Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu iliyowasilishwa na Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Tanzania ni nchi ambayo imeingia katika Mfumo wa Vyama Vingi na hayo yametamkwa na yapo katika Katiba yetu. Kama tunatambua Mfumo wa Vyama Vingi, maana yake tunaamini kwamba Serikali inatambua vyama vilivyopo ambavyo vinaunda huo Mfumo wa Vyama Vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri Mkuu ameeleza kwamba tuko kwenye Mfumo wa Vyama Vingi takriban miaka 23 leo; na vyama hivi vimeendelea kukua kadri miaka inavyoendelea. Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani inaonesha jitihada kubwa sana za kuua vyama hivi kwa kuvinyima haki yake ya msingi ambayo inapaswa kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Uwepo wa vyama hivi unatambuliwa na sheria, ufanyaji wa kazi wa vyama hivi umetamkwa katika sheria. Maana yake Vyama vya Siasa vinatakiwa viendelee kufanya kazi ya siasa kwa kuhakikisha vinaendelea kupata wanachama kadri inavyowezekana na kadri ambavyo miaka inazidi kwenda. Haya yamesemwa na Waziri Mkuu katika hotuba yake ukurasa wa 10, amesema:

“Katika kipindi hiki tumeona ushiriki wa Watanzania katika siasa ukiendelea kuongezeka na uhuru wa kujiunga na vyama vya siasa umeendelea.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unajiuliza, kama Vyama vya Siasa ili viendelee kupata wanachama, maana yake ni lazima vifanye mikutano ya hadhara kunadi na kueleza sera zake, ndivyo ambavyo mwananchi ataamua sasa ajiunge na chama hiki au aende chama hiki au asiwe na chama mpaka pale ambapo ataweza kuridhika kuamua kujiunga na chama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naeleza kwamba ili Mheshimiwa Waziri Mkuu tukuelewe kwenye kauli hii kwamba vyama hivi vinaendelea kufanya kazi yake, halafu huku mmebana uwepo wa mikutano ya hadhara, ni kwa uhakika mnalidanganya Taifa hili na mnawadanganya Watanzania. Utaendeleaje kupima kwamba Chama cha Siasa kinakua kama hakifanyi mikutano ya hadhara ikaongeza wanachama? Vyama vya siasa ni kama Makanisa leo mtu anajiunga, kesho anatoka. Ndivyo hivyo.

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu wanisikilize vizuri, naongelea Vyama vya Siasa. Siongelei Mbunge wala Diwani. Kwa hiyo Mheshimiwa Vuma naomba unisikilize vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama mnakataza Vyama vya Siasa visifanye mikutano ya hadhara, hamwezi leo kuja hapa Bungeni na kutuambia kwamba vyama hivi vimeendelea kufanya vizuri miaka 26 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma, waasisi wa nchi hii walituaminisha Watanzania kwamba tuna maadui watatu wa nchi hii; umasikini, ujinga na maradhi. Kwa yanayoendelea leo, jambo lingine limeongezeka kwa Serikali iliyopo madarakani, adui mwingine ni Vyama vya Siasa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Kwa sababu leo tunashuhudia Waheshimiwa Wabunge mbalimbali na Madiwani mbalimbali kila siku ama wanaripoti Polisi au wanakamatwa wanaingia Polisi, wanakaa ndani, waliowaweka ndani wakiridhika kwamba sasa wamekaa ndani kwa muda, wanaachiliwa wanaendelea. Kila leo, ama kuripoti Polisi au kwenda Mahakamani. Hapa tuna Wabunge wengi wana kesi kila kukicha, wanahudhuria Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Vyama vya Siasa vya Upinzani ni adui mwingine ambaye mmemwongeza. Kwa nini nasema haya? Tumeshuhudia pia kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika za marudio, kwanza tumefanya Uchaguzi Mkuu 2015, wananchi wameamua kwa ridhaa yao kuchagua mwakilishi wa chama chochote ambacho walikipenda kwa wakati huo na wakawaweka madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani tuna Wabunge wanaotokana na CCM, tuna Wabunge waaotokana na CHADEMA, tuna Wabunge wanaotokana na CUF, tuna Wabunge pia wa NCCR na ACT. Ni ridhaa ya wananchi kwenye maeneo yao wakawachagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kiongozi mmojawapo wa CCM anazunguka kuwarubuni na kuwanunua baadhi ya viongozi na Wawakilishi hao ambao wamechaguliwa na wananchi, wanasema wanaunga jitihada wanaingia upande wa pili labda inawezekana ikawa ni haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba hawa ambao wanarudi upande wa pili inatulazimu kurudi kwenye uchaguzi. Hapa Bungeni tulipitisha shilingi bilioni 4.7 kwa ajili ya Tume ya Taifa Uchaguzi kwa uchaguzi wa dharura endapo itatokea Mwakilishi yeyote amefariki au kwa namna yoyote ameacha nafasi ile. Leo baada ya hizi chaguzi ndogo, tumetumia shilingi bilioni 6.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajiuliza, hivi tunafanya kazi ya kurubuni na kununua wahame upande wa pili; tunarudi tena kutumia fedha za walipa kodi kwenda tena kufanya uchaguzi, huku kuna Watanzania wengi ambao hawana huduma muhimu za kimsingi za kijami! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajiuliza…

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia hapa ni bajeti tunayoitumia bila ulazima wowote. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu, naomba unilinde ninapochangia. Kama kuna Mbunge anataka kunijibu, asubiri akipata nafasi na yeye ajibu ninayoyasema. Halafu najiuliza, haya ninayochangia hapa, kama hamjayafanya kwa nini mnahangaika, si msubiri niseme? Kwa nini mnahangaika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni utumiaji mbovu wa fedha za wananchi. Kama tulitenga fedha za dharura endapo kutatokea chaguzi, shilingi bilioni nne, leo tumetumia shiligi bilioni 6.9, kwa nini tusingefikiria kuendelea ku-save hizi hela na kuzielekeza kuliko kurudisha wananchi kufanya chaguzi tena kwa sababu watu wameamua kununua watu na warudi upande wa pili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata chaguzi za marudio zilipofanyika, tumeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa taratibu nzima za uchaguzi. Uchaguzi huu tulipofanya tumeshuhudia ilikuwa ni uchaguzi kati ya chama kilichosimamisha mgombea; mfano mimi nilienda Siha, nilienda uchaguzi mdogo wa marudio Jimbo la Arumeru Magharibi, tumeona ni uchaguzi kati ya CHADEMA na Jeshi la Polisi. Nilishuhudia Wakala anatekwa Kituoni, Polisi yupo, hakemei, hasemi kitu; hakuna anayezungumza, maana yake tumeingia kwenye uchaguzi kati ya Vyama vya Upinzani na Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu inaonekana mmeongeza adui mwingine ambaye hamtaki kumsikia wala hamtaki kuona Vyama vya Siasa hasa vya upinzani vikifanya kazi yao, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Serikali yako, ni kuleta marekebisho ya Katiba hapa Bungeni tufute Vyama Vingi ulimwengu ujue, dunia ijue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitaki kabisa Mfumo wa Vyama Vingi, turudi kwenye mfumo wa chama kimoja. Nadhani hiyo ndiyo itakuwa njia sahihi na mtaendelea kufanya mnayoyafanya kwa kadri ambavyo mtataka.

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba tu kumwambia Mheshimiwa Mwigulu kwa sababu unaingia kwenye Cabinet, naomba upokee ushauri wangu kumwambia Mheshimiwa Rais Magufuli, tufute Vyama vya Upinzani nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waasisi wa nchi hii walituachia tunu za Taifa zikijikita katika umoja, amani na haki, lakini leo tunashuhudia katika nchi hii hakuna umoja. Umoja ule ambao umejengwa na hawa viongozi ambao walitutoa nchi kwenye utumwa na kwenye ukoloni wakatufikisha hapa tulipo, umoja ule haupo. Kwa nini haupo? Kwa sababu tunashuhudia matamko mbalimbali ya viongozi wakiligawa Taifa. Wakiona wananchi hawa wamevamia ardhi, wanasema hawa msiwabomolee kwa sababu walinipa kura; lakini wengine wanabomolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwalimu Nyerere alituachia tunu ya umoja, lakini leo tunu hii inavunjwa, tuliachiwa amani na mmeendelea kuimba kwamba amani ipo, hakuna amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wana hofu. Leo tunashuhudia wananchi wanaopotea, wapo wanaouawa na wako wanaotekwa. Amani ambayo ni tunu ya nchi hii, haipo tena. Kumekuwa na vitisho vingi. Naona leo tunalijenga Taifa kwenye hofu. Watanzania wana hofu. Tunu ambayo tumeachiwa na Waasisi wetu leo inavunjwa na viongozi na Serikali iliyoko madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeachiwa tunu ya haki. Haki hii inatiliwa msisitizo kwenye Katiba ambayo ni sheria mama. Katiba inatoa msisitizo wa haki ya Mtanzania kuongea kuonesha hisia zake ama kwa kuandamana ama kwa kuandika kwenye mitandao au kwa kusema chochote ilimradi asivunje sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wanatishiwa, wanakamatwa, wanakuwa na hofu ambazo zimejengwa na watu walioko madarakani, wanachukuliwa hatua kinyume na taratibu, hakuna utawala wa sheria, hatuheshimu wala hatulindi tunu tulizoachiwa na Waasisi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.