Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima anaotujalia. Nichukue nafasi hii pia kuishukuru Serikali, Mheshimiwa Rais na uongozi wa Bunge kuniwezesha kwenda kutibiwa India na leo nimepona. Najisikia niko vizuri, namshukuru sana Mungu. Naishukuru sana Serikali yangu kwa huruma hiyo na sasa niko kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapema kabisa naunga mkono hotuba iliyotolewa na Waziri Mkuu hapa mbele yetu kwa sababu imejaribu kuangalia maeneo muhimu mengi. Kusema kweli Waziri Mkuu na viongozi wanaomsaidia akiwemo Waziri Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Mawaziri wengine, wanafanya kazi vizuri na wanatusikiliza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja chache ambazo naziwasilisha hapa Bungeni. La kwanza, ni suala la shamba la Milundikwa ambalo nimekuwa nikilizungumza sana katika Bunge hilo. Shamba hili lilikuwa la Serikali na lina ukubwa wa ekari 26,500 baada ya kuacha shughuli zake wakaja Jeshi kwa muda. Wanajeshi walikuja mwaka 1994 baadaye walisimamisha shughuli zao na kuwaachia wananchi. Shamba lile liligawanywa katika vijiji mbalimbali, Kijiji cha Milundikwa kilipewa ekari 12,000, Kasu walipewa ekari 6,000, Kisulu walipewa ekari 2,000, Malongo walipewa ekari 1,000 na zikawa zimebaki ekari 5,500, tukashauriwa eneo hilo libaki kuwa eneo la Halmashauri tuendeleze utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwa busara na namna walivyofanya wakaamua eneo hili kuanzisha Sekondari ya Milundikwa ambayo nayo niliipigia kelele sana hapa kwamba Serikali ilitwaa, lakini lazima nishukuru kwamba Serikali ilikwishatoa pesa nyingi zaidi ya shilingi milioni
360 na sasa tunaendeleza sekondari nyingine japo miundombinu bado haijatosha, tutaendelea kuiomba Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida yangu ni nini? Wanajeshi walivyoingia kwenye eneo hili sisi tulidhani watachukua eneo hili la ekari 5,500 ambalo lilibaki kwa Halmashauri badala yake wamedai eneo lote lililokuwa shamba la Milundikwa ambalo wananchi wa vijiji nilivyovitaja vyote walipewa kwa barua na kwa maelekezo ya mkoa na mimi wakati huo nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilienda kutembelea kwenye vijiji hivi ni kilio, wananchi hawana mahali pa kulima na wamefukuzwa katika maeneo yao, wamebakiwa na ekari 4,000 tu. Kwa hiyo, takriban wananchi 5,000 hawana mahali pa kulima na ni wakulima. Habari hii nimewahi kuipeleka kwenye Ofisi yake Mheshimiwa Waziri, nimeshapeleka pia Ofisi ya Waziri Mkuu, jambo hili nimekuwa nalizungumza peke yangu sijaona kama naungwa mkono na mtu yeyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nimejaribu kuliongea kwenye vikao vya mkoa, nikaambiwa nisiendelee kuongea hilo ni uamuzi wa Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kwanza ni mtu mwenye huruma. Inawezekana sisi wote hatusemi lugha moja, tukilifafanua jambo hili na athari zinazoonekana kwa wananchi, naamini kabisa Mheshimiwa Rais ataona umuhimu wa kuligawa eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanajeshi hatuwakatai wapate eneo lao na wananchi ambao ni wapiga kura wetu lakini ndiyo wakulima na hawana namna nyingine ya kujikimu ni kutegemea kilimo waweze kupata eneo la kulima. Naomba hili lichukuliwe kwa umuhimu wa pekee kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la elimu. Wilaya yetu ya Nkasi chini ya Mkuu wetu wa Wilaya Said Mtanda, wengi wanamfahamu, tumekuja na sera ya kuitikia kwa vitendo elimu bure. Tumejenga madarasa matatu matatu kwa kile eneo ambapo kuna shule ya msingi na sasa tuna madarasa zaidi ya 348, lakini wananchi hawana uwezo wa