Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitamke kwamba kwa vile leo ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuchangia katika Bunge hili, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kwa kishindo mwaka 2015, lakini nimpongeze vilevile kwa kutufanyia kazi kubwa ya kutupatia Baraza la Mawaziri zuri sana. Tunaona kazi wanayoifanya na kila mtu anaiamini. Na mimi naomba nichukue fursa hii kuwaambia Mawaziri wachape kazi, tuko nyuma yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nitamke vile vile kwamba kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuchangia, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Chilonwa, ambao waliona waniamini na mimi niwawakilishe katika mjengo huu katika kuleta matatizo yao na kushirikiana kutatua matatizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu kwa hotuba yake nzuri ambayo ametupa asubuhi hii kupitia kitabu hiki ambapo amejikita vizuri katika masuala ya kilimo na nyanja zake zote. Amegusia kila eneo na namna gani Wizara yake inajipanga, kufanya kwa ajili ya Watanzania; lakini pia katika nyanja za mifugo, pamoja na sekta zote. Ameeleza kwa umakini kabisa, ni nini Serikali inataka kutufanyia sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo amekwenda kwenye suala la uvuvi na sekta zake zote, masuala ya kupanga siku zote yana changamoto, na sisi tuko hapa leo kuijadili hii hotuba yake kwa lengo la kuonesha changamoto zilizopo tukitegemea kabisa kwamba watazichukua na kuzifanyia kazi na kuboresha yale ambayo wanakusudia kuyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii sasa nijielekeze kwenye Jimbo langu la Chilonwa. Jimbo la Chilonwa tunalima sana, lakini huwa tuna matatizo ya hapa na pale ya mvua. Jimbo la Chilonwa tunafuga kwa kiasi chake, tatizo hatuna uvuvi kwetu. Nikizungumzia suala la kilimo, naomba sana kwa upande wa pembejeo ambapo imeonesha dhahiri kwamba safari hii pembejeo zitapatikana kwa wakati na pembejeo zinazostahili. Isiwe kwamba tunaletewa mbegu ambazo unapanda hazioti tena, isiwe kwamba tunaletewa mbegu wakati wa kupanda umepita. Tunaamini haya yaliyozungumzwa hapa ndani ndiyo yatakavyotekelezwa na sisi tunaomba iwe hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kilimo ni biashara. Pale inapokuwa mwananchi analima halafu anakosa sehemu ya kupeleka mazao yake, au analima inakuwa ngumu sana kwake kusafirisha mazao yake kuyapekeka kunakostahili, linakuwa tatizo kubwa sana. Tatizo la miundombinu kuingia vijijini hebu lifanyiwe kazi. Najua Serikali inajipanga, lakini naomba nisisitize kabisa, lifanyiwe kazi na hasa katika Jimbo langu la Chilonwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanalima sana mahindi na kwa taarifa yako, najua Wabunge wengi tunajua humu, mahindi ya Dodoma yana soko kubwa sana duniani. Mahindi ya Dodoma hayatumii kemikali. Dodoma hatutumii mbolea za chumvi chumvi hata siku moja! Dodoma tunahitaji mvua tu! Tatizo letu ni mvua, ndiyo inayotusumbua. Kwa hayo, mazao kidogo tunayopata, yana soko kubwa sana. (Makofi)
Kwa hiyo, naiomba sana Serikali itusaidie kutuwezesha mazao yetu yafike sehemu yanapotakiwa kwenda kiurahisi. Inapokuwa ngumu kuyafikisha mazao sokoni, wanunuzi, walanguzi au wafanyabiashara, wanakuwa na sababu ya kununua mahindi kwa bei ya chini sana. Kama atasafiri kwenda vijijini kwa shida sana, njia haipitiki, anachukua siku tatu kufika sehemu ambayo angetumia masaa mawili, matatu, kwa vyovyote vile atataka kwamba atakapokuja kwenye soko, mahindi yake yawe competitive. Kwa hiyo, atataka anunue mahindi kwa bei ya chini na kwa kufanya hivi, mwananchi anaathirika sana kiuchumi. Kwa hiyo, naomba sana suala la miundombinu, barabara za kuelekea vijijini liangaliwe kwa macho mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mtu aweze kulima lazima kuwe na amani. Nasema wazi, katika Jimbo langu la Chilonwa, vilevile kuna tatizo la migogoro ya ardhi ambayo naweza kuisema vile ni migogoro ya mipaka. Ardhi kwa maana ya wakulima na wafugaji wanavutana. Mipaka inafika wakati fulani Wilaya moja na nyingine kama alivyozungumza ndugu yangu hapa Mheshimiwa Nkamia, tunavutana sana mipaka ya kulima na hasa unapofika wakati wa kulima na Wilaya tunazopakana nazo, ingawa tatizo kubwa kwa kweli ni wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba sana Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia wafugaji maeneo maalum kwa ajili ya malisho, lakini katika maeneo hayo njia rahisi ya kuwafanya waende kwenye maeneo hayo ya malisho ni kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanakuwa na majosho na maji ya kutosha kuwapatia mifugo yao ili waweze kwenda na kufuga huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mazao ya biashara. Bahati mbaya Dodoma mazao ya biashara siyo mengi, lakini tuna alizeti na vilevile tuna zabibu. Namuombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, zao la zabibu ambalo umetuheshimu, limeonekana katika kitabu chako, huku nyuma naona zao la zabibu, hili zao ni mkombozi mkubwa sana wa mwananchi wa Dodoma, lakini tunahangaika nalo kupita kiasi kwa sababu ya soko. Watu wanakuja wananunua kwa bei wanazotaka, wanakwenda kuuza bei kubwa. Mtu akija shambani atanunua kilo moja shilingi 500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako, kilo moja inaweza kuwa na mikungu hata mitano ya zabibu. Ukija mjini hapa mkungu mmoja wewe unanunua shilingi 1,000, yeye ananunua shilingi 500 anakuja kuuza hapa mjini shilingi 5,000. Huyu mwananchi atainuka lini? Dawa peke yake ni kuhakikisha tunamwekea kiwanda cha uhakika cha zabibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu kwa Serikali, iangalie namna ya kuisukuma Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, ina mpango wa kuweka kiwanda, lakini inasuasua sana. Naombe kabisa, ndugu yangu Mheshimiwa Waziri chukua fursa hii, wasiliana na Halmashauri ile ujue shida yao ni nini? Tumefika mara nyingi, tunaambiwa kiwanda kinafuata muda siyo mrefu, lakini kila siku, sasa tuna zaidi ya miaka miwili, kiwanda hakionekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, naomba nichukue nafasi hii kutamka kwamba naiunga mkono hoja. Ahsante sana.