Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami nina machache, najua mengi sana wameongea wenzangu lakini kuna machache ambayo ningependa kuongezea. Nafahamu kwamba kazi ya Bunge ni kuwatumikia wananchi na ni kwa ajili ya ustawi wa wananchi. Kama hivyo ndivyo basi, ina maana kwamba wananchi wangefurahi sana kuona kwamba tunawatetea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu moja tu. Huko mitaani sasa hivi wastaafu wana shida kubwa sana. Wastaafu waliostaafu tangu mwaka jana mwezi wa Julai hawajalipwa mafao yao mpaka sasa hivi. Nyumba hiyo unakuta baba na mama wamestaafu, nyumba hiyo hiyo ina vijana ambao wamesoma mpaka chuo kikuu lakini hawajaajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba Serikali inashughulikia ustawi wa wananchi lakini tuangalie jinsi ambavyo wastaafu hawa hawatendewi haki. Mstaafu anaenda kwenye Ofisi za Serikali kufuatilia mafao yake anaambiwa tunalipa waliostaafu mwezi wa Aprili, ni lini Serikali imeanza kuweka foleni ya wastaafu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu nina watu ambao ni jamaa zangu, majirani, wanajamii na wapiga kura wangu ambao wamestaafu mwezi wa saba mpaka sasa hivi ninavyoongea hawajalipwa mafao yao, wataishije? Januari wameshindwa kupeleka watoto shule sababu ni kwamba hawajapewa mafao. Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa mafao kwa wakati na sheria za ajira zinasema nini juu ya mfanyakazi anapomaliza kipindi chake cha kutumikia Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuna nia ya dhati ya kuinua uchumi huyu mtu ambaye tangu Julai mwaka jana hajapewa mafao yake, angekuwa amepewa angekuwa amejiendeleza kiasi gani? Tuna nia kweli ya kupunguza umaskini, hivi kweli Serikai itapunguza umaskini kwa njia hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa sisi ni Wabunge, hivi leo hii kama tungefika 2020 halafu tuambiwe kwamba mafao yetu tutalipwa 2021 tungekubali? Nauliza Wabunge ambao tupo kwenye Bunge hili, tungekubali 2021 ndiyo tulipwe mafao yetu? Kwa nini tunawafanya hivi wananchi ambao wametutuma mahali hapa kuwatumikia? Kwa nini hatuwasemei na kwa nini Mawaziri wanaohusika wanajua kabisa kwamba wafanyakazi hawa ambao wamelitumikia Taifa hili wameweza kutoa nguvu zao na muda wao, wamemaliza vyema lakini wanashindwa kuwapa stahili zao. Mtu anastaafu mwezi wa Julai, huu ni mwezi wa Aprili, hajapewa hata mafao yake, anaishije? Wanapata depression, wanakufa vifo ambavyo havitegemewi. Kwa nini lakini Serikali inafanya hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuja ku-wind up atuambie sheria zinasema nini na kinachofanyika ni nini? Je, hizi foleni ni mpango wa Serikali, ni Serikali haina fedha za kuwalipa au vinginevyo vyovyote vile atuambie ili tuweze kuelewa na tukawaambie kwamba Serikali sasa hivi inapangisha foleni wastaafu kwa sababu haina hela na kama hela zipo za kufanya mambo mengine kwa nini hazipo za kuwalipa wastaafu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo naomba niongee kuhusu elimu. Watu wote wameongelea kuhusu elimu lakini nilisikia siku moja Mheshimiwa Mkapa anasema kwamba tukae tuzungumze elimu inaenda wapi, tunaelekea wapi na elimu. Nami nataka niulize swali kwa sababu najua kabisa Waziri wa Elimu yupo hapa, atuambie, kuna kitu nilikisikia mijadala ikiendelea juu ya wanafunzi kukariri, tunaambiwa kwamba wasirudie madarasa. Naomba nipate ufafanuzi, hivi kama mwanafunzi amefika darasa la nne amefeli halafu anaendelea la tano huyo tunazalisha wasomi wa aina gani miaka ijayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea kujadili mjadala ambao uwazi kabisa na nini hasara ya kumfanya mwanafunzi akariri? Kama akirudia darasa Serikali inapata hasara gani badala ya kupata faida kupata mtu ambaye ni bora? Ni kwa sababu ya elimu bure tunataka wasiendelee kuwa wengi kwenye madarasa hayohayo wakati wengine