Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kuweza kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba hii muhimu jioni ya leo. Kwanza kabisa niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi inazochukua ili kuweza kukuza uchumi, tumeona kwamba uchumi unakua kwa asilimia 6.8 na Tanzania ni moja miongoni mwa nchi tano za Afrika ambazo uchumi wake unakua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye taarifa tumeelezwa zaidi ya viwanda 3,000 vimeweza kuanzishwa. Kwa hiyo hiyo ni hatua nzuri na ni dhamira ambayo Serikali ilivyoingia madarakani ilionesha kwamba jambo hilo litaweza kufanyika. Juzi tumeshuhudia pia uzinduzi wa lot two ya ujenzi wa standard gauge, hiyo ni hatua kubwa ya kuweza kuimarisha uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia Waziri Mkuu akizunguka maeneo mbalimbali kuhimiza suala la kilimo, kilimo cha pamba kinakwenda vizuri, korosho zimepanda bei na mazao mengine ambayo yameainishwa hapa mazao ya kimkakati. Sasa pamoja na pongezi hizo yapo mambo machache ambayo Wabunge inabidi tushauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na kilimo, ule wigo wa mazao ya kimkakati uko umuhimu wigo huo ukapanuliwa. Kwa mfano, juzi Rais alizindua kiwanda cha mafuta cha alizeti Singida. Sasa zao la alizeti na lenyewe linatakiwa lipewe mkakati Dodoma, Singida na Shinyanga tuweze kulima zao la alizeti na tukilima zao la alizeti kwa wingi tunaweza kusaidia kuokoa fedha za kigeni ambazo zinatumika kuagiza mafuta nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu Bungeni huwa tunalumbana sana suala la kusema mafuta nje yasiagizwe, lakini mbegu zilizopo ndani ya nchi zinakuwa hazitoshi, sasa ni lazima uwekwe mkakati ikiwepo, kuwepo na ruzuku ya mbegu na mbolea ili zao hilo liweze kuzalishwa kwa wingi na tuweze kuvuna mazao ambayo yataleta tija kwenye viwanda vyetu, kwa sababu viwanda hivi vinategemea sana sekta ya kilimo. Kwa hiyo, sekta ya kilimo ikiimarishwa tutaweza kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nimeambiwa kwamba kuna malighafi ngano inaagizwa nje ya nchi na baadhi ya Wawekezaji ndani ya nchi humu, lakini zamani NAFCO walikuwa wanalima sana ngano na ilikuwa ni ya . Kwa hiyo, ni lazima mazao kama ngano na yenyewe yaweze kuangaliwa na tuweze kuyawekea mkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kuzungumza ni suala la elimu, nitazungumza kidogo sana kwa sababu kila siku tumekuwa tunazungumza na Wabunge wamekuwa wakizungumza suala la ubora wa elimu. Nimejaribu kufanya utafiti tu hasa katika Wilaya mpya hizi. Katika Wilaya mpya unakuta kwanza miundombinu yenyewe haitoshi, unakuta Wakaguzi na Waratibu Kata wapo, lakini Waratibu na Wakaguzi hawana usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya kama ya Mkalama haina gari la Wakaguzi, sasa huo ubora wa elimu wameachiwa Mkuu wa Shule na Walimu, kama utaratibu ulikuwa umeweka kuwepo na Wakaguzi wa Wilaya na Waratibu wa Kata ilikuwa ni muhimu kuhakikisha kwamba na mambo yanayohusiana na kusimamia ubora wa elimu yanawekwa vizuri ilikuwa ni jambo la muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la Walimu hawatoshi katika ngazi ya shule za msingi na sekondari na pia tukizingatia kwamba suala la elimu bila malipo limeongeza udahili wa wanafunzi. Pia tunaomba suala la VETA liimarishwe, kuna tozo iliwekwa hapa, tumetembelea VETA hivi karibuni tukaona kwamba pesa zile hazirudi, kwa hiyo tunaishauri Serikali iweze kurudisha ile tozo iliyokuwa inatozwa kwa maana ya kupelekwa VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ni chombo kizuri kimeanzishwa, kinafanya kazi vizuri tuna imani nacho, lakini wenzangu wamezungumzia suala la uwakilishi wa TARURA kwamba wapi tunakutana na TARURA ili tuweze kutoa mawazo yetu. Ni jambo la muhimu inabidi kuangaliwa. Pia bajeti ya asilimia 30 kwa 70 TANROAD na TARURA bado inaleta mashaka ufanisi wa TARURA, TARURA itakuwepo pale lakini haitakuwa na ufanisi sana kwa sababu pesa zinazopelekwa