Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nasoma degree ya kwanza pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilisoma course moja, African Political Thought. Wakati ule napitia kile kitabu, kuna Mwanazuoni mmoja anaitwa Okodiba Noli, aliwahi kusema kwamba “a state is political organization with territoriality recognize boundaries and independent government.” Akiwa na maana ya kwamba nchi yoyote ni taasisi ya kisiasa ambayo ina watu wake, ina mipaka yake lakini kubwa zaidi, ina Serikali ambayo ni independent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia mafuhumu zaidi ya maelezo ya Mwanazuoni huyu, anamaanisha kwamba katika nchi yoyote lazima kuwe na Serikali ambayo kazi yake kubwa ni kulinda rasilimali na kulinda watu wake. Naomba nitumie fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha kwamba inalinda amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na leo hii sisi kama Wabunge tuko katika Bunge hili tukishiriki mijadala hii ya Bunge kwa amani na utulivu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Jeshi la Ulinzi na Usalama na Jeshi la Polisi kwa kuweza kudhibiti hali mbaya ambayo imetokea miezi kadhaa iliyopita pale Kibiti. Sasa hivi sisi wananchi wa Kusini tunapita kwa amani kabisa. Hii ndiyo dhana ya kwamba nchi yoyote iliyokuwa huru lazima iweze kujilinda na iweze kulinda mipaka yake pamoja na raia wake, nalipongeza sana Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, naomba nichukue fursa hii pia kueleza baadhi ya mambo ambayo kimsingi yanapaswa kufanywa sawasawa wakati tunalinda rasilimali na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 25 mwezi wa Tatu pale Mtwara Mjini, kijana mmoja ambaye anajulikana kwa Abdillah Abdulahman, alikuwa katika ufukwe wa bahari wa maeneo ya Kianga akiwa anajitafutia kitoweo, sisi watu wa Pwani tunaita kumbwa, wale wadudu wa sea shells; wakati anajitafutia kitoweo hiki, ghafla wakatokea Jeshi la Polisi ambao tunasema ni kikosi kazi ambacho kimeundwa na Wizara ya Uvuvi na Maliasili, wakawa wamemwita yule kijana. Kijana kwa kawaida, kwa sababu Jeshi letu la Polisi linaogopeka kidogo, alivyoona anaitwa akakimbia. Askari wakaamua kumpiga risasi kisogoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi, wahakikishe ya kwamba wanafanya uchunguzi sawasawa kabla ya kuweza kuchukua hatua hizi za kuweza kuwamiminia watu risasi pale wanapofanya operation maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala la Mahakama ambapo tulipitisha katika Bunge hili tarehe moja mwezi wa Saba mwaka 2017, tulipitisha sheria hapa ya Mahakama ya Mafisadi Tanzania. Jambo la kusikitisha kabisa, ukipitia kwenye Halmashauri zetu, kwa mfano, pale Mtwara Mjini, wafanyakazi wa Halmashauri waliweza kutafuna zaidi ya shilingi milioni 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasilisha taarifa hizi Serikalini kwa muda mrefu sana, lakini jambo la ajabu ni kwamba wanaotafuna hizi shilingi milioni 800 mpaka shilingi milioni 900 hawapaswi kushtakiwa kwenye Mahakama ya Mafisadi. Sasa ni jambo la ajabu sana! Halmashauri kutafuna pesa zaidi ya shilingi milioni 800, ni pesa nyingi sana, pesa ambazo zingeweza kujenga shule, zingeweza kujenga miundombinu, zingeweza kununua dawa, lakini zinatafunwa na wale waliotafuna hawaitwi mafisadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwamba iletwe sheria Bungeni tuipitishe kwamba pesa za Serikali zikitafunwa kuanzia shilingi milioni 200, 300, 400 mpaka 600 bado wapelekwe kwenye Mahakama ile ya Ufisadi. Kuweka shilingi bilioni moja, ni nyingi sana, Halmashauri zetu zinatafunwa sana, tunaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yanavyofukuliwa makaburi katika maeneo mengine; makaburi yanafukuliwa kwenye vyeti, kwenye taasisi za kiserikali, lakini tulikuwa tunaomba sana wale waliotafuna pesa, mabilioni mengi miaka miwili, miaka mitatu, miaka mitano iliyopita, wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mahakama hii ya