Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza sina budi kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri iliyotoa matumaini na iliyomfanya kila Mtanzania aende kifua mbele kutokana na hotuba ilivyopangika. Hata wasomi kwenye redio, kwenye mitandao, kwenye television wanaizungumza speech yake jinsi ilivyokuwa zaidi ya kusomeka imetekelezeka na bado inaendelea kupendwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitazungumzia zaidi tena kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ujio wake Zanzibar wakati ule wa Sherehe za Mapinduzi na alipangiwa kwenye ratiba kwenye mabanda ya maonyesho pale Maisara, watu walifurahi jinsi alivyohudhuria na jinsi alivyotekeleza wajibu wale aliopangiwa. Zaidi ningependa kumuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Waziri wa Muungano na Zanzibar ni sehemu ya Muungano ningependa apange ziara yake kama Waziri Mkuu aje Zanzibar kuimarisha Muungano. Taasisi za Muungano Zanzibar zipo, wafanyakazi wa Muungano Zanzibar wapo kama anavyofanya huku Bara akazitembelea taasisi, akanong’ona na Watanzania waliokuwepo huku, basi tunaomba na Zanzibar afanye ziara kama hiyo. Tunampenda na tunamuomba aje Zanzibar.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza katika ukurasa wa 12 ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu amezengumza kuhusu mafanikio ya Watanzania na takwimu siyo mbaya katika ajira, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu ningesema ajira kweli zinafanywa na zinatekelezwa vizuri, lakini kuna ajira nyingine tunaziacha. Kwa mfano, Mabalozi wetu wako nje tumewapa kazi wanashughulikia diplomasia ya uchumi lakini Watanzania wako wenye Masters, wako waliokuwa na degree, wana Ph.D wamebobea kiswahili, kiswahili sasa hivi kina mantiki kubwa nje ya Tanzania. Watu wengi wanazungumza kiswahili na kinataka walimu wa kiswahili na Tanzania tunao walimu, sasa ajira ni hizi tunaziacha.

Baadhi ya walimu wetu tuwapeleke, tuwaambie Mabalozi watafute hizi ajira kwa upande wa nchi walizokuwepo baadae walimu waende wakasomeshe, ajira itapatikana na Kiswahili kitazidi kuendelea katika kila nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu kazungumzia kwamba tayari tumeshahamia Dodoma, baadhi ya wafanyakazi, baadhi ya taasisi na alifika hadi akasema wafanyakazi 3,829 wamehamia kwa awamu na bado wataendelea na ataimarisha miundombinu. Miundombinu aliyokusudia ni miundombinu mikubwa lakini ya ndani hapa Dodoma tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda barabara ya Sengia, Site Two kule, nenda maeneo ya Area D karibu mtasikia kumetokea ajali maana mashimo yaliyopo ni makubwa, kila mmoja anabidi ayakwepe, huku bajaji, huku pikipiki, huku gari sasa kila mmoja anakimbia shimo anamfuata mwenzie. Sasa kama kweli amekusudia tuiimarishe Dodoma iwe nzuri basi na barabara za ndani pia zitengenezwe ili tuweze kujisikia walipa kodi kwamba tayari Dodoma iko ya kileo na ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu sekta ya uzalishaji ambayo iko ukurasa wa 27. Nakubaliana na maelezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini unapotaka kuzalisha kufungua viwanda ujitahidi kuwa na malighafi na malighafi zetu nyingi ni kilimo.

Sasa tuwahamasishe watu wetu kulima ili waweze kupata malighafi kama ni pamba, kama ni nyanya ama kitu chochote ili wakati tukiwa tunafanyakazi zetu za viwanda tutakapotoa mazao yetu yawe bei rahisi. Ikiwa malighafi tutanunua, tunaimarisha viwanda, itabidi mazao yatakayotoka yawe ghali, sasa lazima tutoe elimu kwa wakulima wetu, tutoe elimu kwa watu wetu wenye viwanda tuwaambie kwamba lazima tutekeleze wajibu wetu ili malighafi iweze kupatikana na tuweze kujitosheleza na kazi zetu ziwe kuimarika kwa mujibu wa shughuli zetu za viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi pia nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama alipofanya ziara yake Zanzibar, akatembelea Mikoa ya Zanzibar kuangalia mambo ya TASAF, kwa kweli ameimarisha Muungano, watu waliridhika na akaona kuanzia awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu vipi inavyokwenda na vipi Zanzibar imejikita katika kupokea mradi huu wa TASAF.

Sasa na yeye pia namwomba kuja kule Zanzibar isiwe ni mara yake ya kwanza tu, aendelee kuja kwa sababu miradi ya Muungano ipo ambayo inamhusu aje kuingalia na Wabunge wenzie tutakuwa pamoja bega kwa bega kuwa nae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja.