Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya hasa katika suala zima la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kusimamia suala zima la kilimo hususan pamba, tumbaku na kahawa, lakini kazungumzia pamba. Mheshimiwa Waziri Mkuu kutoka kwenye 120,000 kwa miaka mitatu mfululizo ya nyuma, tumevuka sasa hivi tunatarajia kuvuna 600,000, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali hususan katika suala zima la pembejeo, katika mikakati hii mikubwa tunayoifanya, basi ni vema iende sambamba na pembejeo ili kusudi mazao haya yasiendelee kuathirika kwa kukosa pembejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Waziri Mkuu, mazao haya mengi tumeyapata, lakini wale tunaokaa kandokando na uhifadhi, tunalo janga la tembo. Tembo wamekuwa wakivamia sana katika maeneo hayo na kusababisha maafa makubwa katika jamii. Basi nalo hilo katika suala zima la ulinzi iwe sehemu ya kipaumbele, hususan maeneo ya Itilima, maeneo ya Nyasosi na maeneo ya Mwalali na Nkuyu na Longalombogo, basi viwekwe vituo ili tembo hawa wasiendelee kuja kuharibu mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu kwa vijana, Mheshimiwa Waziri Mkuu Wizara yake inayo dhamana ya elimu. Naomba na kuishauri Serikali, hususan katika vijiji vipya na mikoa mipya na Wilaya mpya zilizoanzishwa, kumekuwa na changamoto ya kutokuwa na shule katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakijenga madarasa, lakini katika Sheria ya Elimu wanasema lazima tuwe na madarasa sita. Sasa mimi kama mwakilishi wa wananchi, wananchi wananiuliza, hivi tutaanzaje kuwa na majengo sita wakati kuna darasa la kwanza litapita, la pili mpaka la tatu na la nne? Kwa nini tusiwe na manne halafu tuendelee na mwendelezo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, vijana wengi wako kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, ni vyema Wizara ya Elimu ikashauriwa kuwa na mipango ambayo siyo ya kubana sana ili watoto wetu waweze kupata elimu kama tunavyotarajia katika Awamu hii ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Mkoa wetu wa Simiyu. Aliahidi katika Wilaya yangu ya Itilima, nilikuwa sina jengo la utawala, lakini leo ukiingia Itilima mambo yanakwenda vizuri, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la kuanzisha Wakala wa Barabara (TARURA), mimi nishauri katika sehemu ya TARURA, ni vyema hawa TARURA sasa waweze kushiriki katika vikao vya Halmashauri kusudi wapate mawazo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao. Tutakapofanya hivyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu tutakuwa na uboreshaji mkubwa na ufanisi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao. Siyo kama inavyofanya sasa, inafanya yenyewe, wananchi hawajui kinachoendelea katika maeneo husika, lakini katika suala zima, kazi inakwenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la juzi alilokuwa anazungumzia kuhusu la wanunuzi wa pamba hususan katika kuanzisha Vyama vya Ushirika. Vyama vya Ushirika mwendelee kuviimarisha ili kusudi wanunuzi hao wasije wakapoteza fedha zao pindi msimu utakapofika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la vijana kuhusu mkopo. Nimeingia Bungeni leo ni mwaka wa tatu. Nimekuwa nikisikiliza humu ndani Waheshimiwa Wabunge tukizungumzia habari ya asilimia 10. Naiomba Wizara itengeneze mfumo wa fedha hizi kuwa na kapu moja ili vijana katika Halmashauri zetu nchi nzima wawe wanakopa kwa pamoja na kurudishwa ili hizi fedha ziwe na mzunguko katika maeneo mbalimbali ya vijana na generation ya vijana wanaokuja. Siyo hivi inavyokwenda, fedha hizi zinakuwa nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita, nilikuwa napitia katika Mkoa wa Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2017 umekopesha shilingi bilioni 3.9, lakini collection ni shilingi milioni 400. Utaona sasa kizazi kinachokuja huku nyuma, kitakuta fedha hazipo na hizo fedha zitapotea, lakini tukizisimamia vizuri nina imani kwa usimamizi wenu mahiri Mheshimiwa Waziri Mkuu, akilisimamia hili nina imani fedha zile zitasaidia kizazi kijacho na katika mfumo mzima wa uchumi wa viwanda, vijana wetu wanaweza wakajiajiri na wakafanya kazi kubwa sana katika maeneo yetu husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala zima la afya. Naiomba Serikali ya Awamu ya Tano, miongoni mwa Wilaya 67 na Itilima imo kwa kupata Hospitali ya Wilaya. Ninazo Zahanati 28 zimejengwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Mheshimiwa Dokta Magufuli na wewe mwenyewe Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba zile Zahanati basi Serikali Kuu wazimalizie kwa maana ya kwamba wananchi wameshajenga mpaka hatua za mwisho, lakini ziko Zahanati tatu ambazo zimeshakamilika. Nyumba ya Mganga na kila kitu. Tunachosubiri tu ni kupeleka Wauguzi na tuna tatizo na suala zima la watumishi. Itilima inahitaji watumishi katika kada ya Afya watumishi 630, tulionao ni 120; lakini tuna wakazi 342,000. Kwa hiyo, utaona adha hii inayowapata wananchi wa Itilima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, alipofanya ziara yake ya kwanza katika Mkoa wetu wa Simiyu mwaka 2016, alipita akaahidi barabara. Leo wakandarasi wako site na wanafanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika ziara yake aliahidi ujenzi wa mabwawa katika Wilaya yangu ya Itilima na kule Mwapalala, sasa bwawa limekamilika na maji yanatoka kwa asilimia mia moja. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya. Kweli anaitendea nchi haki na kiapo alichoapa, kweli Watanzania wote tunaamini kazi anayoifanya ni kubwa na nzuri zaidi. Nchi yetu ilikuwa haina usafiri, leo ina ndege tatu na nyingine zinaendelea kuja. Hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo.

Ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge tuendelee kumuunga mkono Rais wetu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Mwenye macho haambiwi tazama. Naungana na maneno ya Mheshimiwa Azza, amesema 2020 wataisoma. Wataisoma kweli kweli kwa sababu kazi iliyofanywa ni kubwa na inaonekana na Watanzania wote wanaikubali kazi mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mambo mengi ambayo mmeyafanya Serikali ya Awamu ya Tano, lakini kubwa zaidi kuweza kujitegemea sisi wenyewe kuliko kuwa manamba wa kuendelea kukopa katika nchi za nje. Unapokuwa mkopaji hata heshima ya nchi haipo, lakini sasa wameshika adabu yao na ndege juzi ilipoteremka kila mtu nadhani alinyamaza kimya ambaye alikuwa haiombei nchi yetu mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.