Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namwangalia kidogo mwenzangu mmoja Mheshimiwa mmoja hapo nje alikuwa ananiita anasema ninyi CCM mmekuwa timu pongezi kazi yenu kupongeza tu. Sasa nikamwambia mimi kwa upande wangu Tabora au Tabora Mjini nina mambo mengi tu ya kuipongeza Serikali. Kwa hiyo hata kama anaita timu pongezi tutaendelea kuwa tunatoa pongezi kwa yale mambo mazuri ambayo yanafanywa chini ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Tabora tumebahatika tuna mradi mkubwa wa maji wa zaidi ya bilioni 600 ambao sasa unaendelea; Kiwanja chetu cha ndege kinaboreshwa; alisimama Mheshimiwa Ntimizi hapa aliongelea kile kipande Chaya ambacho kimebaki katika barabara ya kuunganisha kuanzia Itigi mpaka Tabora kwa lami, Mkandarasi yuko anaendelea na kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo sisi Tabora zao la tumbaku kama ambavyo wamekuwa wakiongea wenzangu ni zao la kimkakati. Tulikuwa na matatizo sana ya tumbaku kununuliwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshakuja Tabora mara nyingi na matunda yake yanaonekana, tumbaku nyingi imekwishanunuliwa, kwa hiyo naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo inatimiza ahadi zake. (Makofi)

Mheshiimiwa Mwenyekiti, tunazo changamoto kwenye suala la afya. Kwenye suala la afya sisi pale Tabora Hospitali yetu ya Rufaa ya Kitete, Madaktari Bingwa yupo mmoja tu mpaka sasa hivi na tunahitaji Madaktari Bingwa tisa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kutupatia Madaktari Bingwa ili hospitali ile iweze kuwa inajitosheleza kwa ajili wagonjwa ambao wanakwenda rufaa Bugando, Muhimbili na sehemu zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tangazo pia lilitolewa Bungeni hapa kuhusu madawa au maduka ya madawa ambayo yanazunguka hospitali zetu na kwamba yangefuatiliwa na pengine kuondolewa kabisa. Kwa mfano pale Tabora Hospitali ya Kitete, imezungukwa na maduka ya dawa ambayo yenyewe dawa karibu zote unapata na imekuwa ni kawaida hata dawa ambazo ni za kawaida wagonjwa wamekuwa hawazipati kwenye hospitali, lakini wanapokwenda pale nje wanapata dawa zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunajiuliza zile dawa je zinatoka mle ndani au namna gani kwa sababu wale wanao miliki zile dawa au yale maduka ya dawa wengine ni wauguzi na wengine ni madaktari. Sasa naiomba Serikali lile tamko la kufuatilia ule mlundikano wa haya maduka ya dawa yanayozunguka hospitali zetu wafuatilie isije ikawa ndicho chanzo cha dawa kupotea kutoka mahospitali yetu na kupelekwa kwenye pharmacy ambazo zipo jirani na hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la pembejeo. Tabora wengi ni wakulima kama ilivyo sehemu nyingine, lakini mara nyingi pembejeo haziendi kwa wakati. Kwa mfano, mwaka jana wakulima walipata mbolea katika kipindi ambacho ilikuwa sasa na mazao yameshakuwa kiasi ambacho mengine yalishakuwa yameharibika na hata ilipokuwa imekuja mbolea haikuwa na faida kwa wakulima wengi. Kwa hiyo, naiomba Serikali yetu sikivu kuangalia suala hili la pembejeo za kilimo, ziwe zinawafikia wakulima kwa wakati unaostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la migogoro ya ardhi. Migogoro ya ardhi imekuwa ni changamoto nadhani kwa nchi nzima katika sehemu mbalimbali. Hata hivyo, kwa Tabora kwa sababu ilisemekana au ile Tume ambayo ilipita kwa ajili ya kuchunguza migogoro ile bado hatujapata jibu la migogoro ya ardhi hasa kwa Tabora Mjini. Tabora Mjini imezungukwa na Kambi za Jeshi na migogoro mingi ni kati ya wananchi na jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi iliahidi kwamba itaongea na Wizara ya Ulinzi ili kuangalia ni nani hasa alivamia eneo la mwenzake; kwa sababu wananchi wanadai kwa muda mrefu kwamba maeneo hayo ni ya kwao miaka na miaka na Jeshi la Wananchi wanasema kwamba maeneo yale ni yao. Sasa kwa sababu Serikali ilishaamua muda kwamba itangalia upya ramani, haijajibiwa mpaka sasa hivi na mgogoro ule bado unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naihimiza Serikali kwamba ili kuondoa matatizo ambayo sasa yamekuwa sugu kwenye kata mbalimbali za Jimbo la Tabora Mjini na maeneo mengine, basi wawahishe ule mchakato wa kuangalia upya ramani ili waweze kuweka alama ambazo zitaepusha migogoro ambayo si ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria. Tulifanya ziara juzi juzi katika Mkoa wa Shinyanga, tulikwenda Mikoa ya Simiyu, Geita na tulikutana na changamoto nyingi. Ukiangalia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 62 kuna suala la kesi karibu asilimia 96.3 ambazo zimekwisha, kwa maana kwamba mashauri yake yalishamalizika, lakini uwiano huu ni kwa nchi nzima. Sasa kama ni uwiano kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ni uwiano kwa nchi nzima kuna sehemu zingine ambazo bado kuna mlundikano wa kesi kutokana na uhaba wa Majaji pia na Mahakimu wa kawaida. Kwa mfano sehemu hizi nilizozitaja; ukichukulia Shinyanga Mjini wanatakiwa Majaji sita lakini kuna Majaji wawili tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Simiyu yuko Hakimu mmoja ambaye anashindwa kuzimudu kesi zote kwa sababu kuna upungufu mkubwa wa Mahakimu. Sasa kesi nyingi zinarundikana kwa sababu ya upungufu wa Mahakimu na Majaji pia. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kufuatilia hiyo ili hii figure iliyotolewa hapa ya asilimia 96.3 iendane na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna suala la wenzetu hawa ambao wana matatizo ya uathirika wa UKIMWI kama alivyozungumza mwenzangu mmoja hapa. Nadhani tuwape upendeleo katika pato letu lile la ndani angalau asilimia moja kwenye zile percentage ambazo ni own source katika halmashauri waweze kuchangiwa hawa wenzetu ili kuwawezesha kumudu maisha; kwa sababu wako waathirika ambao kwa kweli bila kusaidiwa hawawezi kujisaidia wenyewe. Nina imani Serikali yangu ni sikivu inaweza ikaliangalia hilo na ikalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana.