Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na ninampongeza Mheshimiwa Waziri Jenista, mwalimu wangu, mwalimu wa wangi lakini na Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya, mambo mengi aliyoyaahidi mwaka 2015 tumeona yakiendela kutekelezeka. Aliahidi ndege zitakuja na tumeshuhudia zikija, kwa kweli tunamshukuru sana.

Nashukuru pia kwa mambo yanayoendelea kutendeka katika Mkoa wa Kigoma. Tunashukuru sana kwa miradi ya barabara inayoendelea. Kwa hiyo, ninashukuru sana na ninaomba tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mara nyingi hata anapofanya ziara zake mbalimbali anasikiliza matatizo ya watu na kuyapatia majibu pale pale. Mwaka jana alikuja katika Wilaya ya Kasulu, kulikuwa na kilio kikubwa cha muda mrefu wananchi walikuwa wakililia Hifadhi ya Kagera Nkanda akayatolea majibu pale pale. Wananchi wa Wilaya ya Kasulu wanafurahi, sasa hivi wanalima, wanazalisha mahindi na maharage. Kwa hiyo, wanaendelea kumshukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la maji. Nchi yetu imejaaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji ikiwemo bahari, maziwa, mito mikubwa na midogo lakini bado tuna tatizo kubwa la maji. Nilikuwa ninaiomba Serikali kwa kutumia vyanzo hivyo ambavyo tulijaaliwa na Mwenyezi Mungu iweze kuhakikisha maji yanafika vijijini. Wanawake muda mwingi wanatumia nafasi ya kwenda kutafuta maji badala ya kutumia nafasi hiyo katika uzalishaji mali. Kwa hiyo, naomba maji yaweze kufikishwa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kasulu hususan Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Vijijini bado kuna tatizo kubwa la maji na katika Mkoa mzima wa Kigoma bado kuna matatizo ya maji, Kibondo, Kakonko na maeneo mengine yote. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba maji Kigoma yaweze kufika. Katika Wilaya ya Kasulu viko vijiji ambavyo vinapakana kabisa na Mto Malagarasi lakini kwa bahati mbaya vijiji hivyo havina maji. Naomba Kijiji cha Kitanga ambacho kiko mbali kabisa na kinapakana na Mto Malagarasi kiweze kupatiwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kuweza kufanya watoto waende kusoma bila kulipa ada yoyote na tunamshukuru Rais kwa kuja na sera hiyo. Pamoja na hayo bado yapo matatizo madogo madogo, watoto wameenda shule, wamekuwa wengi, vyumba vya madarasa vimekuwa vichache, nyumba za walimu hazitoshi. Kwa hiyo, naomba kwa kusaidiana na wananchi, Serikali iweze kuhakikisha madarasa yanajengwa ili watoto wetu waweze kupata sehemu ya kusomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe ombi hapa, ipo shule moja ambayo kutoka Kasulu Mjini kuelekea katika kijiji hicho ni kilometa zaidi ya 100 na kijiji hicho hakina sekondari ya kata. Ili watoto waweze kupata elimu, wanatembea kilometa 50 kutoka Kitanga kwenda Helushingo kwenda kutafuta elimu ya sekondari. Kwa vile wananchi walishaonesha bidii ya kufyatua tofali na kuanza kujenga, naomba sasa Serikali iangalie ni jinsi gani itawasaidia ili waweze kukamilisha vyumba vya madarasa wanafunzi waweze kupata madarasa ya kusomea na waepukane na safari ndefu ya kwenda kutafuta elimu katika Kata ya Helushingo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze Profesa Ndalichako, amekuwa akifanya ziara nchi nzima na tumeshuhudia ziara zake zimezaa matunda, pale alipopita madarasa yameboreshwa na ninamshukuru hata Kigoma Sekondari imeweza kunufaika na ziara zake, lakini na Chuo cha Ualimu Kasulu nacho kimeweza kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishukuru Mawaziri wote, ziara wanazozifanya kwa kweli, wanakopita huku na kule tunaweza kunufaika. Mwaka jana Mheshimiwa Ummy alizunguka katika Mkoa wa Kigoma tuliweza kunufaika tukapata magari nane kwa ajili ya Wilaya zote za Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, ninaendelea kuwapongeza Mawaziri kwa ziara zao. Bado tunalo tatizo la watumishi katika vituo vya afya, katika zahanati na hata katika hospitali za Wilaya. Kwa mfano katika hospitali ya Wilaya ya Kasulu, wauguzi hawatoshi, waganga hawatoshi. Nurse mmoja anaweza akahudumia wodi moja akiwa yeye peke yake amuwekee mgonjwa maji, ahangaike kwenda kupima temperature, kwa kweli tunaomba Serikali iongeze watumishi katika hospitali ya Wilaya ya Kasulu na hata katika hospitali nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru Wilaya mpya zile za Buhigwe na Kakonko nimeona tulitengewa shilingi milioni 500 katika Wilaya ya Buhigwe zimekwenda na hospitali ninaamini itaanza kujengwa, lakini na Kakonko zilishaanza kupelekwa kidogo kidogo. Ninaomba basi, pesa zilizosalia zipelekwe ili tuweze kupata hospitali katika Wilaya ya Kakonko na Wilaya ya Buhigwe ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Uvinza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wahamiaji haramu na wakimbizi; Mkoa wa Kigoma umapakana na nchi ya Burundi na DRC, kuna wimbi kubwa la wakimbizi wanaoingia wengine kihalali kwa kuletwa kwa sababu wanakuwa wameingia wakati ule wa vita na wengine ambao wanapita njia ya panya, kwa hiyo, Mkoa ule una wakimbizi wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano halisi, Kijiji cha Kitanga wanaingia wakimbizi wengi sana. Kwa mfano, pesa hizi zinazotolewa kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye maisha duni, pesa zinazotolewa na TASAF, wakimbizi ndio wanaonufaika. Nimeshuhudia wakimbizi 70 wakipewa pesa za TASAF wakati wananchi wa Tanzania hawapati pesa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kulalamika kuhusu wakimbizi wanaoingia Kitanga, lakini mpaka sasa hivi bado wakimbizi wanaingia. Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi ninaomba kabisa kule Kitanga mtupie macho kule kwa sababu, wakimbizi wanaingia kwa wingi na ndio hao wanaoendelea kunufaika kwa kupata pesa hizo za TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa naomba niongelee kuhusu uwezeshwaji, jana nimeongea nilipokuwa ninauliza swali la nyongeza. Ninamuomba Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa sababu kule Kigoma tayari kuna vikundi vingi, kuna SACCOS nyingi, ninaomba basi kwa sababu mikoa mingine ilishafikiwa na mifuko ile ya uwezeshaji, naomba safari hii katika bajeti hii Mheshimiwa Jenista Mhagama macho yako uelekeze mkoani Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo ninaomba nishukuru, ahsante sana na ninaunga mkono hoja.