Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa pongezi kwa Serikali kwa kazi nzuri ambayo wameifanya na wanaendelea kuifanya. Vilevile naomba nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji wa hotuba yake. Watanzania wanaona, Watanzania wana akili, lakini ambacho wenzetu walikuwa wanakililia na ndicho ambacho Mwenyezi Mungu ametujaalia, sisi tunaendelea kumuombea Mheshimiwa Magufuli kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ya kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote ndugu zetu wa upande wa pili walitaka Mheshimiwa Rais ambaye atathubutu, Rais ambaye atakwenda kutenda, kwa hakika Mheshimiwa Magufuli anatenda na sisi Wabunge wake tuko nyuma yake tunawa-support Waheshimiwa Mawaziri wetu kwa kazi nzuri ambayo wanaifabnya ya kuwatumikia Watanzania na hatimaye naamini Watanzania wale wale watakwenda kufanya maamuzi mwaka 2020 kwa kadri wanavyoendelewa kutumikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi naomba nichukue nafasi hii kutoa ushauri; yako baadhi ya maeneo ambayo kwenye bajeti ya mwaka jana nilisimama hapa nilishauri, lakini niishukuru Serikali yangu kwa sababu baadhi ya mambo mengi wameyafanyia kazi na kwa wakulima wetu sisi ambao tunawawakilisha yameanza kuleta tija kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge waliotangulia wa Mikoa ya Lindi na Mtwara wamezungumzia sana masuala ya elimu, kilimo, miundombinu, nishati na maeneo yote yanayohusu huduma za kijamii. Mimi naomba nijielekeze kwenye eneo la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulitoa mapendekezo ya kusaidiwa wakulima wetu kupata pembejeo hasa sulphur bure na Serikali yetu sikivu ilifanya hilo zoezi kwa kutoa sulphur na pembejeo nyingine kwa wakulima wetu. Uzalishaji ulipanda na wakulima wetu wamepata tija kubwa sana kwa zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kutoa hizi sulphur na pembejeo nyingine bure bado yako maeneo ambayo tulifikiri ni muhimu tukaendelea kushauri, tukamshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Wizara ya Kilimo waangalie namna ambavyo wanaweza sasa ku-fast track ili wakulima wa maeneo haya waweze kupata pembejeo kwa haraka iwezekanavyo. Hapa tunapozungumza leo ni mwezi wa nne tayari watu wameshaanza maandalizi ya mikorosho. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana watu wa Wizara ya Kilimo waharakishe upatikanaji wa pembejeo ili wakulima wetu waweze kuhudumia mikorosho yao kwa wakati ili waweze kuendelea kuzalisha na hatimaye tuliingizie taifa letu kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka pia nishauri ni eneo ambalo linahusu malipo. Utaratibu ambao umetumika kwa msimu wa mwaka jana 2017 toka tumeanza utaratibu huu mpya wa stakabadhi ghalani ulioboreshwa bado kuna baadhi ya makampuni ambayo yamekuwa yanachukua korosho za wakulima yameendelea kuchelewesha malipo kwa wakulima wetu. Yako baadhi ya maeneo mpaka sasa hivi baadhi ya makampuni hawajamaliza kulipa fedha za wakulima ambazo zimeshauzwa toka mwaka jana wakati ambapo minada ilishafungwa toka mwezi wa kumi na mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo pamoja na timu yake watie mkono katika kuhakikisha makampuni yote ambayo yalichukua korosho za wakulima wanamalizia kulipa malipo ili wakulima waweze kupata nafasi ya kuhudumia mashamba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nilishauri Serikali yetu ni eneo la ufufuaji wa viwanda. Katika jimbo la Nachingwea tunacho Kiwanda cha Ubanguaji wa Korosho ambacho kwa muda mrefu hakifanyi kazi. Pia kupitia Wizara yetu ya Viwanda ambayo tayari nilishakwenda kufuatilia walitupa maelekezo ya kufufuliwa kwa viwanda vyote ambavyo vilishakufa tangu muda mrefu. Korosho inayozalishwa katika maeneo haya tulipenda sana ipate thamani kubwa zaidi kwa kubanguliwa katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wawekezaji ambao wameingia ubia na baadhi ya vyama vyetu vikuu ikiwemo Lindi Farmers. Hata hivyo bado uwekezaji ambao unaendelea kule haujakaa vizuri, kupitai Wizara ya Viwanda Mheshimiwa Waziri lakini pia watu wa kilimo naomba watie mkono waone wale wawekezaji wa Sunshine ambao wamechukua viwanda vya Nachingwea, Mtama pale pamoja na maeneo mengine ya Newala waweze kuona nini ambacho kinaendelea ili ikiwezekana katika msimu huu wakulima wetu waweze kubangua korosho na kuipandisha thamani ili tuweze kupata pesa kubwa zaidi ya hii ambayo tunaipata sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nilishauri