Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nakushukuru. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema nami kuchangia katika hoja iliyopo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunahitaji amani na amani haichezewi. Watu wanajaribu kuangalia ubinafsi bila kuiangalia nchi inakwenda wapi. Popote panapotokea vita wahanga ni wanawake na watoto. Leo wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta. Tumeiona Libya sasa hivi wanawake na watoto wanahangaika. Tumeiona Iraq, wanawake na watoto wanahangaika, tunaiona Somalia, wanawake na watoto wanahangaika, tumeiona Rwanda, wanawake na watoto walihangaika, wanakuja mpaka Tanzania kama wakimbizi na Burundi hivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo chokochoko ndogo ndogo zinazoanza ziwe za kidini, ziwe za kisiasa. Wachungaji, Maaskofu na Mashehe watangaze dini. Nia ya kupewa nafasi hiyo kutangaza uadilifu, kuitangaza amani kwa wananchi wao. Wakianza Maaskofu, Mashehe kujiingiza katika siasa, siasa ni propaganda. Sasa wanataka kutangaza mchezo wa propaganda waingize katika dini, haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Serikali isimamie kikamilifu. Kwa mfano, mimi hapa mlemavu, ikianza vita mtakimbia humu nyote, mtaniacha mimi niko humu ndani. Hivyo mhanga namba moja ni mlemavu. Wagonjwa waliokuwa mahospitalini watakuwa wahanga wa vita. Wazee watakuwa wahanga wa vita. Watanzania hatutaki vita. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, kama wana hoja, iletwe hoja patafutwe ufumbuzi na usuluhishi. Kutumia majukwaa ya dini kutangaza mazungumzo ambayo yatawafanya vijana wapate mihemko, waingie mtaani wafe wao wakimbie, haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kuna clip ya mtoto amekimbia Syria, ameokotwa na UN ameshika nguo ya mama yake na dada yake, anasema nakwenda kumshtakia Mungu, mama yangu anauawa namwona hivi hivi, baba amekimbia. Wanaume hawana uvumilivu na watoto. Pakianza vita, wanaume wote wanakimbia wanaacha akinamama wanahangaika hapa. Wanawake Tanzania nzima, tuungane tupinge hii kitu. Tutakaoathirika ni wanawake. Haikubaliki na wala haitakubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunashiba kwa vile pana amani hapa. Tunataka maji hapa kwa vile pana amani. Mnataka barabara kwa vile pana amani hapa. Bila amani hakuna maji wala barabara. Bodyguard anamkimbia Rais, bodyguard anamkimbia Waziri Mkuu, kila mmoja anatafuta taharuki, anakimbia anakwenda anakokwenda kwake. Tusilichukue kama ni kitu cha mzaha, ni kitu hatari. Watanzania nimewaangalia leo nilikuwa nasikiliza hotuba ya Mheshimiwa Rais Nyerere akisema hivi: “Kuna watu wanaangalia maslahi ya mabepari na kuna watu wanaangalia haki za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hao wanaoangalia haki za mabepari waangaliwe kwa macho mawili ili wasituingize katika mgogoro.” Hata hiyo amani isimamiwe kwa ukamilifu. Kama kuna wanaovunja amani upande huu na upande wa pili vile vile ushughulikiwe. Msumeno unakata mbele na nyuma, haukati sehemu moja. Italeta furaha na faraja kuona wale wanaotaka kuleta uharibifu wa amani nchi hii wanashughulikiwa bila kuangalia anatoka wapi? Anaelekea wapi? Amani ni amani tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie miradi na mikopo ya Tanzania. Kwa muda mrefu Tanzania ina madeni makubwa, tena madeni makubwa sana lakini madeni haya yalisababishwa na mikataba ambayo haikufanyiwa analysis. Nitatoa mfano, anakuja World Bank, anatoa mradi wa Selous, ule mkopo nitalipa kwa miaka 25, lakini anakupa condition ambayo badala ya kusema utafaidika, anafaidika yeye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuja kututawala, sasa hivi wanatutawala kwa kupitia mikopo. Mkopo wa shilingi bilioni 500 anakwambia utalipa kwa miaka 25. Kila mwaka kwa maana hiyo nitalipa shilingi bilioni 20. Shilingi bilioni 20 nikichukua mwakani riba inarudi pale pale mpaka miaka 100 mkopo huo hauishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile wao wanacheza na akili yetu bila kuangalia sisi wenyewe kama hicho wanachokifanya kina usahihi gani katika kufanya analysis? Analeta mkopo wa shilingi bilioni 500, anaweka na conditions za pembeni. Watakuja kufanya kazi ma-expatriate wetu, watalala katika nyumba kubwa, wanataka wafanyakazi wanne, mshahara wake kwa mwezi dola 20,000; kila mwisho wa mwezi atakwenda Mikumi au Serengeti. Ile mikataba ya pembeni ukiisoma inatia kinyaa kabisa. Haiifanyi nchi hii kama itaweza kukwamuka kwa kupitia hii mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jiulize, ilijengwa reli ya kati, kutoka Kigoma mpaka Dar es Salaam kwa kodi za vichwa za Watanganyika wakati ule. Kila Mtanganyika aliambiwa atoe kodi; na waliijenga reli kwa hela zetu kutoka Kigoma mpaka Dar es Salaam. Matokeo yake ilikuwa ni wao kuja kuchukua madini, wao kuchukua pembe na wamefaidika wamekuwa matajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutajirika, wamekuja na system ya pili ya mikopo. Naomba, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mwenye dhamana na Mawaziri, waiangalie mikopo kwa umakini sana. Nina imani kuwa hii kazi ndugu yangu anaiweza. Awaokoe Watanzania ambao wanaangamia na mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkopo wa Selous, umeletwa mkopo maeneo ya Udzungwa, Mikumi na Ruaha, zote ziko chini ya TANAPA. Wanataka kujenga viwanja vya ndege, barabara kutoka Lindi kwenda Liwale hakuna. Kwa nini wasituambie tunataka mkopo huu ukajenge barabara ya Liwale ili watalii waende Liwale? Kwa nini wasijenge barabara ya kwenda Namtumbo ili watu waende Namtumbo? Wanatupa conditions ambazo zinatufanya tunakwazika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mradi huu utapita, najua kweli hii Serikali siyo sikivu na nitaufuatilia. Kama Serikali ni sikivu, mkopo wa World Bank unaokwenda Selous ufanyiwe kazi ili mwananchi wa mikoa mitano hii ikiwemo Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambayo tumeiacha kwa muda mrefu kwa miradi mikubwa, kwa kweli sitakubaliana nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mradi wa SAGCOT. SAGCOT ni Sothern Agriculture Corridor of Tanzania. Lindi, Mtwara na Ruvuma tuliachwa. Hii ni mikakati ya makusudi ya kutufanya Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma tuendelee kuwa maskini. Sasa wamelala waliolala, sisi bado tuko macho. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu ameturudisha tena kuja kuangalia haya, je, wataendelea kutukandamiza Mikoa ya Kusini? Kama unataka kuleta msaada wa utalii kusini, unaiachaje Kilwa, wakati Kilwa katika heritage ilikuwa namba 21? Naomba mradi huu wa World Bank utushirikishe Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa kikamilifu ili tuwe beneficiary kwa mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia barabara. Hata Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi katika kutembelea mikoa yote; Mikoa ambayo iko nyuma ni Lindi, Mtwara na Ruvuma katika barabara. Sasa uwiano wa maendeleo, kuna wengine wanapaishwa kwa maendeleo, wengine wanawekwa nyuma, haikubaliki. Watanzania ni Watanzania wote tunahitaji kula hii keki. Leo Mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma tuna produce korosho ya kutosha; uchumi wa nchi uko juu; leo umwambie mtu twende Liwale, hawezi kufika. Mwambie mtu aende Milola sasa hivi hafiki. Hakuna barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba bajeti itakayokuja ya Wizara ya Ujenzi iangalie mikoa ambayo imeachwa kwa muda mrefu ipewe priority. Hii itatufanya na sisi tufarijike kujiona na sisi tuko ndani ya keki ya Watanzania. Tunawaona wenzetu Kaskazini wanavyosaidiwa huko, nasi tunataka Kusini iende sambamba na mikoa mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, nimekuja kuzungumza hayo machache kuitangaza amani, amani hii itatusaidia katika kilimo, afya na elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana.