Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze kwa kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi na kwa Mkuu wake, jemedari wetu Mkuu Dokta John Pombe Magufuli, kwa kuongoza kazi nzuri anazozifanya, anatekeleza vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na hili niliseme tu, kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ninavyomuona namkumbukia sana Simba wa Nyika, Marehemu Mheshimiwa Mfaume Kawawa ambaye enzi hizo alikuwa akiagizwa kutekeleza jambo anatekeleza, Mungu amrehemu mahali alipo. Waziri Mkuu kila anapopewa nafasi ya kutekeleza mambo anatekeleza vizuri sana. Nimpongeze kwa kweli kwa mambo yote hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza mambo madogo tu kwenye hii bajeti na kwenye hii hotuba ninayotaka kuitoa hapa au kwa maelezo ninayotaka kutoa; kwamba, hivi mtu akipata nafasi ya kuchangia kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, hivi mwaka ujao yale aliyoyasema atayaona mawili, matatu yametendeka au ni kusema tu halafu yanaishia hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kusema kwamba kwa nafasi hii nitakayokuwa nayasema hapa nataka kuyapima kwamba mwaka ujao nitakuja kuona nafasi nilichangia kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, yale niliyoyasema japo mawili matatu yametendeka? Kwa hiyo, nafikiri hili jambo litakuwa bora zaidi kwa Bunge kuchangia hii ofisi kwa sababu ndiyo eneo kubwa ambalo Waziri Mkuu analiongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze kwenye miradi ya Jimbo langu la Bunda. Tuna miradi ya maji, katika miradi ya maji ya Jimbo la Bunda iko miradi mingi sana. Nimpongeze Waziri wa Maji, amekuja pale mara nyingi sana, kuna Mradi mmoja unaitwa Nyang’alanga – Mgeta ambao ulianza kwa bajeti ya milioni 495, sasa una milioni 910 mradi haujaisha na maji hayajatoka. Kila siku ripoti zinakwenda na hakuna ukaguzi unaofanyika wa kutoa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,ahati nzuri Naibu Waziri wa Maji amesema wale wote wanaohujumu fedha za maji watakipata cha moto. Namwomba afike pale sasa aone namna ya kuwashughulikia mradi wa maji Nyang’alanga ili kuweza kumuondoa mtu ambaye amekaa pale kwa muda mrefu na hakuna kazi inayofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mradi wa Malambo. Bunge lililopita nilizungumza hapa malambo 12 yaliyokuwa yanataka kutengenezwa ya zamani kuyafufua. Tunayafufua kwa sababu kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye Jimbo langu ni kilometa 25 lakini sisi maji hatuna tuna tabu sana ya maji katika Jimbo la Bunda. Tunataka kufufua malambo ya zamani yaliyochimbwa na Mtemi Makongoro na tumeleta bajeti kwenye Wizara ya Maji na Katibu Mkuu Wizara ya Maji alipokea huo mradi wetu na tunaomba aushughulikie, ninashauri haya mambo yafanyike mapema ili tuweze kupata maji kwenye Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya wanyama waharibifu kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina vijiji 11 ambavyo wanyama waharibifu wapo kila siku, kila mazao yanayolimwa yanaliwa, hata katani zinazopandwa zinaliwa, hata pamba inayolimwa sasa hivi inaharibika. Tunaomba Serikali sasa ichukue hatua za kutosha za kuzuia wale wanyama wasiwe wanakuja kuharibia wananchi mazao ili wananchi waweze kujineemesha kwa sababu yale mazao ndiyo kipato chao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu fidia. Toka haya mazao yameanza kuliwa tunadai zaidi ya milioni 360, kulikuwa na milioni 400 wameshalipa karibu milioni 182, kwa hiyo bado milioni 360 