika ofisi yetu ili kusaidiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Lubeleje amezungumza kwa hisia sana kuhusu masuala haya na namshukuru. Wakati mwingine utu uzima unasaidia kuonesha tofauti. Asilimia 50 ya Watanzania ni watu wa umri wa chini ya miaka 18. Asilimia 44 ya Watanzania ni watoto chini ya miaka 14. Kwa hiyo, unapokuwa na Taifa la watu wengi ni wenye umri mdogo, wanakuwa hawajapata kuona nchi ilikuwaje miaka iliyopita na ilivyo sasa. Kwa hiyo, wanaona huu uharibifu uliopo na hali iliyopo sasa ndivyo nchi ilivyo, kwa hiyo, wanakosa uchungu na hamasa ya hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mzee Lubeleje, amekula chumvi nyingi na anaposema hasa kwamba miaka ya 1960 nchi hii haikuwa hivi, ni kweli, ana ushuhuda kwa sababu ameona ilivyokuwa huko. Kwa kweli tungependa yeye na wazee kama yeye wapate nafasi hizi za kutuelimisha sisi vijana, tuone kwamba uoto wa asili na landscape ya nchi yetu, kwa kweli inaharibika kwa haraka sana katika miongo hii kadhaa aliyoishi, ambayo vijana wengi wa sasa wataishi, hali itakuwa mbaya zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamshukuru sana kwa ushuhuda wake. Kama nilivyomwelekeza Naibu Waziri, atakwenda Jimboni kwake. Kwa kweli hali ni mbaya, ndiyo maana tumepeleka huu mradi mmoja Jimboni kwake kwa ajili ya kusaidia watu wa Mpwapwa. Nafahamu kuna habari ya makorongo mengi yanayopitisha maji na kuharibu mazingira na Naibu Waziri atakuja kuyaona.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Salum, amezungumza kwa hisia sana na kwa kweli ametufundisha na kutueleza jinsi gani baianuai inavyopotea. Kwenye kisiwa kama cha Zanzibar ambapo eneo ni dogo na utajiri wa Zanzibar; utajiri wa Tanzania kwa kweli haupo chini ya ardhi peke yake kwa maana ya madini. Utajiri ni kwenye maarifa ya Watanzania lakini pia ni kwenye uoto na mimea na wanyama ambavyo Mungu ametujaalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya nchi hapa duniani zina aina chache sana za mimea, aina chache sana ya wanyama, ndiyo maana wanakuja huku na dunia inavyoenda kuna baadhi ya nchi hata sauti ya ndege watoto wanaozaliwa miaka inayokuja watakuwa hawaijui mpaka waje kwetu. Sasa na sisi tukipoteza ndege wale, ina maana vizazi vijavyo tutakuwa tunahadithiana kwamba, bwana kuna ndege fulani aliishi miaka hiyo alikuwa na rangi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utajiri mkubwa kabisa wa nchi yetu ni baianuai (bio-diversity); wingi wa mimea na wanyama. Sasa huu mkataba tunaouzungumza leo, makubaliano haya yapo chini ya makubaliano ya UNFCC United Nations Convention of Climate Change na siku ile yale makubaliano yalivyowekwa sahihi kule Brazil kulikuwa na mkataba mwingine unaitwa Mkataba wa Uhifadhi wa Baianuai (Convention on Biological Diversity) ambao sisi ni wanachama wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ule mkataba unatoa fursa nyingi za kuhifadhi baianuai. Pia unatoa nafasi ya nchi yetu kutajirika na kunufaika na baianuai yetu tuliyonayo. Baianuai siyo kwa maana tu ya kuja kuitazama, lakini kuitumia kwenye tiba, utafiti na kadhalika. Mnafahamu madawa yote yanatokana na miti; na mnapoharibu miti na mimea mnapunguza uwezo wa kujitibia siku zijazo. Kwa hiyo, uharibifu wa mazingira ndugu zangu unahusu pia hata tiba yetu kwa miaka inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashukuru kwamba hilo tumelizungumza na sisi kama Serikali, tunaendelea na utekelezaji wa mikataba yote hii miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana Mheshimiwa Mbunge amezungumza kwamba tubadilike. Leo tunazungumza mabadiliko ya tabianchi lakini inawezekana cha kwanza kinapaswa kuwepo ni mabadiliko ya tabiamtu ili tuweze kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Kwa sababu kama mabadiliko ya tabiamtu hayatokei, itakuwa ni vigumu sana kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumezungumzwa pia kuhusu kuni na mkaa na Mheshimiwa Mbogo vile vile amezungumza kuhusu kuni na mkaa. Nataka nizungumze kwamba sisi tunaangalia matumizi ya nishati hizi za tungomotaka wanaita (biomass) katika suala zima la deforestation na landscape degradation, kwamba huu uoto unaouona, ardhi, mimea; hii landscape ya nchi yetu inayopendeza, kasi yake ya kuharibika ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo, ufugaji, utalii maji, zote zina uhusiano na hifadhi ya mazingira. Kwa hiyo, tunapopata uharibifu wa landscape, huu uoto, hizi sekta nyingine zote haziwezi kufanikiwa. Kwa hiyo, uchumi wa nchi yetu na ukuaji wa uchumi na umaskini na ustawi wa watu, unafungama moja kwa moja na hifadhi ya mazingira. Huwezi kutofautisha!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunasema hapa, tunataka kuhamasisha Wabunge wote wawe wanamazingira. Kama unataka kuzungumza maji Jimboni kwako, huwezi kuyapata bila hifadhi ya vyanzo vya maji, bila hifadhi ya miti na kadhalika. Kwa hiyo, nafurahi kwamba waliochangia karibu wote wamesaidia kutoa elimu na wamesaidia kuonesha hisia katika mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye matumizi ya kuni na mkaa, sisi kama Serikali tunashirikiana na tutashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kwamba tunatengezea mpango mkubwa wa Kitaifa wa matumizi ya nishati. Tayari maelekezo yametolewa kwenye Wizara ya Nishati na Madini kutunga sera mpya ya nishati ya tungomotaka (biomass policy) ili tuwe na mwongozo wa namna gani tunapata nishati ya kupikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi kinachotokea ni kwamba miti iko vijijini lakini ukataji wake unanufaisha watu wa mijini. Watu wa mjini hawana miti, lakini watu wa vijijini kuni zile wanakata matawi tu. Ili mtu wa mjini apate mkaa, ni lazima akate mti wenyewe, gogo lile. Sisi kwenye shule, Magereza na Mahospitali, hatutumii kuni za matawi tu, ni lazima tukate mti wenyewe. Ukienda unakuta lundo la magogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tumetumia kifungu cha 13 cha Sheria yetu ya Mazingira ambacho kinasema kwamba Waziri mwenye dhamana ya mazingira ana uwezo wa kuelekeza mamlaka zozote za kisekta, binafsi na taasisi kufanya mambo ambayo yatahifadhi mazingira. Kwa hiyo, tumetoa maelekezo kwa shule, Magereza, hospitali na tumewapa mwaka mmoja kwamba waondokane na matumizi ya kuni na mkaa na tumeanza hapo UDOM.
Mheshimiwa Naibu Spika, UDOM pale pana wanafunzi takriban 30,000, wanapikiwa chakula mara tatu kwa siku. Sasa hebu fikiria kulisha watu 30,000 mara tatu kwa siku, kiwango cha kuni kinachotumika ni kikubwa sana. Ukienda pale utataka kutoa machozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale tumewaambia ndiyo watakuwa wa kwanza na bahati nzuri tumekubaliana kwamba watu wanaowapa zabuni pale, wote sasa ili upate zabuni ya kupika chakula, hauwezi kupata kama unatumia mkaa au kuni. Kwa hiyo, tutaona mabadiliko yaliyotokea pale