ni eneo la stakabadhi ghalani katika mazao mengine. Tunakwenda kwenye msimu wa kilimo cha ufuta Mkoa wa Lindi tumeadhimia kuingiza ufuta safari hii katika stabadhi ghalani. Niombe Wizara ya Kilimo ione namna inavyoweza kuhamasisha na kuangalia mikoa mingine yote inayolima ufuta ili tutakapoanza kwenda kutekeleza mfumo huu basi ukae katika misingi ambayo itakuwa haitoleta shida na haitopishana kati ya mkoa mmoja na mkoa mwingine; na hii kwa sababu kipindi cha nyuma ufuta umeuzwa kwa kila mkoa kwa utaratibu ambao si ule ambao tumeuzoea wa stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tulishakuja kwako mwaka jana na mwaka huu sisi tumeshapitisha katika vikao vyote tulikuwa tunafikiri ni wakati wenu sasa kama Wizara muone namna ambavyo mtasimamia ili tuhakikishe mfumo huu utakapoanza kwa msimu huu basi uwe ni uniform katika maeneo yote yanayolima ufuta, lengo likiwa ni lilelile kuongeza tija kama ambavyo tunafanya vizuri katika zao la ufuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitajka nilkizungumzie ni eneo la zao la mbaazi. Mwaka jana tumelalamika sana juu ya changamoto za bei kwa zao la mbaazi ambalo wakulima wetu wengi wamechangamkia na kuiona fursa. Mheshimwa Waziri wakati anakuja hapa tulimuomba atupe ufafanuzi, lakini pia atueleze namna ambavyo wale wanunuzi hasa Wahindi ambao waliingia mkataba walivyojipanga kwenda kununua mbaazi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunapata shida kidogo kuwahamasisha wakulima wetu juu la suala la ulimaji wa mbaazi kwa sababu bado hatujawa na uhakika. Kipo kitengo ambacho kinashughulika na utafiti ndani ya Wizara ya kilimo, tunaomba kitengo hiki sasa kitoe maelekezo; kitoe dira lakini pia watupe uhakika wa masoko ili tuweze kupata nguvu ya kuwahamasisha wakulima wetu kama wanaweza wakaendelea kulima mbaazi kama zao la biashara au walime kama zao la chakula kama ambavyo tulikuwa tunafanya kipindi cha nyuma. Jambo hili nafikiri litatusaidia ili kuweza kuondokana na kile ambacho kimejitokeza miaka miwili mfululizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pilli ambalo nilitaka nichangie ni suala zima la miundombinu ya barabara. Hatuwezi kujadili maendeleo hatuwezi kupanga mikakati mizuri kama hatuwezi kuangalia hali ya barabara zetu. Kwa mwaka jana barabara ya Masasi - Nachingwea - Nanganga, tulitengewa shilingi bilioni tatu na milioni mia tano; nimefuatilia sana na ninaendelea kufuatilia sana. Hiki ni kilio cha wanachi wa jimbo la Nachingwea ambao wanapakana na Wilaya ya Masasi, wanapakana na Wilaya ya Ruangwa, Liwale. Barabara hii ni barabara ya kiuchumi; naomba niwaombe watu wa Wizara ya Ujenzi ya waone namna wanavyoweza kwenda kuanza utekelezaji wa ahadi ambayo wamenihaidi kwa miaka miwili sasa mfululizo; kwamba ujenzi utaanza na anatafutwa mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa jimbo la Nachingwea na maeneo yote ya jirani wamenituma na wanaendelea kunisisitiza kuendelea kuiomba Serikali yao sikivu iweze kuanza ujenzi huu kwanza kwa kulipa fidia, lakini pili kwa kuanzisha ujenzi ambao sasa utatusaidia kusafirisha mazao yetu bila matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiondoa barabara hii iko barabara inayotoka Nanganga kwenda Ruangwa kwenda kutokea Nachingwea barabara hii tayari usanifu umeshafanyika tunasubiri ahadi ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa kiwango cha lami. Iko barabara inayotoka Nachingwea kwenda Ruangwa kuunganisha Kiranjeranje; ni barabara ambayo ikifunguliwa nayo itakwenda kufungua uchumi wa Mkoa mzima wa Lindi kwa sababu Wilaya ya Nachingwea na Wilaya za jirani ndizo Wilaya ambazo zinaongoza kwa kusafirisha na kutoa mazao ambayo kimsingi yanaletea faida kubwa sana taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo la nishati. Hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa yetu si mzuri…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzunguzaji)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana kupitia watu wa Wizara mashine walizozileta Lindi waende wakazifunge, muda tuliokaa kusubiri unatosha sana. Tumepewa miezi minne umeme utakwenda kutatuliwa, lakini muda huo ni mwingi tunaomba Wizara wazifunge zile mashine ambazo tayari wameshazileta ili tukae tuwe na umeme wa uhakika ambao utatuwezesha kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru sana na ninaomba nionge mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante.