Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Kwanza kabisa naipongeza sana hotuba ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri iliyofanyika. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuwafanyia Watanzania. Hata ukiangalia michango ya Wapinzani, imebaki mambo machache ambayo naamini baada ya bajeti hii, watakaa sawa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishasema humu ndani kwamba mimi ni darasa la saba; na humu ndani tuna matabaka tofauti, inawezekana ni vizuri zaidi kila mtu akatetea wenzie. Nampongeza Mheshimiwa Rais alipoenda pale bandarini akiwa anazungumza na watumishi wa Bandari kuhusiana na suala la vyeti fake na wale walio-forge kutoka darasa la Saba kuwa na vyeti vya form four, alitamka waziwazi mchana kwamba wale wote walio-forge vyeti kutoka darasa la saba kwenda form fourwafukuzwe kazi, lakini wale walio na vyeti vyao vya darasa la saba na kazi wanazozifanya wanafanya vizuri, waendelee na kazi, kila mtu alisikia na suala hili lilisemekana lilizungumzwa mchana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa humu ndani kuna wasomi wengi, lakini pia kuna wa darasa la saba wengi na huko nje hata ninyi wenye degree humu ndani, kuna ndugu zenu wa darasa la saba ambao walikuwa wameajiriwa hizo ajira ndogo ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri sana Serikali yangu, ninashangaa ni kwa nini wamewafukuza Watendaji wa Vijiji wa darasa la saba. Wanataka hizi nafasi za darasa la saba, hizi za utendaji wapewe watu waliotoka Vyuo Vikuu. Ni wapi? Ni Wilaya gani? Ni Kijiji gani ambako mmepeleka Mtendaji graduate akaweza kufanya kazi akawazidi darasa la saba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefukuza madereva, hivi niwaulize ndugu zangu Waheshimiwa Mawaziri, wewe unasomesha mtoto wako English Medium kwa hela nyingi anaenda sekondari, form six, Chuo Kikuu, akitoka Chuo Kikuu tena akawe dereva? Hivi tunafanya mambo gani ya ajabu? Ninaomba sana Serikali yangu tena na Wabunge wenzangu wa CCM tuitake Serikali itoe tamko la kuwarudisha watendaji hawa kwenye kazi, siyo kuwalipa. Haiwezekani mtu amefanya kazi toka mwaka 2004, unakuja kumfukuza leo. Hatuzungumzi suala la kulipwa mafao, warudishwe kazini watoke kwa muda wao wa kustaafu na hili limefanyika hata kwenye Majeshi. Kwenye majeshi enzi hizo, watu walikuwa wanachukuliwa darasa la saba, leo wengine ni Mameja, wengine ni ma-OCD, wameachwa mpaka wastaafu. Iweje Watendaji tunawafukuza? Mtu amebakiza miaka miwili, unamfukuza! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe Serikali iwarudishe. Kama Serikali itakaidi, mimi nataka niwape ushauri, kwa sababu humu ndani kuna Wabunge kama sikosei 100 na zaidi wa darasa la saba, siyo la saba tu, hata form four failure wamo, vyuo vikuu wenye vyeti havieleweki wamo humu ndani. Ninaomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi mnisikilize vizuri, ni kwamba kama hamwezi kuwarudisha hawa Watendaji na sisi Wabunge wa darasa la saba humu ndani mtufukuze. Halafu siyo kwamba mtufukuze, kwa sababu ukiangalia…
T A A R I F A . . .
MHE. JOSEPH K MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kama ni taarifa, lakini record yako inajulikana Chuo Kikuu ulikuwa na kazi gani. Sasa unaweza ukawa ni wewe mmoja wao. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni hata sababu ya Wabunge wa darasa la saba kuwa humu ndani na wale wenye vyeti ambavyo nimevitaja, ni bora katiba ikatuondoa humu ndani. Mkituondoa, mturudishe kwa Viti Maalum kama makundi mengine yaliyoko humu ndani, kwa sababu na sisi tuko wengi wa darasa la saba. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuangalia, hebu naomba uangalie tu ukurasa wa 49, kipengele cha elimu ukisoma namba 80 pale waliodahiliwa kuingia darasa la kwanza walikuwa milioni mbili, waliodahiliwa kutoka darasa la saba kwenda form one mpaka form four ni 500,000. Kwa hiyo, darasa la saba tena wamekuwa wengi kuliko walioenda sekondari. Ukiisoma hii taarifa, haikufafanua kutoka kwenye 500,000 kwenda chuo kikuu utakuta kuna 100,000. Kwa hiyo, ukipiga hesabu ya kawaida, sisi tuko asilimia 85. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ukiangalia walipakodi wakubwa Tanzania na Mheshimiwa Mipango na Waziri wa Viwanda yuko hapa, wajasiliamali wanaolipa kodi kubwa na wenye viwanda vingi ni darasa la saba. Hebu asimame hapa anitajie mtu mwenye kiwanda anayelipa kodi Serikali mwenye chuo kikuu hapa. Wote tumewaajiri, halafu sisi tunakuja tunatozwa kodi, tunaonekana hatufai hata kwenye kazi zinazolingana na elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, kama tunaondolewa kwenye Katiba, nasi tuwekwe kwenye kundi la Viti Maalum kama wanawake na walemavu, nasi tuwakilishe, twende hivyo hivyo na kwenye Baraza la Mawaziri. Kwa sababu tunakosa wawakilishi kwenye Baraza lenu ndiyo maana mnataka kuwatoa hawa watu.