Mafisadi iweze kuwachukuliwa hatua. Kwa sababu Wanasheria wanasema kwamba sheria haiendi retrospective, lakini kwa sababu Taifa hili limetafunwa sana, Taifa hili tumekuwa masikini hapa kwa sababu ya watu wachache, wajanja wachache ambao tuliwapa dhamana ya kusimamia rasilimali zetu, lakini wamechukua pesa zetu na mwisho wa siku Tanzania tunasema ni maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukipitia kwenye sekta mbalimbali, kwa mfano, Sekta ya Utalii, mabilioni ya pesa yameweza kutafunwa sana. Jambo la ajabu sana, niliwahi kuzungumza wakati nachangia mjadala wa taarifa za Kamati hapa; Taarifa ya Kamati ya Maliasili na Utalii, ukipitia Olduvai Gorge ni eneo pekee ambalo binadamu wa kale alipatikana duniani, liko Tanzania, ni Olduvai Gorge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma ukipitia taarifa za Serikali, Olduvai Gorge ilikuwa inakusanya karibu shilingi 1,700,000,000 kwa mwaka. Sasa hivi wajanja wachache wakahakikisha kwamba Olduvai Gorge wanaitoa kwenye eneo la malikale na kulipeleka kwenye Taasisi ya Ngorongoro na badala yake sasa hivi linakusanya shilingi milioni 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ufisadi. Watendaji wana under estimate pale kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi. Tunaomba Mahakama hii ya Ufisadi Tanzania, ifanye kazi yake ipasavyo. Tusiseme kwamba eti mpaka pesa ifike shilingi bilioni moja, basi mtu aweze kushtakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hapa nimezungumza pia wakati naanza utangulizi wangu kwamba mtengano wowote wa Kitaifa unataegemea na kugawana fursa hizi sawasawa kama Taifa. Leo hii Tanzania kila kanda ina hospitali ya kanda, isipokuwa kanda ya Kusini pekee, jengo linaanza kujengwa takribani miaka 10 iliyopita hivi sasa, mpaka leo halijakamilika pale Mtwara Mitengo. Mpaka leo jengo la Hospitali ya Kanda ya Kusini limejengwa zaidi ya miaka 10 halijakamilika, lakini maeneo yote kuna Hospitali za Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshindwa kuzungumza maeneno haya kwa muda mrefu sana. Tumekuwa tukiongea kwa muda mrefu sana kwamba rasilimali hizi za Taifa zigawanywe sawasawa ili kanda nyingine na Kanda ya Kusini pia tuweze kupata Hospitali hii ya Rufaa, pesa ziweze kutengwa kwenye bajeti zinazokuja, nasi Wanakusini tuweze kunufaika na rasilimali hizi za Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu sana; na ikumbukwe mwaka 2013 wananchi wa Mikoa ya Kusini waliandamana sana wakidai rasilimali ziweze kuwanufaisha kama Watanzania wengine. Wapo watu waliokuja kupotosha Watanzania, wakasema kwamba Wanakusini wanahitaji gesi watumie peke yao, kitu ambacho hakikuwa sahihi kabisa. Tulichokuwa tunasema ni kama ilivyo kwenye korosho kwamba korosho zimekusanya mabilioni ya pesa, pesa zote zinapelekwa katika Mfuko wa Hazina na zinatumika kwa ajili ya Watanzania wote kununua dawa, kujenga barabara na miundombinu mingine ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema suala la umeme Kusini limekuwa ni kizungumkuti sana. Tunaipongeza Serikali kwamba imenunua mashine mbili ambazo zinaenda kutoa megawati nane; bado tatizo la umeme litakuwa ni endelevu, ni miezi zaidi ya saba hivi sasa, Mtwara na Lindi hatuna umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili linapelekea viwanda kutojengwa Mtwara. Pia limepelekea wawekezaji kukimbia Mtwara. Tunaiomba Serikali, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ije na mpango wa kudumu wa kuhakikisha kwamba Mikoa hii ya Kusini tunakuwa na umeme wa uhakika ili wawekezaji waweze kuja Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kama Serikali ingeamua kuondoa tatizo la umeme Kusini ingenunua mashine moja tu ambayo inatoa megawati 20; na tulikuwa tunapitia taarifa mbalimbali, Wizara ikaenda wataalam wakaenda kuangalia Ujerumani, kuna mashine moja ambayo itaweza kutoa megawati 20 za umeme ambazo zitaweza kusambaza umeme Mtwara na Lindi, inauzwa shilingi bilioni 50 