Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niwe mchangiaji katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai; pili, kwa dhati ya moyo wangu kabisa namshukuru sana Rais wetu wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuleta maendeleo katika Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kazi kubwa anayoifanya na ambayo inaonekana dhahiri ya kuleta maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo inabidi nichangie ni eneo la afya. Kwanza kabisa naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, kwa taarifa sahihi zilizopo ni kwamba Halmashauri yangu ya Nzega DC ni mojawapo ya Halmashauri 67 ambazo zimepewa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga hospitali mpya. Napongeza sana hatua hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ni matumaini yangu, kama ambavyo tumeelezwa kwamba fedha hizi zinakuja na ramani maalum kutoka Wizarani; na kwamba kwa kuzingatia matumizi ya force account katika ujenzi wa miradi sasa hivi, ni matumaini yangu kwamba shilingi 1,500,000,000 zitatosha kabisa kujenga hospitali hii mpya kwa kutumia force account na ramani maalum ambayo imekuwa tested kwenye ngazi ya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo liko dhahiri ambalo ni lazima nipongeze ni hali ya upatikanaji wa dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya. Tunafahamu kwamba Kitaifa Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza bajeti ya dawa kutoka bajeti iliyokuwa awali, mwaka 2015 ambayo ilikuwa around shilingi bilioni 31 kwa mwaka, imeongezwa mpaka shilingi bilioni 269 kwa mwaka. Hili ni ongezeko kubwa sana na kwa Halmashauri yangu ya Nzega DC pekee ongezeko hilo limetoka shilingi milioni 300 kwa mwaka 2015 mpaka shilingi milioni 700 mwaka huu. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 na ushee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni jambo ambalo liko dhahiri sana na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene na Halmashauri ya Nzega DC kwa ujumla, ninapongeza kwa dhati, kwa sababu hali ya upatikanaji wa dawa kwa kweli ime-improve, imeongezeka kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo sasa inabidi lifanyike na huu ni ushauri wangu, baada ya kuhakikisha sasa tunapata dawa za kutosha kwa kuwa na bajeti ya kutosha, jambo kubwa ambalo inabidi lifanyike sasa ni ku-address tatizo la uhaba mkubwa wa waganga na madaktari katika vituo vyetu vya afya, hili bado ni tatizo. Mimi katika kituo changu cha afya cha Itobo na Bukene ambavyo ni vituo ambavyo vimejengwa kwa hadhi ya kisasa, vina vifaa vizuri vya kufanyia upasuaji, lakini katika vituo vyote hivi viwili mganga anayeweza kufanya upasuaji ni mmoja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Itobo kuna mganga mmoja tu anayeweza kufanya upasuaji na hata Kituo cha Afya cha Bukene pia kina mganga mmoja tu anayeweza kufanya upasuaji. Sasa kutokana na workload, idadi ya wagonjwa wanaokuja kupata huduma pale, huyu mganga mmoja kwa kweli ameelemewa, hawezi kutoa huduma stahiki inavyotakiwa.

Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tumeweza ku- address tatizo la access to health services, sasa twende hatua nyingine ya ku-address tatizo la quality (ubora wa huduma za afya) kwa maana ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na Waganga na Madaktari na vifaatiba vya kutosha ili huduma hii muhimu iweze kupatikana kwa wananchi wetu ambao wanaihitaji sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la miradi ya maji. Kwanza nitumie fursa hii, kama Mbunge wa Jimbo la Bukene, lakini Mbunge katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, kuipongeza Serikali kwa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria. Tunafahamu kwamba Serikali imewekeza shilingi bilioni 600 ili kuhakikisha maji yanatoka Kahama na kufika Tabora Mjini. Kutokana na zoezi hilo, sisi watu wa Nzega tunanufaika; tuna vijiji vingi sana ambavyo vitapitiwa na maji na kufanya wananchi wetu wapate maji salama ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya mradi huo mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, Serikali kwa kutumia Mfuko wa Maji wa WSDP (Water Sector Development Programme) imetupatia shilingi bilioni tatu kwa ajili ya miradi ya bomba yanayotokana na visima virefu. Katika Jimbo langu la Bukene pekee tunakwenda kupata visima virefu katika Vijiji vya Mambali, Lugulu Lwanzungu, Luhumbo, Bukene yenyewe, Kabanga, Itunda, Kasela, Isagehe, Ilagaja, Lyamalagwa, Mwamala na Kayombo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni vijiji 12 ambavyo shilingi bilioni tatu itatumika kutafuta maji chini ya ardhi na kujenga miradi mikubwa ya kusambaza maji ya bomba. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo liko wazi. Kama mwakilishi wa wananchi, naipongeza Serikali kwa juhudi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kuwe na flexibility katika matumizi ya fedha hizi, kwa sababu eneo letu la Nzega na Mkoa mzima wa Tabora kuna tatizo la kupata maji chini ya ardhi. Sasa hivi mkandarasi yuko site, lakini visima vingi anavyochimba anakwenda mpaka mita 150, 200, lakini anakosa maji. Kwa hiyo, kuwe na flexibility kwamba endapo tutakosa maji chini ya ardhi, fedha hizi ziruhusiwe kutumika katika vyanzo vingine ambavyo siyo lazima iwe chini ya ardhi, kuna vyanzo vya mabwawa, kuna vyanzo kwa mfano maji ya Ziwa Victoria yakifika Nzega yenyewe pia yatakuwa chanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, fedha hizi zitumike kwenye usambazaji kwa sababu kuna uwezekano tukakosa kupata maji chini ya ardhi kwa visima vyote ambavyo tumepanga kupata. Kwa hiyo, ushauri wangu hapa ni flexibility ya matumizi ya fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni la barabara; ninafahamu kwamba sasa hivi mkandarasi yuko site kwa maana ya kufanya upembuzi wa kina kwa barabara ya kilometa 189 ambayo inatoka Tabora kupitia Mambali – Bukene – Itobo – Mwamala – Kagongwa na hatimaye kuunganisha na Mkoa wa Shinyanga. Hii ni barabara muhimu sana kwa sababu itaunganisha Mikoa ya Tabora na Shinyanga kwa kupitia maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa sana wa mpunga, alizeti na mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba Serikali ifanye usimamizi wa karibu sana kwa huyu Mkandarasi anayefanya usanifu wa kina, kwa sababu mkataba unasema, anapaswa kukabidhi kazi hii mwisho wa mwezi wa Kumi na Mbili mwaka huu. Kwa mujibu wa makubaliano ya awali ni kwamba barabara hii katika Miji ya Bukene na Itobo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.