Naiomba sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa hili Waheshimiwa Wabunge tuungane kwa pamoja, ondoeni hata uvyama kwa sababu hawa darasa la saba mna shangazi na wajomba zenu waliofukuzwa, mkijipigia makofi wenye Chuo Kikuu wachache tutakutana 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nizungumze suala la uvuvi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, suala hili hiyo operation nilizungumza kipindi kilichopita, operation ina maana nzuri na hakuna mtu anayekaa kwenye Kanda ya Ziwa aneyeshabikia uvuvi haramu. Ila uendeshwaji wa zoezi haukufuata haki. Tunazo mpaka risiti za watu wa Wizara, mtu ametozwa shilingi milioni 20 halafu risiti ikaandika 2,015, tunazo. Kwa nini mnakuwa wagumu kuunda Tume ya kuwachunguza hawa watu. Kuna Bray sijui kuna Sokomba huko Wakurugenzi, ni miradi wametoa watu wao Dar es Salaam kuwapeleka kule, wanachukua hela za watu wetu. (Makof)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri iundwe Tume ikachunguze zoezi hili. Nataka nikwambie kwamba ujasiriamali anaohamasisha Mheshimiwa Rais, sisi darasa la saba tunaupokea kwa hali na mali. Kuna watu leo wako Sirari pale, wamepewa vibali vya Serikali na Wizara ya kuleta mitego; mtu amepewa kibali mwezi wa Tano, mwezi wa nane, akaanza process za mkopo, akapata hela mwezi wa kumi na moja, akapeleka order. Amerudi hapa mwezi wa kwanza. Serikali imekagua ikasema iko sawa, Wizara ya Uvuvi, TBS sawa; kodi ikalipwa, kesho yake Mheshimiwa Waziri Mpina amesema mitego isitoke. Nimefuta vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mtu mpaka leo anaendelea kutozwa storage ya pale Sirari. Hakuna huruma, halafu mnahamasisha watu wafanye kazi. Ndugu zangu naomba sana, Mheshimiwa Waziri hebu unda Tume ichunguze suala hili la uvuvi. Kiukweli sisi watu tunaotoka maeneo ya uvuvi, mnatupa wakati mgumu sana kuzungumza na watu wetu. Hamfanyi haki. Naombeni sana iundwe Tume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nilikuwa naomba kuishauri Serikali, katika uchumi wa Mheshimiwa Dkt. Magufuli anataka tujitegemee sisi wenyewe kwa kulipa kodi, tuachane na wahisani, lakini hizi sheria ambazo tunazitumia, ni za Kiingereza ambazo zinataka sisi tuendelee kuwa Watumwa wa Wazungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano, kuna sababu gani kijiji ambacho kama Mjumbe mmoja aliyechangia kwamba watoto wa shule wanatembea kilometa 11, wananchi wamehamasishana, wamejenga madarasa mawili, matatu wakajenga Ofisi ya Mwalimu, wakajenga choo kizuri na mazingira mazuri. Wizara inakataa kufungua, inasema mpaka tufikishe madarasa saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule inaanzaga na darasa la kwanza, siyo darasa la saba. Ziliwekwa zile sheria ili tuendelee kukopa, tukamilishe kila kitu, tutaanza vipi? Umejenga madarasa mawili, unaanza na darasa la kwanza, mengine yatajikuta shule imefunguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo, kuna sheria ambayo imewekwa inasema Kituo cha Afya hakiwezi kuwa Hospitali ya Wilaya. Ni hizo hizo sheria za kuendelea kufanya sisi watumwa tukakope hela kwa Wazungu. Kama tunatumia hizi hizi hela zetu za kupeana shilingi 200/shilingi 300/=, mimi Kituo changu cha Afya kinapungukiwa majengo mawili, kwanini ile shilingi 200 isiki-top kile Kituo halafu kikawa Hospitali ya Wilaya? Tunadanganyana hiki kitakuwa Kituo cha Afya halafu hapo hapo tutajenga Hospitali ya Wilaya, ambapo unaniletea shilingi milioni 500. Miaka 20 mimi nimeshakufa, Ubunge simo, nani anapata hiyo faida?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali na Wawaziri mfikirie upya kuangalia hizi sheria za kuendelea kutufanya sisi tuwe tegemezi. Kama tunajitegemea wenyewe, turudi kwenye kile ambacho tunaweza kukifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Wizara ya Viwanda, Mheshimiwa Waziri Mwijage naomba sana kwa ushauri wangu hata nchi za China tunaenda kule, hawakuzingatia sana mambo ya viwango ndiyo maana wamefika hapa, ndiyo maana ukienda leo utapata shati la Tanzania, utapata shati la Marekani bei inakuwa tofauti. Sasa kuna kitu mnasema gauge 32, gauge 34, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri tuachie hata gauge 38 hata 40 kulingana na umaskini wa Watanzania watu wetu Wasukuma wanataka wauze mahindi anunue bati aezeke nyumba, wewe uking’ang’ana na hiyo size yako ya gauge 30 mbona kwenye Matembe na majani huendi kuzuia?(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.