Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa nafasi niweze kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu. Kwa namna ya kipekee naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na kazi nzuri anayoifanya katika kusimamia. Kwa namna ya kipekee nimpongeze sana dada yangu, Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na ndugu yangu, Naibu Waziri, Mheshimiwa Antony Mavunde, kwa kazi nzuri sana wanayoifanya katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajielekeza kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwenye eneo la kilimo. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesema kwamba Watanzania walioajiriwa katika Sekta ya Kilimo ni kati ya asilimia 65 mpaka 75. Pamoja na ajira ya Watanzania wengi katika eneo hili, lakini bajeti inayopelekwa kwenye eneo hili ni ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji halisi ya kwenye bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tulikuwepo kwenye Makubaliano ya Maputo na Maraba ambapo katika makubaliano haya tulikubaliana kwamba asilimia 10 ya bajeti itengwe kwa ajili ya Sekta ya Kilimo. Katika hali ya kusikitisha kabisa, katika eneo ambalo linaajiri watu wengi, hata asilimia tano ya bajeti iliyotengwa kwenye eneo la kilimo haitokani na Bajeti Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nichukue fursa hii kumshauri sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama tunataka tuwasaidie wale wakulima na kama kweli tuna target ya kweli kwenda kwenye uchumi wa viwanda, ambapo katika uchumi huo raw material ya kutosha inapatikana kwenye eneo hili la kilimo zaidi ya asilimia 85, tutakuwa tunajidanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama we are serious enough tu-invest kwenye eneo hili ili tuwe tuna uhakika kwamba tunaweza kuwasaidia wakulima na ile dhana ya kwenda kwenye uchumi wa viwanda itapatikana kama wakulima wengi watapata fursa za kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano tu, mwaka 2017 kumekuwa kuna mgogoro mkubwa sana. Wakulima wamejitoa, wamelima sana lakini matokeo yake wamepata hasara, tumeshindwa kununua yale mazao kwa sababu tulikuwa hatuna masoko ya uhakika. Naishukuru Serikali kwa kuruhusu kwamba sasa hivi mahindi tunaweza tukauza nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, NFRA wameomba kwenye bajeti yao shilingi bilioni 86, lakini cha kusikitisha inaonekana Serikali haitaweza kuwapa hata robo ya ile hela waliyoomba. Sasa tutakwenda kweli tunakokusudia? Kwa hiyo, uchumi ule wa viwanda hauwezi kupatikana kama hatutakuwa serious kwenye kuwekeza kwenye eneo hili la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha sana, haya ni masikitiko ambayo tunayo wawakilishi wananchi; mara ya mwisho Mheshimiwa Waziri Mkuu alikaa na Mawakala wa Pembejeo lakini mpaka leo halijatoka tamko lolote la Serikali kwamba ni lini watawalipa wale Mawakala wa Pembejeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea Waziri Mkuu alipokuja kwenye kusoma hotuba yake hapa, angesema mpaka sasa hivi tumeona Mawakala kadhaa ndio ambao wako supposed kulipwa kwenye hili eneo. Sasa Mawakala wanakufa, mali zao zinataifishwa na mabenki kule, hali inazidi kuwa mbaya. Kwa hiyo, nataka Waziri Mkuu atakapokuja kuhitimisha namwomba sana azungumzie hili kwani mawakala wanataka kumsikiliza kule nje, atoe kauli ili waweze kujua kwamba Serikali yao imeamua kuwasaidia kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubali kwamba tunataka tuwekeze kwenye eneo la kilimo, lakini tunawekezaje kwenye eneo hili? Nataka nizungumzie kidogo suala la pareto. Pareto inalimwa nchini hapa, lakini cha kusikitisha kabisa, ile hatua ya mwisho ya kuitengeneza ile pareto ili tupate bidhaa, haifanyiki hapa nchini. Yale material yanachukuliwa yanapelekwa Marekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimesema tuwekeza sana kwenye eneo hili. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuwahamasishe wakulima katika maeneo mbalimbali, walime pareto kwa wingi ili ile final product ipatikane hapa ndani ya nchi. Ikipatikana itatusaidia kama Tanzania kupata hela nyingi katika maeneo haya. Refining ifanyike hapa hapa Tanzania. Tukifanya hivyo kwenye eneo hili, tutakuwa tuna uhakika wa kutengeneza ajira ya kutosha ambayo wananchi wetu watapata kutoka kwenye maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme tu kwamba ili twende kwenye uchumi wa viwanda, lazima tuhakikishe Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda inafanya kazi simultaneously. Wasipofanya kazi kwa pamoja, uchumi wa viwanda utakuwa hadithi katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la maji. Maji ni uhai. Ukizungumza hapa, hakuna Mbunge ambaye hana tatizo la maji. Sasa sisi kama Wabunge tumekuja na hoja mbalimbali kuhusu kesi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza, sisi kama Wabunge tuliomba Serikali iongeze Sh.50/= kwenye kila lita ya petrol. Kwa masikitiko makubwa, katika hotuba ya Kamati ya Kilimo ya mwaka 2015/2016, Bunge lako hili liliazimia kwamba Sh.50/= iongezwe pale, lakini maazimio ya Bunge yanashindwa kutekelezwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, atakapokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu atuambie, kwa nini wanashindwa kutekeleza maazimio ambayo Bunge lako Tukufu limepitisha hapa? Maji ni uhai, lakini kwa masikitiko makubwa sana tuna tatizo. Serikali ilikuwa inatakiwa ipate shilingi bilioni 500 kutoka kwenye Serikali ya India kwa ajili ya kupeleka maji katika miji 17. Serikali inapata kigugumizi gani cha kutokusaini ule mkataba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yangeenda kwenye ile miji 17, nina uhakika kabisa tungepunguza gap kubwa la matatizo ya maji katika maeneo haya. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali, kwa sababu Head Prefect wa Serikali ndio Waziri Mkuu; aje atuambie Serikali iko tayari sasa hivi kusaini mkataba wa shilingi bilioni 500 ili miji 17 iweze kupata maji ya uhakika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia, kwamba imefika wakati sasa uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini uwepo, kwa sababu maji yana tija. Kwa mfano, bajeti ya mwaka 2017 nyingi ambayo tumefanikiwa katika maeneo imetokana na Mfuko wa Maji. Mfuko wa Maji ulitengewa shilingi bilioni 158 na mpaka sasa hivi zimeshatumika shilingi bilioni 130 ambazo zinatokana na Mfuko wa Maji. Asilimia 66 ya bajeti ambayo imetoka kwenye maji inatokana na Mfuko wa Maji. Kwa hiyo, kuna haja ya kuongeza hela kwenye Mfuko huu ili watu walio wengi waweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiongeza hii shilingi 50, nina uhakika kabisa tutapata shilingi bilioni 316. Tukiamua kila shilingi bilioni kumi tukaipeleka kwenye kila mkoa, baada ya miaka mitatu kutakuwa hakuna kabisa tatizo la maji. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali, sisi ndio wenye wananchi; ukiongeza hiyo Sh.50/= sisi ndio tutakwenda kuwaambia wananchi kwa nini tunataka Sh.50/= iongezwe kwenye maeneo haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu, sisi kama CCM, Serikali ya CCM, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu tuichukue ajenda ya maji kama ndiyo ajenda ya kufa na kuzikana kusudi tuweze kuwatua akinamama ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuchangia ni eneo la…
T A A R I F A . . .
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa. (Kicheko/Makofi))
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa kwa sababu Mbunge mwenzangu anataka Mheshimiwa Waziri Mkuu asikilize zile hoja, sisi Wabunge tunasema nini? Waziri Mkuu ndio Head Prefect wa Mawaziri wote, atusikilize. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maazimio very sensitive ya Bunge ambayo Bunge lako Tukufu limepitisha, hasa la kuongeza Sh.50/= kwenye tozo ya maji. Wabunge wote kilio chao cha msingi ni maji. Nimesema tu kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tunataka tuichukue agenda ya maji kama ndiyo ajenda kuu katika Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni eneo la mifugo na uvuvi. Kuna baadhi ya Wizara kazi yake ni ku-consume tu. Wizara ya Miundombinu yenyewe inapewa hela na kutumia tu, lakini kuna baadhi ya Wizara zikiwezeshwa zitakuwa zinapewa hela na zenyewe zinatoa hela. Kwa hiyo, ufike wakati tuziangalie Wizara kama ya Mifugo na Kilimo, kwamba kama ikiwezeshwa vizuri to some extent tunategemea kupata hela (returns) kutoka kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umekuwa ni utaratibu wa kila mwaka kwa hizi Wizara hatowezeshwa fedha za kutosha. Kwa hiyo, ufike wakati tuzisaidie hizi Wizara. Eneo hili ndilo ambalo linatengeneza ajira kwa urahisi kuliko maeneo mengine yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la mwisho ambalo nataka nilizungumze kuhusu maziwa. Hili eneo la maziwa ni very sensitive. Kama tunaweza ku-protect maziwa yanayotoka nje ya nchi, tutakuwa tumeisaidia nchi yetu kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kuvilinda viwanda vya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya kuvilinda viwanda vya ndani ni lazima tu-protect viwanda vyetu kwa kuongeza kodi kwa bidhaa za nje. Kwa masikitiko makubwa asilimia 80 ya maziwa yanayokuwa imported kutoka nje ya nchi, yanaliwa na viongozi na taasisi za Serikali. Kwa hiyo, badala ya kusaidia kuvilinda viwanda vyetu vya hapa nchini, sisi tumekuwa ndio tunachangia kuvi-promote viwanda vya nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, litoke tamko kama lililotoka kwenye furniture kwamba sasa umefika mwisho wa kutumia maziwa kutoka nchi ya nje, hasa kwenye ofisi zetu za Serikali.