Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Malindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Nimejipanga kuchangia katika eneo moja tu, lakini kumetokezea kitu ambacho itabidi nikiseme ambacho kimetokezea jana usiku na ambacho kinahusiana na hali ya usalama na utata utata na matatizo haya ya kukamatana kamatana bila ya kujitambulisha wanaokamata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana usiku huko Pemba Wete wamekamatwa vijana sita Sued Nassoro, Khamis Abdallah, Abdallah Chumu, Juma Kombo, Said Shomari na Uledi Khamisi, wamechukuliwa na watu ambao wamekataa kujitambulisha lakini wananchi kwa bahati waliziona nambari zao za gari wakachukua na leo asubuhi tulipoanza kuulizia RPC wa Kaskazini na Kusini wote wanasema hawako mikononi mwao. Kwa hivyo, wamekamatwa na watu wasioeleweka, tunaongezea ule msamiati wa watu wasiojulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu hasa mimi nitabakia katika sukari. Nataka kutazama sukari bigger picture. Sukari kwa maana ya kwamba ni kilio cha Wazanzibari, ni mkusanyiko wa vilio vingi kinaji-manifest katika sukari; kwa maana kwamba kutokana na matatizo, mivutano ya kisiasa au sekeseke la kisiasa ambalo tumekuwa tukiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu pia kumekuwa na tatizo la kiuchumi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar au wafanyabiashara wa Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wa Zanzibar wanafikiri kwamba hii ina ukandamizaji, ina unyanyasaji, ina kuipendelea Bara zaidi kuliko Zanzibar lakini pia inaleta sintofahamu ambayo watu wengi wanafikiri inafanywa makusudi ili kuitia Zanzibar kitanzi cha uchumi. Kwa sababu yapo mambo mengine hayana logic lakini yamekuwa yakitokezea, na watu wanauliza au kwa sababu sisi ni Visiwa. Kwa sababu yako mambo mpaka tunafika tunajiuliza au sisi ni visiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi imekuja hii zana ambayo inaelezwa hapa ya kutojitosheleza; kwamba ikiwa wewe hujitoshelezi katika bidhaa usiuze kwingine, bila kujali uhuru wa soko, bila kujali upana wa soko. Sasa nafikiri hii ni principle mbaya haifai kuendelezwa na inapaswa ikomeshwe mara moja. Maana yake nini, maana yake ni kwamba kama leo unawaambia Wazanzibari hawawezi kuuza sukari kwa sababu mahitaji yao ni tani 17,000 wanazalisha tani 8,000 maana yake kesho utawazuia wasiuze viazi, kesho kutwa utawazuia wasiuze nguo, kesho kutwa utawazuia wasiuze kingine kwa sababu tu mahitaji yao ya ndani hayajajitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hii ni principle mbaya sana, tunakwenda katika hatua isiyokuwa na msingi kabisa. Tunafanya protectionism ya viwanda au kiwanda cha sukari dhidi ya ndugu yako au kwa sababu sisi ni Kisiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana inayoenezwa ni kwamba pengine Wazanzibari watapenyeza sukari kutoka nje. Kwani hivi sasa sukari haiingii kutoka Malawi, kwani hivi sasa sukari haiingii kutoka kwingine inayoingia kwenye soko la Tanzania ambalo lina starve? Soko la Tanzania hivi sasa linahitaji tani laki tatu na hamsini kwa mwaka. Kila mtu anajua uzalishaji una upungufu wa tani laki moja nzima, sukari inatoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sukari ikipitia Zanzibar, hata ikiwa inatoka nje inapita Zanzibar inakuja katika soko la Muungano, kwa nini iwe vibaya kwamba inatoka Zanzibar wakati pia soko la Muungano linaagiza sukari kutoka nje ili kujaza lile pengo? Au kwa sababu sisi ni Kisiwa kwa maana nyingine tunahukumiwa kwa vitu ambavyo kwa kusema kweli vinatuumiza sana moyoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatukuungana kwa ajili ya kugawana umaskini tu, tumeungana katika kugawana pia na neema. Sasa kama tunazuiana tusigawane neema, mtu anajiuliza Muungano huu una faida gani kwa Wazanzibari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ulikuwa unatarajia nini kuungana na Zanzibar ambayo ina eneo la kilomita elfu mbili za mraba vis-a-vis nchi ambayo ina kilomita elfu tisa za mraba? Ulitarajia nini unaungana na Zanzibar ambayo watu wake sasa hivi ni milioni moja na laki tano vis
