Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi kunipa fursa hii niweze kuchangia hoja yetu ambayo iko mezani. Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi katika Ofisi hiyo, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu wote na watendaji wote wa Wizara hiyo wanavyochapa kazi katika Awamu hii ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii naona imejipambanua sana imeweka kipaumbele katika miradi ya miundombinu; miradi ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, reli, miradi hiyo ya miundombinu. Miradi hii ni miradi ambayo inachochea ukuaji wa uchumi. Kwa hiyo, ninawapongeza na kuwapa moyo muendelee kuwekeza katika miradi hiyo kwa sababu inachochea sana ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendeleze pale ambapo aliishia Mheshimiwa mwenzangu Mheshimiwa Oran Njeza Mbunge wa Mbeya Vijijini. Uwanja wa Songwe sawasawa na Serikali mmekula ng’ombe mzima tunashindwa kumalizia mkia, uwanja umejengwa ni mzuri sana, bado kuweka taa za kuongoza ndege, bado uzio na kumalizia jengo la abiria. Mbeya, Nyanda za Juu kote huko kuna fursa nyingi sana ya mazao. Kuna ndizi, kuna maua, kuna viazi, kuna mpunga anaolima Mheshimiwa Haroon, vyote vinahitaji usafiri wa kwenda nchi za nje.

Kwa hiyo, naomba uwekezaji uliobaki ni mdogo sana, kuweka taa kuweka na uzio na kumalizia uwanja wa ndege ni mdogo mno. Naomba Serikali katika bajeti hii ionyeshe nia ya kwelikweli kwamba inamalizia uwanja wa ndege wa Songwe ili biashara iendelee kama kawaida. Inauma sana pale ambapo ndege inatoka Dar es Salaam inafika Songwe inakuta kuna ukungu inageuza kurudi Dar es Salaam ni hasara kubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali imalizie mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Stiglers Gorge ni mzuri sana utaongeza nguvu kwenye uchumi, utaongeza umeme karibu megawati 2100, lakini mradi huu unategemea maji, maji ya Mto Ruaha, Mto Kilombero, Mto Rufiji, mto huu unakauka. Mto Ruaha, Kilombero, Rufiji inakauka seriously. Ukiuona mto huu ulivyokuwa mwaka 2008 na leo utalia. Mheshimiwa Makamu wa Rais ameenda Iringa kutembelea Bonde la Mto Ruaha akashtuka, ameunda Tume ya kufuatilia mto huo. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili ameenda Kilombero ameona Kilombero, ameona mto unavyokauka na vijito vyake ambavyo vinaingia kwenye mto huo vinakauka naye akaunda tume ya kufuatilia mto huo.

Naomba Wizara zote zinazohusika zikae pamoja ziunganishe vichwa pamoja na Chuo Kikuu cha SUA, tuunganishe vichwa na kuurejesha mto huu uweze kuweze kuleta maji kwenye Bwawa la Stiglers isije ikawa white elephant.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee barabara ya Mbeya - Chunya - Makongorosi. Naishukuru sana Serikali imejenga barabara hiyo imefika Chunya kilometa 72, sasa hivi bei ya usafiri kutoka Mbeya kwenda Chunya ni shilingi 3,500 kama ilivyo kwingine kutoka Mbeya kwenda Tukuyu, na wananchi wangu wanaanza kusafirisha mazao kwa haraka kutoka Chunya kwenda Mbeya. Sasa hivi Serikali inaanza mwaka huu kujenga barabara hiyo kutoka Chunya kwenda Makongorosi, naishukuru sana. Wakati huo huo inaanza kujenga kutoka Mkiwa kwenda Itigi ili tukutane katikati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina ombi; mara nyingi nimeongea hapa kwamba barabara hii ya Mbeya Chunya imekamilika lakini malori yanayobeba mbao yanayobeba tumbaku Chunya - Mbeya yanabeba lumbesa. Wakifika Mbeya ndiyo wanagawa yanakuwa malori mawili, kwa hiyo, barabara inaumia. Hii barabara sasa hivi kwetu sisi ni mboni ya jicho inaumia, naomba Serikali iweke weigh bridge hata mobile weigh bridge tuweze kuilinda barabara hii, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la maji vijijini. Naunga mkono Wabunge wenzangu wengi wameongelea suala hili na wameiomba Serikali kwamba kama Serikali ilifanya vizuri iliunda TANROADS inajenga barabara vizuri, ikaunda REA inaweka umeme vijijini vizuri, imeunda TARURA imeanza kazi vizuri ya kuweka barabara za vijijini na mijini, umefika wakati wa kuweka Wakala wa Maji Vijijini. Naunga mkono sana hoja hiyo.

Pamoja na hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja Chunya alitukuta tuna shida ya maji kwenye Mji wa Chunya akaidhinisha fedha zimetoka na kinajengwa kisima kikubwa sana Chunya na nadhani katika mwezi huu na mwezi ujao kitakamilika, kwa hiyo wananchi wa Chunya kwa asilimia 80 watapata ahueni ya maji. Naomba fedha iliyobaki itolewe kwa muda ili tutatue tatizo la maji kwa wananchi wa Chunya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wananchi wa Mji wa Makongorosi nao wanachimba kisima, kuna wananchi zaidi ya 20,000 wana shida sana ya maji, naomba Serikali nayo ielekeze macho kwa wananchi hawa wa Makongorosi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Bwawa la Matwiga Serikali imetoa fedha nyingi sana kujenga Bwawa la Matwiga. Bwawa hili likikamilika litaweza kuhudumia kata zaidi ya sita, sasa limechimbwa limejaa maji liko tayari, linasubiri miundombinu ya mabomba, matanki ili tuweze kupeleka maji kwenye kata hizo. Naomba Serikali itoe fedha haraka kwenye bajeti hii ili tukamilishe mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chunya ni moja kati ya Wilaya kumi ambazo ziliteuliwa na Serikali kwamba wajenge Vyuo vya VETA. Tukakubali tumetenga eneo lakini mpaka sasa hivi chuo hakijajengwa, naomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu atakapokuja hapa atuambie ni lini watatoa fedha za kuanza kujenga Chuo cha VETA kwa Wilaya ya Chunya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo la mwisho, kuna Watendaji wa Vijiji na wa Kata. Watendaji hawa wamekuwa wana sakata refu sana na Serikali. Serikali ilisema watendaji ambao waliajiriwa wakiwa darasa la saba walidanganya vyeti waliondolewa kuanzia mwaka 2004, lakini wale ambao walioajiriwa kabla ya hapo waliendelea kufanya kazi. Mwaka huu Serikali inawaondoa hawa watendaji kuleta watendaji wengine, inasema walipewa muda wa kujiendeleza hawajafanya. Sasa watendaji hawa ndio wamesaidia kujenga shule za sekondari, wamesaidia kujenga vituo vya afya, wamesaidia kujenga zahanati, walikuwa hawana muda wa kujiendeleza, naiomba sana Serikali hawa watendaji wengi karibu wanaelekea muda wa kustaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba watendaji hawa waachwe wamalizie muda wao wastaafu kwa amani hawakutenda kosa lolote, hawakusema wako form four hapana, waliajiriwa wakiwa darasa la saba.

Kwa hiyo, naomba Serikali iwe na moyo wa huruma, kwenye human face iwaache watendaji hawa wamalizie muda wao wastaafu kwa amani kwa sababu wameifanyia kazi Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.