kule zitakuwa hazitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunaomba Serikali iweze kuangalia namna ya kuipatia pesa zaidi TARURA ili kubadilisha mfumo wa mgawanyo labda iwe 40 kwa 60. Tunafahamu kwamba barabara za lami ni gharama na barabara ikishakuwa ya lami inatakiwa iendelee kuwa ya lami lakini bado tunahitaji barabara za vijijini ili ziweze kutoa mazao vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya niipongeze Serikali kwa kutoa pesa kuimarisha vituo vya afya Tanzania nzima ikiwemo Mkalama tulipata milioni 300 za kununua vifaa na kasi ya ujenzi inaendelea vizuri na sasa wananchi watapata tiba na Serikali itaonekana kwamba ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya msingi ambayo bado ipo hapa ni suala la Wilaya mpya ikiwepo Wilaya ya Mkalama. Sasa Wilaya mpya hazina hospitali za Wilaya, kwa hiyo kwa maelezo ama jibu ambalo lilitolewa na Naibu Waziri wa Afya asubuhi natumaini na Mkalama nayo mwaka huu itapata hospitali ya Wilaya. Bado tunasisitiza kwamba Wilaya mpya zote ziweze kupata hospitali, hilo ni jambo muhimu na ule mnyororo wa tiba uweze kukaa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme tunaipongeza Serikali kwa kuweka mikakati ya kuongeza umeme katika gridi ya Taifa, kuanzisha Stieglers Gorge na miradi mingine kama Kinyerezi I, II na III. Ni jambo zuri kuleta umeme ambao utasaidia viwanda na viwanda bila umeme haviwezi kuwa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiunganisha na hapo, suala la REA, REA inafanya kazi nzuri lakini bado katika baadhi ya Mikoa speed yake ni ndogo na scope yake kwa maana ya kwamba nguzo ngapi zinakaa katika kijiji ni jambo muhimu ambalo inabidi liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri muhusika kwa sababu alifika katika Mkoa wetu wa Singida na bahati nzuri alifika Mkalama na alifanya kazi nzuri na kuna mahali umeme umewaka lakini bado tunataka kwenye miradi ya REA II ambayo ilikuwa haijakamilishwa iweze kukamilishwa, maana yake nguzo zipo kule na waya zipo wananchi wanaangalia, sasa wanaanza kusema umeme tutauona lini, wanaanza kukata tamaa, lakini kwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano nafikiri jambo hili litakaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala moja la msingi, suala la maji vijijini. Hotuba ya Waziri Mkuu imezungumzia suala la maji vijijini, lakini katika bajeti tuliona kwamba kulikuwa na mradi wa vijiji 10, visima hivyo virefu vimechimbwa vipo lakini havijajengwa na ukiangalia bajeti nyingi kwenye Wilaya wanatoa milioni 400 mpaka milioni 600. Mradi mmoja kujenga ni milioni 400, ina maana kama umechimba visima 10 itachukua miaka 10 kuweza kujenga miradi hiyo ya maji. Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo inabidi litafakariwe upya na liweze kupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tuanzishe Wakala wa Maji, tumeanzisha Mfuko wa Maji lakini sasa ianzishwe Wakala wa Maji kama vile REA inavyofanya kazi.
Wakala wa Maji akianzishwa atakuwa na kazi ya kutafuta pesa na kutekeleza miradi na kukabidhi miradi. Jambo hilo litakuwa mwarobaini wa upatikanaji wa maji hasa vijijini. Kwa hiyo, jambo hilo na lenyewe tunashauri Serikali iweze kulichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kupongeza baadhi ya taasisi, nipongeze TEA kwa sababu wanasaidia sana katika sekta ya elimu, wamefanya kazi kubwa sana na hata Jimboni kwangu wameweza kufanya kazi kubwa sana. Pia nipongeze TAMISEMI kwa kusaidia miundombinu na kuleta watumishi inagwaje bado tunahitaji watumishi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu inatekeleza sasa ili kuunganisha Mkoa kwa Mkoa. Daraja la Sibiti linaendelea vizuri na kabla ya kuja huku nilifika Sibiti na wananchi wana matumaini sana na daraja la Sibiti, tukimaliza Daraja la Sibiti sasa tunatarajia kwamba barabara hiyo itajengwa barabara ya lami na kuweza kurahisisha usafiri wa mizigo na raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja. Ahsante.