-a-vis milioni hamsini na tano? Ulitarajia nini kuungana na Zanzibar ambapo upande mmoja una soko kubwa na upande mmoja una soko ndogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulitarajia Zanzibar a-survive vipi kibiashara? Ulimfikiria Zanzibar afanye nini aingie katika soko? Kama unazuia Zanzibar asiingie kwenye soko la Tanzania Bara ina maana unamzuia Zanzibar asiingie kwenye soko la Afrika Mashariki. Otherwise tunaingia katika matatizo ambayo kusema kweli kama hatukuyapatia suluhu basi utakuwa mgogoro mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Zanzibar tulizuiliwa Zantel isiingie Tanzania Bara kwa muda wa miaka mitano. That was the first mobile company, the biggest, ikafa. Kwa maana sasa hivi ipo taabani imeshanunuliwa na Tigo. Hata hivyo, hivi sasa bidhaa nyingine zinazuiliwa, kwa mfano ukitoka Zanzibar kuna maji ya drop yanazuiliwa kuja huku. Kwa muda mrefu maziwa ya Bakhresa yalizuiwa kuja Tanzania Bara. Kuna njia inaonekana kuna watu wanafanya makusudi ili kui-starve Zanzibar kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nauliza hivi hatujui kwamba Zanzibar kwa udogo wake inahitaji ipate mahali ipate soko? Itafika lini Zanzibar kwa udogo wake itengeneze magari ya kujitosheleza halafu iuze nje, itengeneze TV za kutosheleza halafu iuze nje? Let use our brain.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wawili watatu hapa, mmojawapo Mheshimiwa Kitwanga jana na leo amekuja na fikra mpya, tufikiri upya, tusifikiri kizamani, tufikiri kisasa, kwa sababu kama hatujatengeneza mazingira ya Zanzibar kusonga kiuchumi unatengeneza bomu lingine. Bomu ambalo likilipuka linaweza kuwa kubwa zaidi kuliko bomu hili la kisiasa ambapo pengine watu wakipewa vyeo wananyamaza, watu wakibebelezwa wananyamaza lakini watu wakiwa na njaa watashindwa kunyamaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa biashara nyingi Zanzibar zimefungwa kwa sababu ya hii double taxation ambayo mara nyingi inatokezea ikija huku. Imesemwa, imesemwa, imesemwa, lakini mpaka hivi leo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri ikiwa kwamba tumeungana sisi kwa mambo matatu ambayo yote nafikiri yana shaka katika Muungano huu; la kwanza tumeungana kama vile tunatafutana. Kuna habari nyingi mara nyingi zinazungumzwa kuwa Zanzibar ni kichocho. Hivi kichochoro Zanzibar tu, hakuna mipaka ya Sirari, hakuna mipaka ya Horohoro, hakuna mipaka mingine yote ya Tanzania? Hivi bidhaa zinazopitishwa Zanzibar kuja huku ndiyo ukikusanya zote pamoja itakuwa ndiyo zinapita zile ambazo zinapita katika mipaka yote ya Tanzania? Hilo moja, lakini la pili kwani… (Makofi)
TAARIFA . . .
MHE. ALLY SALEH ALLY: Nafirikiri It is very dismissible amechukua very minor issue, mimi ninazungumzia sukari katika picha kubwa, lakini Waziri anajikita katika swali moja ambalo kwa miaka hamsini ya Muungano halijapatiwa suluhu. Ikiwa mpaka leo Mawaziri wanazungumza miaka hamsini na tano baada ya Muungano kwa maana gani? Bora Waziri angekaa tu akasubiri wakati wako ajibu kwa sababu hapo hajajibu kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, nafikiri lazima tuwe na mfano wa kuonesha kama uchumi wa Zanzibar haukuwa supported kama vile kwa mfano EU walipoungana na nchi maskini Portigual na Spain walitengeneza mpango maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niulize leo hii hapa Serikali ya Muungano imetengeneza mazingira gani ya kiuchumi ya Zanzibar? Mtu ataniambia Zanzibar kuna Serikali yake. Serikali gani ambayo haina taratibu za kupata mikopo, lazima ipite kwenye Serikali ya Muungano, Serikali gani ambayo sera zake kuu zinafuata sera za nchi, kama ni sera za kifedha, kama ni sera nyinginezo? Kwa hivyo nyingine si kweli kwamba Serikali ya Muungano imeleta tatizo hili, tatizo hili lipo mpaka leo kila siku linaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tukubali tu kwamba Zanzibar ina potential…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)