zinadaiwa, tunaomba Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na nimwombe Waziri Mkuu ahimize hii fidia ya wakulima iweze kupatikana kwa Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya afya katika Jimbo langu. Tumejenga zahanati tano na mpaka zahanati zingine tumeshaezeka, tunaomba Serikali, kwa sababu Bunge lililopita Wabunge walisema hapa, maboma yote ya zahanati zote na maboma ya vituo vya afya wakasema na Bunge la Bajeti hapa tulizungumza na Bunge lililopita tulizungumza, kwamba maboma yote yashughulikiwe na yaletwe hapa Bungeni na tuweze kutengeneza mkakati maalum wa kuyamaliza, sasa sijui hatua imefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa maboma matano ya vijiji vilivyotengeneza kwenye jimbo langu, Kijiji cha Kambubu, Chiling’ati, Komalio na Malambeka ili waweze kupewa fedha za kuweza kumalizia majengo haya. Nimuombe Waziri wa Afya aweze kutusaidia na Wizara ya TAMISEMI iweze kutusaidia katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya barabara, habari ya barabara ya lami kutoka Makutano kwenda Nyamswa hadi Sanzati, inaitwa makutano ya barabara ya lami kutoka Makutano – Sanzati. Ninavyozungumza hii barabara bila unafiki, Mheshimiwa Waziri Mkuu namshukuru sana alikuja Mkoa wa Mara na akapita kwenye ile barabara akaiona, ni vitu vya aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayopita kwenye maeneo ya kaburi la Baba wa Taifa imekaa miaka zaidi ya sita haimaliziki na wale watu wanaotengeneza hiyo barabara wale wakandarasi hawaguswi, hivi ni akina nani hawa? Barabara ipo kila siku na vumbi zinakwenda kwenye kaburi la Mwalimu pale, hakuna mtu anamaliza hiyo barabara, why?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii tupo tunavuta upepo, huu upepo tunaovuta ni wa Mwalimu. Jamani mambo gani hayo? Aibu hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameliona hilo, nadhani atalishughulikia haraka iwezekanavyo ili tuweze kuzungumza haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara ya Nyamswa – Bunda, tuliahidiwa kupewa mkandarasi lakini hajaenda. Tuna Barabara ya Sanzati – Nata, mkandarasi hajapatikana, na kuna barabara ya kutoka Bunda kwenda Buramba na Buramba – Kisoria, mkandarasi bado naye anasuasua hajawa kwenye uwezo mzuri. Tunaomba Serikali ione namna gani ya kumaliza zile ahadi zake na hasa ile miradi ya muda mrefu ambayo inahitaji kumalizika. Barabara ya Makutano – Nyamswa – Sanzati ni ya muhimu sana, imeleta kero kubwa sana kwa wananchi wa Butiama na wananchi wa Kata ya Nyamswa na maeneo mengine yaliyopakana na barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi; namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja Mkoa wa Mara, amezungumza na ametusaidia mambo mengi, lakini migogoro ya Vijiji vitatu vya Silolisimba, Lemuroli na Mkomalilo bado vina matatizo ingawaje Mkuu wa Mkoa anajitahidi kumaliza tatizo hilo, lakini bado, tunamuomba na bahati nzuri siku moja Mheshimiwa Naibu Spika alitamka hapa Bungeni kwamba Serikali ishughulikie namna ya kumaliza tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuone namna gani ya kulimaliza ili wananchi waweze kukaa vizuri kwa sababu kila siku ni mapanga. Bahati nzuri miezi miwili iliyopita wananchi wawili walikufa kwa ajili ya mapigano ya hiyo mipaka, kwa hiyo tunaomba tuone namna ya kulimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya Watendaji; katika jambo ambalo Wabunge tunashauri kwa kila mara na kama tuko Kikatiba katika kushauri jambo hili, hili suala la Watendaji hawa ambao tumepanga kuwafukuza, nadhani katika jambo ambalo tunaweza kulihimiza Bunge lifanye ni namna gani ya kuwaacha wale Watendaji wamalize muda wao, kwa sababu wengi wamemaliza miaka miwili, mitatu, minne, mitano, kuna haja gani ya kuwatoa sasa hivi? Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri tuone namna gani na tupate majibu mapema ili tujue namna ya kuwasaidia hao Watendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina miradi ya REA vijiji 21, Jimbo langu katika Mkoa wa Mara ndiyo Jimbo lenye vijiji vingi ambavyo havijafikiwa na umeme ingawaje Mheshimiwa Waziri amenisaidia vijiji vingine huko nyuma vilikuwa 32 sasa vimebaki 21. Tunamwomba yule mkandarasi wa REA kwenye Jimbo langu na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alifungua mradi wa REA kwenye Jimbo langu, ajitahidi kumhimiza mkandarasi aweze kuimaliza ile miradi kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya Bandari ya Musoma, kuna miradi mikubwa pale ya Kimkoa, kuna mradi wa bandari na kuna mradi wa kiwanja cha ndege Musoma na mradi wa Hospitali ya Kwangwa. Kwa hiyo, Mkoa wa Mara kuna miradi mikubwa kimkoa, tunaomba Serikali iangalie namna ya kuimaliza ili wananchi wa pale waweze kupata huduma za kutosha katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu la Bunda na Bunda nzima na Jimbo la Bunda, ardhi yetu imechoka sasa, tunaomba kama kuna uwezekano wa kupata pembejeo kwa ajili ya wakulima sasa na sisi tuingizwe kwenye mradi huo wa kupewa pembejeo ili wakulima waweze kupata mazao mazuri kwa sababu ardhi yao imechoka kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya Walimu wa sayansi shule za msingi na sekondari. Katika maeneo mengi ya Jimbo la Bunda kuna sekondari zaidi ya tisa hakuna Mwalimu hata mmoja wa sayansi. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri sasa Waziri anayehusika aweze kuona namna gani ya kutusaidia Walimu wa sayansi kwenye sekondari tisa katika Jimbo la Bunda ambazo hazina Walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vingine naviona hapa nikivisoma huwa vinanitia kichefuchefi kidogo. Kuna deni la watumishi wa Serikali, lakini ukiangalia deni la watumishi wa Serikali kuna vitu vingine vya kujitakia. Hivi inawezekanaje leo tuna watumishi wanaokaimu wengi katika Wizara mbalimbali na kila mtumishi anayekaimu anapewa nusu ya mshahara wa mtu aliyekuwepo katika nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kama Mkurugenzi aliyetoka alikuwa anapokea mshahara wa milioni tano na yeye anaenda kukaimu anapokea milioni mbili na nusu na anakaa miaka kumi, mitano, saba, kumi na tano. Sasa hii kwa nini tunaitafutia Serikali madeni, kwa nini tusibadili sheria hizi za utumishi za kukaimu na sheria zile za kwenda kwa wakati wanakaimu kama ni mtu kwenda kukaimu tumwambie akaimu bure, sio akaimu kwa kulipa mshahara, tunatia madeni Serikali bure na tuangalie ile sheria namna ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kuangalia sheria ndogo hizi au sheria za Wanyamapori, Maliasili na Utalii na hasa zile sheria za fidia. Fidia imekuwa ndogo sana lakini mbaya zaidi kuna sheria zile za fidia ambazo hazijakaa sawa. Kwa mfano, kutoka mpaka wa wanyamapori kwenda kwa wananchi wanasema iwe ni mita 500, mita 500 ni nusu kilometa, lakini kutoka hiyo nusu kilometa buffer zone kwenda mpaka kilomita 1000 mkulima anatakiwa kulipwa kama amelima shamba heka 20 halafu tembo amekwenda amekula mazao yote, anatakiwa kulipwa heka tano tu, heka 15 nyingine ni sadaka, hii sheria ya wapi tena? Nafikiri kwamba ni vizuri wakaangalia hiyo sheria...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.