Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema na hatimae nimesimama humu ndani kuweza kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan; Mheshimiwa Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa; na Baraza lote la Mawaziri na Watendaji wote wa Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya. Hongereni sana, kazi inaonekana, chapeni kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba nianze na kituo cha Buhangija, Kituo cha Watoto wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali mwaka huu wa fedha wametupa shilingi milioni mia mbili themanini na sita na laki sita ambazo zimeweza kujenga madarasa manne, mabweni mawili na matundu 18 ya vyoo. Tunaishukuru sana Serikali kwa kukiona kituo hiki, lakini kituo hiki bado kina upungufu mwingine ambao unahitaji kukamilishwa na hata mwaka jana nilivyokuwa nachangia nilisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha watoto wenye ulemavu Buhangija kina upungufu wa watumishi. Kina upungufu wa Walimu wa watoto wasiosikia. Kituo hiki mahitaji yake ni Walimu nane lakini kina Walimu wawili tu. Mheshimiwa Jenista hata mwaka jana nilisema naomba akitazame kituo hiki. Walimu wawili tu hawatoshelezi kuwafundisha watoto hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo hiki kina walezi wawili tu wakati mahitaji ni walezi nane. Kituo hiki cha Buhangija hakina Mpishi hata mmoja, wapishi wanaopika pale ni kwa kujitolea na wanalipwa kama vibarua. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kulifanyia kazi pamoja na kuboresha mazingira hayo lakini watumishi hawa waweze kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sekta ya afya; niishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa ambayo imeendelea kufanya katika sekta ya afya. Katika Mkoa wangu wa Shinyanga imeweza kuwezesha ujenzi na uboreshaji wa vituo sita vya afya. Kituo cha Afya cha Iyenze kilichopo Halmashauri ya Mji Kahama, Kituo cha Afya cha Chela kilichopo Halmashauri ya Msalala, Kituo cha Afya cha Ukune kilichopo Halmashauri ya Ushetu na Kituo cha Afya Tinde na Samuye Halmashauri ya Shinyanga Vijijini pamoja na Kituo cha Afya cha Songwa kilichopo Halmashauri ya Kishapu. Tunaishukuru Serikali na tunaipongeza kwa kazi kubwa wana kazi inaonekana, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uboreshaji wa vituo hivi, kuna matatizo mengine ambayo yanastahili wagonjwa hawa kupewa rufaa. Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu haina Hospitali ya Wilaya. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini huu ni mwaka wa nane sasa naiongelea Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini. Tulishaanza ujenzi lakini ujenzi huu umekuwa ukisuasua kwa sababu hatupewi fedha za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu sikivu, nimemsikia asubuhi Mheshimiwa Naibu Waziri akisema kwa mwaka huu wa fedha kuna hospitali za Wilaya 67 ambazo zitakwenda kujengwa. Namwomba na nina hakika kwamba Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Hospitali ya Wilaya ya Ushetu zitakuwepo katika orodha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatendea haki Mkoa wangu wa Shinyanga nisipoongelea Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga unakwenda taratibu na hii ni kwa sababu fedha ambayo inatengwa imekuwa ikitengwa fedha kidogo na hivyo kufanya ujenzi huu usikamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kuna upungufu mkubwa wa watumishi. Mahitaji ya Hospitali ya Mkoa wa shinyanga watumishi ni 474, lakini waliopo ni 285 tu. Kwa takwimu zilizopo watumishi 30 ndani ya miaka miwili hii wanakwenda kustaafu, hivyo niiombe Serikali kuweza kuongeza watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kusema na mwaka jana kwenye bajeti nilisema Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ina uhitaji wa Madaktari Bingwa 21, lakini mpaka hivi ninavyoongea kuna Madaktari Bingwa wanne tu. Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akinamama mmoja, Daktari wa Watoto mmoja, Daktari wa Upasuaji mmoja na hivyo kufanya tatizo la Madaktari Bingwa katika hospitali hii linakuwa ni sugu, niombe hospitali iweze kuletewa Madaktari hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa elimu. Nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali sikivu ya Awamu ya Tano imeweza kufanya mambo makubwa katika Mkoa wa Shinyanga. Nianze na Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ilipata milioni mia moja sabini na kwenda kujenga hosteli ya Sekondari ya Burige na Sekondari ya Ntobo Sekondari, tunaishukuru sana Serikali. Halmashauri ya Ushetu imepeleka fedha