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali kweli ingekuwa na nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba inataka kuondoa tatizo la umeme Kusini, basi ingeweza kununua mashine moja ya megawati 20, inauzwa shilingi bilioni 50, siyo nyingi. Kwenye korosho tunakusanya billions of money ambazo zinasaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie kwa jicho la kipekee kabisa, suala hili la umeme Kusini liweze kwisha. Hatutaki kurudi kule tulikotoka, wananchi wanadai sana. Ukifanya mikutano hadhara, kila mwananchi anazungumza suala la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Serikali iliyopita iliweka utaratibu kwamba pale kunapotoka rasilimali yenyewe, hii gesi basi wananchi wapate unafuu. Ikaweka punguzo la kuunganisha umeme, badala ya kuunganisha umeme kwa Sh.370,000/= ikawa Sh.190,000/= hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila mwananchi anakuja kwenye mikutano ya hadhara anauliza kwani hili punguzo ambalo Serikali liliweka kwa nini mmeliondoa wakati gesi ipo? Nami nauliza, gesi bado ipo, kwa nini punguzo ambalo Serikali iliweka kwenye umeme, leo hii Serikali inasema imeondoa punguzo hili? Naomba sana kwamba sekta hii isaidie Wanakusini ili Serikali iweze kusemwa sawasawa na wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuna suala hili la dawa za kulevya. Tunaipongeza Serikali, imeweza kuzuia dawa za kulevya nchini, ni jambo zuri sana, kwa sababu vijana wetu walikuwa hawaeleweki; ilikuwa inapoteza nguvu kazi. Serikali lazima iwekeze vya kutosha kudhibiti uvutaji na uenezaji wa dawa za kulevya Tanzania. Naiomba Serikali, pale inapofikia kuangamiza madawa ya kulevya, kama inavyochoma moto mashamba ya bangi, basi hata tukikamata Cocaine na Heroin tushuhudie zikiwa zinachomwa hadharani kama zinavyochoma bangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku Serikali imekuwa inatuambia kwamba imekamata kilo 10 kilo 20, gramu sijui ngapi za Heroin au Cocaine, lakini hatuoni zinaangamizwa au zinachomwa moto. Tunataka Serikali iangamize tukiwa tunaona kama tunavyoona kwenye bangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu, pia hotuba ya Waziri Mkuu imezungumza kwamba inatenga zaidi ya shilingi bilioni 20.8 kila mwezi kupeleka shule za msingi na sekondari kwa maana ya kugharamia elimu ya msingi. Ni jambo jema sana. Wakati huo wa nyuma kulikuwa na michango mingi katika shule ambayo ilikuwa inachangishwa na wazazi. Leo hii ukipita maeneo ya kusini, mzazi ukimwambia achangie hata chakula cha mtoto wake ili mtoto aweze kusoma akiwa ameshiba, kile anachofundishwa aweze kukielewa sawasawa, anasema na Serikali imesema elimu bure. Nani amekwambia uchangie? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetamka hapa kwamba michango yote ipitie kwa Mkurugenzi. Mkurugenzi huyu mnamtwisha mzigo mkubwa sana. Haiwezekani leo mpaka mchango wa Sh.5,000/= wa shule ya msingi, shule zote zilizopo za msingi na sekondari akusanye Mkurugenzi. Tunarudisha nyuma elimu yetu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mkurugenzi huyu apunguziwe mzigo na Serikali itoe tamko kwamba suala la chakula cha mchana shuleni kuanzia shule za msingi mpaka sekondari ni jambo la lazima na wazazi lazima wahusike kuchangia chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili limezungumzwa na wenzangu hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia suala la migogoro ya ardhi, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeliona hili kwamba kuna migogoro mingi ya ardhi, ni kweli kabisa. Naitaka Serikali pale ambapo iliahidi kwamba italipa fidia, kwa mfano pale Mtwara Mjini, Mji Mwema, basi ahakikishe kwamba inalipa fidia za wananchi wale siyo Serikali inakuwa na kauli mbili mbili kwamba, leo wanasema tutatoa fidia maeneo tuliyoyachukua, baadaye inasema Serikali haiwezi kutoa. Tutazungumza haya katika Wizara ya Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makaazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.