Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi nami niweze kuchangia Hotuba aliyoiwasilisha Waziri Mkuu. Aliiwasilisha kwa umahiri mkubwa, hatuna budi kuiunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa anazozifanya akishirikiana na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Serikali. Kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu sisi wote tunaiona. Tunaiona kwa macho, tunaiona kwa vitendo na ushahidi wake upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kauli mbiu imezaa matunda kwa kuleta Bomba la Mafuta kutoka Hoima kwenda Tanga ambako ni kwetu, lazima nitaje Korogwe kwa sababu ni kwetu. Tumeona hizo juhudi za reli ya standard gauge, tunaona hizo juhudi za ununuzi wa ndege tatu ambazo wengine wanabeza, wanabeza halafu baadaye wanapanda. Tumeona juhudi za upelekaji wa umeme wa REA vijijini, tumeona juhudi za ujenzi wa viwanda, tunaona juhudi vile vile za ujenzi wa ukuta wa Mererani ambao Mheshimiwa Rais leo ameenda kuufungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi zote hizi zinafanywa na viongozi wetu ambao tumewachagua kutoka 2015 hadi 2020, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa ule wa 10 ameeleza ni namna gani Serikali inavyosimamia uhuru wa wananchi kujiunga katika vyama wanavyovitaka. Sasa nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kusimamia hayo hadi Chama cha Mapinduzi kimeweza kushinda Kata 58, kimeshinda Majimbo matano, haki ya Mungu hiki chama dume, hapana chezea CCM, kabisa hao wengine wajikaze. Pamoja na hayo naomba niendelee kuipongeza Serikali yangu na nitaipongeza sana, mtalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali pale kwangu Korogwe kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Korogwe imeniwezesha kunijengea Stendi ya kisasa kwa gharama ya bilioni nne. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuja kuifungua ile stendi anasema haipo stendi kama ile ya Korogwe, naishukuru sana Serikali. Hata hivyo, tunajengewa Soko la Kimataifa kwa gharama ya bilioni moja point mbili, hivi kwa nini nisiipongeze Serikali? Hilo nalo ni dogo? Lazima niipongeze Serikali kwa kazi ambayo inaifanya. Piga makofi kabisa ndugu yangu wa CHADEMA huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Maji. Tuna mradi wa maji ambao umeanza, unafanya kazi, kwa maana ya Msambiazi; tulitengewa milioni mia sita na saba, mkandarasi yuko kazini, mradi ule umekamilika asilimia 96. Tuna mradi wa Lwengela Relini na Darajani tulitengewa milioni mia tano na nane, mradi ule mkandarasi yuko kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tatizo kubwa la maji pale Korogwe Mjini Waziri wa Maji alitembelea Wilaya ya Korogwe akaamua kwamba tuachane na kuchimba visima tutumie ule Mto Ruvu, walituletea milioni mia tano ambapo sasa hizo milioni mia tano zimeweza kujenga chanzo cha maji ambacho kitatupatia maji katika Mji wetu wa Korogwe. Ninachokiomba kwa Wizara ya Maji sasa, naomba sasa nipatiwe fedha kwa ajili ya miundombinu ambayo itafikisha maji kwenye maeneo hayo yote ambayo tumetengewa fedha kwenye mradi ule wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nilipoonana naye aliniambia watatutengea bilioni mbili ili ziweze kutusaidia kuweza kupata miundombinu ili kusudi ile miundombinu iweze kusambaza maji katika ule Mji wa Korogwe. Kwa hiyo, hayo ni maendeleo mazuri yanayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda. Niendelee kuipongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya ya kuhimiza suala la viwanda. Pale Korogwe tulikuwa na kiwanda cha matunda, katika suala la ubinafsishaji kiwanda kile kilibinafsishwa. Yule bwana aliyepewa kiwanda kile aliamua kuondoa mashine zote akahamia nazo Dar es Salaam, jengo lile limebaki gofu. Kitendo cha kuondoa zile mashine kimesababisha akinamama na vijana hasa ikizingatiwa Korogwe, ikizingatiwa Muheza tunalima sana matunda, yanaoza hakuna kwa kupeleka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Serikali yangu, kwa sababu jengo lile sasa limebaki ni gofu tuombe tupewe sisi Halmashauri ya Korogwe ili tuweze kulitumia kwa kuwawezesha akinamama na vijana waweze kutengeneza matunda kwa kutumia kile kiwanda, watengeneze juice kupitia kile kiwanda, viwanda vidogo vidogo ili kusudi waweze kujiwezesha kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la umeme wa REA. Naishukuru Serikali kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo. Nami kama mmoja wa watu ambao nina uhitaji na umeme wa REA niliomba nipatiwe umeme wa REA kwa kata zangu kama tano, sita hivi; Kata ya Kwamgumi, Kwamndolwa, Old Korogwe, Mtonga, Mgombezi na Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri niliongea nao wamenipokea vizuri sana na waliahidi kwamba watanisaidia ili niweze kufanikisha hili. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana yule Mkandarasi anasema vile vijiji havipo kwenye orodha yao. Kwa hiyo walikuwa wanaomba ikiwezekana wapelekewe hiyo orodha ili kusudi waweze kuanza kuifanya kazi ya kuweka umeme katika wilaya yetu au katika kata zile ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara; naipongeza TARURA, natofautiana kidogo na ndugu yangu maana yake mwenzangu yuko vijijini mimi niko mjini. TARURA kwangu kwa maana ya barabara inafanya kazi vizuri. Inafanya vizuri isipokuwa kwa sababu ni wilaya ya mjini, naomba barabara za mjini; nilimsikia Mheshimiwa Waziri juzi nilipokuwa nimeuliza swali la nyongeza alisema halmashauri za miji zimewekwa kama halmashauri 25 ambazo zitaanza kujengewa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati tunaendelea kusubiri mpango huo wanatengeneza kwa kiwango cha changarawe. Sasa niombe hawa wanaotengeneza kwa kiwango hiki cha changarawe, TARURA, watengewe mafungu kwa ajili ya kujenga hii mitaro, mifereji kwa mawe ili kusudi barabara hizi ziweze kudumu kwa muda mrefu wakati tunaendelea kusubiria habari ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu. Naishukuru Wizara ya Elimu ilinisaidia kunipatia fedha kwa ajili ya kujenga Maktaba ya Chuo cha Ualimu pale Korogwe, walinipatia milioni mia mbili na arobaini na tano. Naomba niwataarifu tu kwamba kazi inaendelea vizuri imefikia asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ile maktaba ikikamilika itatusaidia kwa watoto wetu, wanachuo pamoja na shule zetu za sekondari; ni maktaba kubwa ambayo nadhani hata nchini hapa atakayekuja kuifungua ataiona kwamba ni kubwa kuliko za maeneo mengine yote ambayo wamejenga zile maktaba…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.