UDOM yatatusaidia kutoa mfano kwenye taasisi hizi kubwa zenye watu wengi kuhusu kuondokana na hili suala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni jambo ni kubwa, sisi kama Serikali tunalichukulia kwa uzito wake. Matumizi ya nishati nchini yanafungamana na umaskini kwamba masikini zaidi ndio wanagharamia nishati zaidi. Pia tusisahau kwamba wewe unatoka Pemba; ukitazama mkaa unaopelekwa Pemba kutoka bara, haulingani na idadi ya watu walioko Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kule kwenye hizi bandari za kwetu; Mbweni, Bagamoyo utaona magunia ya mkaa yanaenda Pemba. Unajua yanaenda wapi? Hayaendi Pemba, yakifika Pemba yanaenda shimoni, Mombasa. Yakifika Mombasa yanapakiwa vizuri yanaenda Somalia au Uarabuni kuchoma kondoo vizuri. Maana wale wanataka kuchoma kondoo na mkaa mzuri; na yakienda Somalia yanasaidia ku-finance Al-shabaab.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkaa wetu tunaweza tukauona hapa ni jambo la kawaida lakini una muunganiko na value chain kubwa sana ambapo wote kama Serikali na Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ndiyo inahusika moja kwa moja na haya mambo, inabidi tukae tupange vizuri. Kwa sababu siyo tu kwamba mkaa unaokatwa nchini unatumika nchini, unaenda nje ya Tanzania vile vile. Kwa hiyo, tunakata miti yetu sisi kwa manufaa ya watu wengine huko nje ya Tanzania. Kwa hiyo ni suala la kulizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia matumizi bora ya ardhi. Moja ya changamoto kubwa inayosababisha sisi tushindwe kuhimili mabadiliko ya tabianchi ni kwamba tuna kilimo hiki cha kuhamahama. Mtu anavamia msitu, analima mtama misimu miwili, ardhi ikiharibika anakata tena kipande kingine cha msitu. Kwa hiyo, baada ya miaka michache unakuta msitu wote umefyekwa. Au wale wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi kama nchi, wajibu wetu ni kuweka taratibu za kutumia vizuri ardhi. Kielelezo na shabaha ya maendeleo ni kutumia ardhi kidogo kuvuna zaidi. Nitatoa mfano, nchi ya Uholanzi, eneo lake ni dogo kuliko Mkoa wa Katavi, yaani Mkoa wa Katavi ni mkubwa kuliko Uholanzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Uholanzi ni nchi ya pili duniani kwa kuuza bidhaa za kilimo pamoja na kuwa na eneo dogo. Ukiondoa Marekani, inakuja Uholanzi. Uholanzi wanauza dola bilioni 90 za mazao ya kilimo kwenye eneo kama la Mkoa wa Katavi. Kwa hiyo, ndiyo kielelezo cha maendeleo. Nasi tunaweza kufika huko. Wanafanya hivyo bila kutumia GMO wala nini, ni kilimo tu endelevu na wanahifadhi mazingira na ni kuzuri. Kwa hiyo, naamini maendeleo yetu yatafikiwa tutakapokuwa tumefanya mambo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbogo nashukuru sana kwa mchango, nimekupata. Tutashirikiana na Serikali za Mitaa na tumezungumza na wenzetu wa Wizara ya Fedha, Naibu Waziri yupo ananisikia, tumependekeza kwamba kila Wizara na kila Halmashauri iwe na budget code yaani zile…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, naomba urudi ukae kidogo.....