katika Shule ya Msingi Nonwe milioni mia moja tisini na mbili na Shule ya Msingi Bugomba milioni mia moja tisini na mbili na hivyo kufanya mazingira ya shule hizi kuwa mazuri na kuwavutia watoto na uandikishaji kuendelea kuwa mkubwa katika shule zetu hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niingie katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Halmashauri ambayo Mimi ni Diwani na ni Halmashauri ambayo nahudhuria vikao vyake vya Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Shinyanga Vijijini ina Shule ya Sekondari ya Zunzuri, shule hii ni kongwe, shule hii ina kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne lakini Halmashauri tulikaa kwenye Baraza la Madiwani tukakubaliana shule hii tuweke kidato cha tano na cha sita. Baadhi ya miundombinu tumekwishaiweka katika shule hii, vimebaki vitu vichache ambavyo havijakamilika bwalo la chakula, bweni moja, ukarabati wa maabara tatu pamoja vifaa vyake na vitanda 48.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa naomba niseme kwenye shule hii ya sekondari. Hazina walikuwa wanapeleka fedha katika shule moja inaitwa Tinde Day wakifikiri kwamba ile shule ni ya Boarding. Kwa hiyo fedha zile zilikuwa zinakwenda pale kimakosa, Halmashauri na Mkurugenzi wakachukua jukumu la kuiandikia barua Hazina kuomba kubadilisha fedha zile kuzipeleka kwenye Shule ya Sekondari ya Zunzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI walijibu barua ile wakakubali kuruhusu kubadilisha fedha hiyo na baada ya TAMISEMI kutoa barua kuruhusu kubadilisha fedha hiyo Halmashauri ilianza kutumia fedha hizo. Kwa masikitiko makubwa Hazina wameandika barua kumzuia Mkurugenzi asiendelee kutumia fedha hizo kwa matumizi ya Shule ya Sekondari Zunzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa Hazina ni nani na TAMISEMI ni nani! TAMISEMI wameruhusu na fedha ile ikaanza kutumika ili kuboresha maeneo haya na kidato cha tano kiweze kuanza kufanya kazi, lakini leo hii Hazina wameandika barua kumzuia Mkurugenzi na wanamtaka Mkurugenzi arudishe fedha ile. Naomba majibu ya Serikali, Serikali ni moja, Halmashauri ni moja ni kwa nini wanazuia matumizi ya fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusemea Shule ya Sekondari ya Zunzuri, naomba niisemee Shule ya Sekondari ya Wasichana iliyopo Tinde. Shule ya Wasichana ya Tinde ni ya kidato cha tano na sita. Shule hii ina miundombinu mizuri, nyumba za Walimu za kutosha, madarasa ya kutosha, maabara, lakini shule hii haina bwalo wala ukumbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha unapokuwa katika mazingira yale kama mvua inanyesha wanafunzi wanakula nje wakati mwingine wananyeshewa na mvua. Mheshimiwa Waziri wa Elimu nilimwomba na narudia tena kumwomba leo hii humu, chonde chonde aitizame Shule ya Wasichana ya Tinde. Yeye ni mama nina hakika anajua akimwelimisha mwanamke, akimwelimisha binti atafika na yeye hapo alipofika yeye, naomba aitizame Shule ya Wasichana ya Tinde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Sasa naomba niongelee Shule ya Msingi Masunula iliyopo katika Kata ya Usule. Shule ya Masunula ipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Shule hii imekuwa ikifanya vizuri kwa miaka mitatu mfululizo, imekua ikiongoza ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa shule hii haina nyumba hata moja ya Mwalimu. Hivi tunawatazamaje Walimu hawa ambao kwa miaka mitatu mfululizo wameweza kutufundishia watoto wetu na shule ile kuweza kuongoza kwa ufaulu. Niiombe sana Serikali tunaomba waitizame shule ya Msingi ya Masunula waweze kutujengea nyumba za watumishi kwa sababu shule hii haina nyumba hata moja ya mtumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga fedha za maendeleo, kwa masikitiko makubwa hili naomba niliseme. Mwaka 2016/2017 tuliidhinishiwa fedha za maendeleo bilioni 1.6, lakini fedha ambayo Halmashauri ilipokea ni milioni 420 tu. Fedha zingine zote hazikuweza kufika. Mwaka wa fedha 2017/2018 tuliidhinishiwa bilioni 1.7; mpaka hivi ninavyoongea Halmashauri haijapokea kiasi chochote cha fedha ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili naomba sana Serikali ilitazame kwa macho mawili, ni kwa nini halmashauri yetu tunakuwa tunaidhinishiwa pesa, lakini fedha hizi hazifiki. Naomba nipate majibu ya kutosha ni kwa nini Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mpaka sasa hivi hatujapata fedha ya Maendeleo hata shilingi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisemee suala la Watendaji. Suala la Watendaji...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na naunga mkono hoja.