Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa ninaombanimshukuru Mungu aliyetupa uzima na uhai tumeweza kufika kwenye Bunge hili ambalo ametupa kibali yeye. Hatukuja kwa uwezo wetu tumekuja kwa uwezo wa Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kuwatumikia Watanzania, tunaona jitihada zake ni nzuri mno kupita kiasi maana yake bajeti hii ni ya kupongeza tu kwa sababu kazi kubwa inafanyika na tunaona jinsi Serikali inavyowatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze sana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu. Vile vile naomba nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kazi kubwa anayoifanya. Tunaiona kazi yake, juzi alikuwa Geita kwenye Mwenge, tumekuona dada yetu mpendwa umefanya kazi nzuri sana. Pia niwapongeze Naibu Mawaziri kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa najua ajira ni shida sana, lakini naiomba Serikali yangu sikivu najua mpaka sasa hivi kweli kuna watendaji ambao walikuwa darasa la saba lakini watendaji hawa wametufanyia kazi kubwa sana Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata wamefanya kazi kubwa wemetujengea shule, wametujengea dispensary na vituo vya afya. Tunaomba watendaji hawa warudishwe kazini wasubiriwe muda ambao wataweza kustaafu ili waweze kupata haki zao. Najua Serikali yangu sikivu mmesikia mnaweza kutenda kitendo hicho ili hawa watu waweze kurudi makazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze tena kwa ndege ambayo imefika tumeona uzinduzi wake. Nasi Mkoa wetu wa Katavi tuna uwanja mkubwa sana wala hatuombi uwanja leo. Sisi tayari tuna uwanja, lakini hauna ndege. Hivyo, tunaomba sasa kwa sababu kuna ndege
nyingine imefika mpya na sisi sasa Serikali mtupangie ratiba ili na sisi wananchi wa Katavi sasa tuweze kufaidi matunda ya Serikali ya Awamu ya Tano, kwa sababu jitihada ni kubwa tunaziona kwa macho na wananchi wa Katavi wana maeneo ambayo watajivunia kwa sababu wana eneo kubwa sana la utalii, tuna Mbuga ya Katavi, sasa watalii wataweza kufika Katavi kwa urahisi kwa sababu uwanja wa ndege tunao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali yangu kwa route zitakazopangwa sasa hivi ya ndege hii mpya, basi na Katavi mtuangalie kwa jicho la huruma ili na sasa na sisi tuweze kupata watalii na Serikali yetu iweze kuingiza mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ndani ya nchi yetu kuna mikoa ambayo tuliongeza Katavi, Njombe, Geita pamoja na Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Mikoa mpaka leo hawajapata makazi, hawajengewa nyumba za kuishi pamoja na Ofisi zao. Kwa mfano, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi Mkuu wa Mkoa mpaka leo anatumia jengo la Halmashauri ya Manispaa. Naomba basi sasa hivi tupange mikakati mizuri tuweze kuwajengea ofisi kwa sababu Mkuu wa Mkoa anahitajika apate ofisi yake ili aweze kufanya kazi vizuri. Vilevile akipata makazi atakaa vizuri sana na akafanya kazi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuangalie Mkoa wa Katavi kwa sababu hana nyumba wala hana ofisi na siyo vizuri hawa watu kuhangaika hangaika, wanatakiwa wapate sehemu ya kukaa mahali pazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mawasiliano, naomba niipongeze sana Serikali kwa jitihada ya kuweka mawasiliano katika maeneo mengi. Mkoa wa Katavi bado kuna maeneo mawasiliano hayajafika kabisa na mazingira yetu Mkoa wa Katavi ni magumu. Ukiangalia kama Kata ya Ilunde. Ilunde jiografia yake ni ngumu sana, vilevile Ilunde kuna biashara nyingi ambazo zinafanyika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu iangalie basi Kata ya Ilunde iipeleke mawasiliano, wakipata Kata ya Ilunde na kuna Kata jirani inaitwa Kata ya Ilela, Kata ya Ilela nayo watapata mawasiliano kwa urahisi. Naomba sana maeneo haya ni maeneo ya biashara wanalima karanga, wanavuna asali, kuna vitu vingi vinavyofanyika maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine ya Utende, kuna maeneo mengine Wilaya ya Tanganyika, maeneo ya Sibwesa, kuna