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutoa pendekezo kwamba, saa yetu ile pale mbele itengenezwe. Kumbe inakuwa sahihi mara mbili kwa siku. Naona imesimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasema kwamba, kuhusu mapendekezo ya Mheshimiwa Mbogo kuhusu ushirikishwaji wa Halmashauri na viongozi kwenye maeneo yetu ya vijiji, Wilaya na Halmashauri tutayachukua, tumeyazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mipango yetu katika Ofisi yetu ya Makamu wa Rais ni kufanya kazi kwa karibu zaidi na Serikali za Mitaa. Katibu Mkuu anayo maelekezo yetu kuandaa mikutano baina ya ofisi yetu na Serikali za Mitaa kwenye level ya Mawaziri, Makatibu Wakuu, lakini pia kujaribu kutumia fursa za vikao mbalimbali vilivyopo ikiwemo vikao vya RCC ili kuweza kwenda kutoa elimu kwao, lakini kuweka makubaliano ya ushirikiano ikiwemo ushirikiano katika kuhakikisha kwamba Sheria ya Mazingira inazingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata baadhi ya masuala ikiwemo ya usimamizi wa sheria, ikiwemo ya kufanya hizi habari za tathmini ya athari kwa mazingira, baadhi ya mambo tunafikiria kuyakasimu kwenye Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, mpango huo upo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kabla sijakaa, itapendeza kama tutakubaliana ndani ya Serikali kuwa na budget code, ili kila Halmashauri katika bajeti yake iwe na sehemu inasoma namba zile, “Hifadhi ya Mazingira,” ili fedha ziweze kupangwa kwa ajili ya hawa Wakuu wa Wilaya, kama ulivyosema, wapate OC ya kuzunguka na kusaidia kwenye hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupanda miti, Naibu Waziri amelizungumza kwamba tutalipa msukumo mpya na tutafanya sensa ya miti. Pia, niseme tu kwamba, kama tulivyozungumza kwenye Azimio kwamba pale Morogoro tumeanzisha kituo kinaitwa National Carbon Monitoring Centre ambapo kuna teknolojia ya kujua kasi ya uharibifu wa mazingira maeneo ambayo miti inahitaji kurejeshwa. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Maliasili ni mhusika pia kuhusu masuala ya misitu, kwa hiyo, tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba tunafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi kuhusu misitu, siyo kupanda miti mipya, ni kutokata iliyopo. Katika miti yote iliyopo Tanzania, 95% ni ile iliyokuwepo, 5% tu ndiyo iliyopandwa. Kwa hiyo, ili ufanikiwe zaidi kwenye hili jambo, usikate miti, bali uhifadhi ile ambayo haijakatwa na hiyo itatusaidia tutakapowezesha watu kutotegemea miti zaidi katika maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Kamala kwa hoja nzuri alizoziwasilisha za sababu ya kuunga mkono. Tunakushukuru na tunakubali kwamba sisi kuridhia haya makubaliano kutatusaidia kuweza kupata fursa. Zaidi tunafurahi kwamba yeye kama Mbunge, anaona haja ya Serikali kuwa na rasilimali nyingi zaidi na Bunge mna wajibu pia wa kupanga fedha kwa ajili ya hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa fedha kwa ajili ya hifadhi ya mazingira haziko kwenye bajeti peke yake, ziko namna nyingi ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Mazingira ambapo kwenye sheria ile unategemea moja ya vyanzo vilivyoandikwa vya Mfuko, nacho ni subvention appropriation kutoka kwenye Bunge, ukiondoa kwenye bajeti. Kwa hiyo, Bunge lina uwezo wa kuamua lenyewe kwamba licha tu ya bajeti ya Serikali kwa Ofisi ya Makamu wa Rais, pia tunaweza kabisa kupangia Mfuko wa Mazingira kiasi fulani cha fedha na Mfuko huu utakapopata fedha hizo, basi utatuwezesha kufanya kazi zetu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nadhani nimeweza kuzungumza yote yaliyozungumzwa, lakini niseme tu kwamba, ushauri uliotolewa tutauzingatia. Tunaomba sasa utusaidie namna ya kwenda kwamba, tunatoa hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naomba kutoa hoja.