kuezeka, wananchi wameshaitikia vizuri, wametimiza wajibu wao. Naiomba Serikali, kwa namna yoyote mtakavyoweza kutusaidia ili wananchi wasivunjike moyo tuweze kumaliza kuezeka madarasa haya ili yaweze kuleta maana ya kuhamasisha wananchi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la lingine ni afya. Nchini kwetu kuna sera mbalimbali na nashukuru sana jana katika swali langu, kusikia kwamba Serikali imekubali sasa ombi letu la muda mrefu mimi na Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Ally Keissy la kujenga Hospitali ya Wilaya katika Wilaya ya Nkasi. Jambo hili ni faraja kwetu, tumelipokea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado vituo vya afya tumekuwa tukivijenga kila mahali. Kwenye Jimbo langu wananchi wanajenga vituo vya afya vinne, tumewahamasisha. Licha ya ahadi tuliyoipata jana lakini bado kuna vituo vya afya vitatu na zahanati zaidi ya 15, zote hizi tumewahamasisha wananchi na sasa wanatimiza wajibu wao, lakini tunaomba Serikali iweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la umeme. Katika vijiji vyetu imeonekana tutapelekewa umeme katika vijiji karibu vyote lakini wakandarasi wamechelewa. Kuna eneo muhimu sana ambalo nafikiri kama inawezekana wakandarasi waanzie ambapo ni Vijiji vya Sintali, Nkana na Mkunachindo. Vijiji hivi vilisahaulika mara ya kwanza, vikisaulika mara ya pili tena inaweza kuwa sio vizuri sana. Naomba sana hilo liangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya watumishi ambao leo hii tunaambiwa utumishi wao usitishwe kwa sababu wana elimu ya darasa la saba. Jambo hili ni maumivu makubwa sana. Nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri karibu miaka 17, nimeshirikiana na hawa kujenga Wilaya ya Nkasi, kujenga zaidi ya sekondari 23 na sasa niko Mbunge, naendelea kushirikiana nao. Unapowaambia wanaondoka bila kufahamu au kutambua juhudi ambazo wamechangia kwenye maendeleo ya Wilaya, Serikali na wananchi kwa ujumla hii ni dhambi. Hivyo, naiomba Serikali hii sikivu na yenye huruma iweze kuliangalia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo kwetu ndiyo alfa na omega na kwenye hotuba hii nimeona maendeleo ya kilimo na juhudi zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuunganisha matrekta. Ni juhudi nzuri zinazotupeleka kwenye kilimo ambacho kitaleta tija zaidi kwa sababu tunatumia mashine. Hata hivyo, uunganishaji huu ungefanyika hata Mkoa wa Rukwa ambako tunalima, pengine ingependeza zaidi kulikoni tunafanyia sehemu ambayo hata kilimo hakifanikiwi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile changamoto za kilimo amezieleza mwenzangu hapa ni kwamba sisi Mkoa wa Rukwa msimu wetu wa kulima unaanza Oktoba, mbolea tunapata mwezi Februari, suala hili ni kilio kwa wakulima. Nilifanya ziara hivi karibuni, kwa kweli ni kilio. Naomba Waziri na Serikali itambue, nchi hii ni kubwa, inawezekana hatujui misimu mbalimbali, sisi kwetu tunahitaji pembejeo zitufikie Septemba ndiyo tutaweza kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mtuhakikishie pembejeo hizi zinapatikana kwa wingi. Mwaka huu pamoja na Mheshimiwa Rais kuingilia kati jambo hili lakini bado pembejeo ziliisha ikabaki wakulima wanalima bila pembejeo na sasa hivi sisi Mkoa wa Rukwa chakula hakitakuwa kingi sana kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile masoko ni muhimu sana. Tulitembelea Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko huko Iringa, pamoja na majukumu mengine kumbe kuna jambo muhimu ambapo ingeweza kuwasaidia wakulima. Wajibu wake ni pamoja na kutafuta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.