biashara, wanalima mpunga na wanafanya shughuli nyingi za kijamii ambazo zinaingiza mapato ndani ya Serikali yetu. Naomba katika maeneo haya mtandao uweze kufika, kwa sababu mtandao sasa hivi ni maisha, kwa sababu mtandao ukipiga simu biashara kila kitu kinakuja kwa wepesi zaidi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika maeneo ya Ilela pamoja na Ilunde wanatamani sana na wenyewe wapate TBC Radio, hakuna usikivu wa radio yetu ya Serikali. Wanatamani sana waweze kusikia matangazo ya TBC. Naomba sana upande wa radio basi tupate mawasiliano hayo ili nasi tusikie matangazo ya Kitaifa, Kimataifa pamoja na Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niipongeze Mifuko ya jamii PPF, LAPF pamoja na NSSF. Wamekuwa miongoni mwa jamii kwa asilimia kubwa sana. Wanasaidia sana maendeleo ndani ya jamii zetu, vilevile kusaidia jinsi gani wananchi wanavyofanya kazi zao na wenyewe wanawasaidia kupitia maombi ambayo yanafika katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kabisa ni jinsi gani kupitia elimu bure wananchi wengi wamehamasika kupeleka watoto mashuleni. Sasa hivi ndani ya maeneo yetu ndani ya vijiji vyetu na vitongoji vyetu wananchi wengi wamehamasika kujenga majengo, wamehamasika kujenga vitu vingi ambavyo Serikali inaenda kuwahamasisha, unakuta maboma yale yanaishia kwenye lenta.
Mheshimiwa Mwenyekiti,aiomba sana Serikali yetu kupitia Halmashauri zetu yale maboma wananchi walikoyafikisha basi waweze kumaliza kwa sababu watoto wetu wengi sana wanasoma kwenye miti wengine, hatuna vyoo vya kutosha, najua kwa sababu wanafunzi wamekuwa wengi ndani ya madarasa na maeneo yetu, vyoo tulivyovijenga kupitia wananchi vimekuwa havitoshi, basi naomba Serikali yangu sikivu, tuweke mikakati maalum, kwa sababu tumeona jinsi gani sasa hivi Serikali yetu ilivyokumbuka zile shule za Sekondari za zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Elimu. Waziri wa Elimu amesimamia vizuri sana, shule zile kongwe zote zimeboreshwa zimekuwa nzuri sana kusema kweli, lazima tupongeze kwa hili, kwa sababu tumekwenda kwenye shule kongwe tumeona jinsi gani matengenezo yalivyotengezwa, basi tunaomba Serikali kupitia shule za misingi sasa, kwa sababu shule nyingi za misingi zimeharibika mazingira yake siyo rafiki kwa watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri mtoto akikaa kwenye mazingira rafiki atasoma vizuri. Hivyo, naiomba Serikali yangu sasa ichukue jukumu hili, kupitia TAMISEMI tuanze kuboresha shule zetu za msingi pamoja na mazingira yao ya kwenda maeneo nyeti ili watoto wale waweze kusoma vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umeme, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi REA III haijafanyika kabisa kwa sababu Mkandarasi sijui alipelekwa Mahakamani, hakuna kitu chochote kinaweza kufanyika. Sasa wananchi wa Mkoa wa Katavi wanahitaji umeme, maeneo mengi tukipita kwenye Kata zetu hakuna umeme na kuna sehemu zingine ni za biashara, watu wanajishughulisha na mambo mengi, sasa unakuta umeme hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu, sasa hivi katika bajeti hii najua bajeti hiyo imeshapita ya wakati ule REA III, lakini bado tuna nafasi ya kuweka tena mikakati mipya ili Mkoa wa Katavi katika yale maeneo yote REA III haijapita, tunaomba iweze kufanyika kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Katavi kupitia maeneo mengi wanahitaji nao waweze kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jeshi la Polisi. Najua Jeshi la Polisi tunalipenda sana wanatulinda usiku na mchana, basi nao tuwawekee vizuri mazingira yao. Unakuta kwenye kituo cha Kata ukienda kuona nyumba ya Askari wetu ni nyumba ya udongo inasikitisha. Naomba basi tujitahidi kuwawekea mazingira mazuri, wanafanya kazi vizuri tuwawekee mazingira mazuri ili waweze kufanya kazi vizuri na kuendeleza amani ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga Mkono hoja. Nashukuru kwa barabara inayoanzia Tabora – Mpanda, nashukuru sana na Wakandarasi wako site, hongera sana.