wanaingia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itoe jibu ambalo litakuwa makini tuelewe kabisa kwamba Serikali inasema wanafunzi wasikariri kwa sababu inaogopa gharama itakayoingia kwa sababu itakuwa na wanafunzi wengi au sababu yoyote ya msingi ambayo itaonesha kwamba ni kweli Serikali imesema hivi kwa sababu hizi na hizi, vinginevyo tunaomba wakati ana-wind up atuambie ni nini kinataka kufanyika kwa Serikali na hii elimu kweli tuna nia ya dhati na elimu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulisoma, tulikuwa tunarudia mpaka mara sita, tuko hapa leo hii tunasema watoto wasirudie, darasa la nne aende mpaka la saba. Halafu akishafika la saba hajui kusoma na kuandika, akishakuwa hajui kusoma na kuandika anafanya nini au anakuwa wa kitu gani? Ningependa kusisitiza Serikali ipambanue huo mjadala unaoendelea. Kama kweli ni kutokukariri watupe sababu, kama kuna kukariri tutashukuru kwa sababu ndivyo tunavyohitaji iwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kuongelea ni kwamba, bajeti ya mwaka jana tuliongelea kwamba tunahitaji tozo ile ya mafuta iende kwenye maji. Ni jambo jema na tuliona ni jema kweli, lakini kama imeshaenda tangu wakati huo, hatujui kwamba ilienda ngapi kwa sababu hatujaona imeenda ngapi lakini cha muhimu ni kwamba ikienda kule inafanya yale matarajio na kama haifanyi yale matarajio sababu ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa kwangu mimi kule Kibaha, niliandika swali kuuliza kwamba miradi ya Kibaha inajengwa chini ya kiwango, wananchi wa Kibaha wanakosa maji siyo kwa sababu hela hazijatolewa. Ilitolewa shilingi milioni 531 mradi wa maji, vikao, imepotelea yote porini kwa sababu mabomba yamewekwa mabovu na hayako kwenye viwango, badala ya kuweka connector kachomelea moto, sehemu nyingine kafunga mipira ikawa maji yanamwagika, mradi ukakataliwa na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukataliwa na wananchi ukarudishwa Halmashauri, wana miezi nane mpaka sasa hivi watu wa Vikawe hawapati maji, lakini Serikali ilishatoa shilingi milioni 530 lakini zimepotea kwa sababu watendaji wamekula zile hela. Tangu siku ile niliyosema Serikali haikufanya kitu chochote mpaka sasa hivi ninaposema ni miezi nane, ukienda Vikawe hakuna maji na shilingi milioni 531 zilishaliwa, tunaelekea wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la wajasiriamali wadogo wadogo wanaoinua maisha yao. Kwa kweli Waziri wa Viwanda alisema kwamba tuanzishe viwanda vidogo vidogo, wanawake wajasiriamali wameanzisha, wengine wanasindika spices lakini tatizo ambalo limetokea ni kwamba tozo ndogo ndogo kwenye viwanda vidogo vya wajasiriamali ni nyingi mno. Mtu anatengeneza spice anaambiwa anatakiwa apate usajili TFDA, anatakiwa aende OSHA, anatakiwa aende TBS, wote hao wanachukua hela za huyu huyu mjasiriamali mdogo ambaye ndiyo kwanza anahangaikia maisha yake tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hivi vitu vyote visiwekwe pamoja gharama zipunguzwe ili hawa wajasiriamali waweze kupata faida. Inafikia mahali wajasiriamali wanakata tamaa, wanaona kwamba hawapati kitu chochote. Tutaendelea kuzalisha maskini kwa sababu tu Serikali imeweka mlolongo wa tozo ambazo zingeweza zikawekwa pamoja na zikaleta faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ningependa kuzungumzia jinsi ambavyo viwanda tumevipokea sawa, kuna mwenzangu mmoja ameongelea, lakini kuna tatizo ukaguzi wa viwanda na shughuli zinazofanywa katika viwanda hivyo. Hawa vijana wetu tumesema watapata ajira, sawa, lakini mwisho wa siku tunazalisha magonjwa ambayo Serikali itaingia tena hasara ya kutibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kiwanda pale Kibaha kinazalisha sabuni, vijana wameajiriwa lakini hamna vitendea kazi, hamna mask, wanafanya kazi vumbi za sabuni zote zinaishia kwa vijana hawa. Vijana hawa wanaishia kuwa na TB… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)